MABADILIKO YA TABIANCHI YANAVYOATHIRI BEI YA SAMAKI ZNZ, JAMII INA WAJIBU WA KULINDA RASILIMALI ZA BAHARI
Kupanda kwa joto la bahari na kuharibika kwa mazingira ya mazalia ya samaki kunaweza kuathiri uzalishaji, kipato cha wavuvi na upatikanaji wa kitoweo kwa wananchi.
Na Maryam Nassor
Kwa muda mrefu, samaki wamekuwa sehemu muhimu ya chakula na maisha ya
wananchi wengi wa Zanzibar, hususan wanaoishi katika maeneo ya mwambao ambao
hutegemea rasilimali za bahari kwa chakula, kipato na shughuli mbalimbali za
kiuchumi.
Katika kipindi cha hivi karibuni,
kupanda kwa bei ya samaki kumeanza kuwa changamoto kwa familia nyingi, hasa
zile zenye kipato cha chini ambazo zinategemea samaki kama chanzo muhimu cha
protini katika milo yao ya kila siku.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi wanalazimika kubadili aina ya
kitoweo kwa kuchagua vyakula wanavyoweza kumudu, huku dagaa wakigeuka kuwa
miongoni mwa machaguo yanayopatikana kwa gharama nafuu zaidi.
Hali hiyo inaibua maswali kuhusu mustakabali wa rasilimali za bahari na
uhusiano wake na maisha ya wananchi, hususan wakati dunia ikiendelea kukabiliwa
na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Mabadiliko ya tabianchi si suala linalohusu ongezeko la joto na
mabadiliko ya misimu pekee, bali yana athari katika mifumo ya uzalishaji wa
chakula, uchumi na upatikanaji wa rasilimali za asili.
Kwa upande wa bahari, ongezeko la joto la maji, mabadiliko ya mikondo ya
bahari na kuharibika kwa mazingira ya matumbawe ni miongoni mwa changamoto
zinazoweza kuathiri makazi, mazalia na usambazaji wa samaki.
Utafiti uliochapishwa katika jarida la kisayansi kuhusu mazingira na
uvuvi Zanzibar unaonesha kuwa mabadiliko hayo ni miongoni mwa changamoto
zinazoweza kuathiri upatikanaji na uzalishaji wa samaki.
Aidha, taarifa iliyochapishwa na gazeti la The Citizen Machi 13, 2025,
inaeleza kuwa Uchumi wa Buluu Zanzibar unakabiliwa na hatari zinazohusiana na
mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo kupanda kwa kina cha bahari, mmomonyoko wa
fukwe na matukio ya hali mbaya ya hewa.
Hali hiyo inaonesha kuwa kulinda bahari si suala la kuhifadhi mazingira
pekee, bali ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika
na rasilimali hizo kwa chakula, kipato na maendeleo ya kiuchumi.
MABADILIKO YA BAHARI YANAATHIRI MAISHA
YA WANANCHI
Athari za mabadiliko ya mazingira ya bahari zina umuhimu wa kuangaliwa
kwa karibu kutokana na utegemezi wa wananchi wengi wa Zanzibar kwa rasilimali
hizo.
Kwa baadhi ya familia, samaki si kitoweo cha kawaida tu, bali ni sehemu
ya lishe na utamaduni wao wa chakula. Hivyo, kupanda kwa bei yake kunaweza
kuathiri uwezo wa kaya kupata chakula chenye virutubisho muhimu.
Fadhili Abdallah, mkazi wa Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja,
anasema kupanda kwa bei ya samaki kumeifanya familia yake kupata changamoto
katika kumudu kitoweo hicho licha ya Serikali kuendelea kuimarisha Uchumi wa
Buluu.
"Kiukweli, licha ya Serikali kuimarisha Uchumi wa Buluu, kitoweo
kimekuwa bei kubwa kwa mwananchi wa kawaida. Hatuwezi tena kumudu kula samaki,
tunaambulia kula dagaa tonge," anasema.
Anaeleza kuwa hali hiyo inawaathiri zaidi wanawake ambao katika familia
nyingi wana jukumu kubwa la kupanga matumizi ya fedha za nyumbani na
kuhakikisha familia zinapata chakula.
Kwa upande wake, Mtumwa Omar kutoka Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja,
anasema upatikanaji wa samaki na uwezo wa wananchi kuununua umebadilika
ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Anasema kupanda kwa gharama za mahitaji mengine ya nyumbani kunafanya
baadhi ya familia kushindwa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kununua
samaki.
"Awali, watu wa Kaskazini walikuwa wanakula samaki kwa wingi, lakini
kwa sasa hali ni tofauti. Ukishanunua mahitaji mengine ya chakula kama mchele
na nazi, inakuwa vigumu tena kutoa shilingi 5,000 mpaka 20,000 kununua samaki
ambao wakati mwingine hawatoshi kwa familia nzima. Mwishowe unaishia kula mboga
au dagaa," anasema.
Uzoefu wa wananchi hao unaonesha namna mabadiliko ya gharama za chakula
yanavyoweza kuathiri uchaguzi wa lishe katika kaya, hasa zile zinazotegemea
kipato cha kila siku.
Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kuwa kupanda kwa bei ya samaki
hakusababishwi na mabadiliko ya tabianchi pekee. Mahitaji ya soko, gharama za
uvuvi, usafirishaji na mfumo wa usambazaji pia vina nafasi katika mwenendo wa
bei.
WAVUVI NAO WANAKABILIWA NA CHANGAMOTO
ZA MAZINGIRA YA BAHARI
Wakati wananchi wakikabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei ya samaki,
wavuvi nao wanakabiliwa na mabadiliko ya mazingira yanayoweza kuathiri shughuli
zao za kila siku.
Makame Vuai Juma, mvuvi kutoka Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja, anasema
baadhi ya wavuvi wanalazimika kwenda maeneo yenye kina kirefu cha bahari
kutafuta samaki kutokana na mabadiliko ya mazingira ya bahari.
Anasema, ongezeko la joto la maji
linaweza kuathiri upatikanaji wa baadhi ya samaki katika maeneo ya karibu na
mwambao.
"Mabadiliko ya tabianchi yamepelekea kwenda kuvua kina kirefu cha
bahari kutokana na joto kuongezeka baharini, hali inayosababisha samaki
kutopatikana kwa urahisi katika maji ya karibu na mwambao," anasema.
Hata hivyo, anabainisha kuwa ongezeko la mahitaji ya samaki kutokana na
kukua kwa shughuli za utalii katika maeneo ya Kaskazini Unguja nalo linachangia
kupanda kwa bei ya kitoweo hicho.
Maelezo hayo yanaonesha kuwa changamoto ya upatikanaji na bei ya samaki
ina sura mbalimbali zinazohitaji kuangaliwa kwa pamoja.
Mabadiliko ya mazingira ya bahari yanaweza kuathiri maeneo ya uvuvi, huku
gharama za shughuli hizo na ongezeko la mahitaji ya soko vikiongeza changamoto
kwa wavuvi na wananchi wanaotegemea samaki.
Anasema , kuna umuhimu wa kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu uhusiano kati
ya afya ya bahari, shughuli za uvuvi na usalama wa chakula.
TAKWIMU ZA UVUVI NA UMUHIMU WA
KUZIELEWA
Pamoja na malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya samaki,
takwimu za Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar zinaonesha kuwa
uzalishaji wa samaki katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ uliongezeka kutoka tani
5,437 mwaka 2022 hadi tani 8,525 mwaka 2023.
Aidha, thamani ya samaki waliovuliwa katika wilaya hiyo iliongezeka
kutoka shilingi bilioni 34.875 mwaka 2022 hadi shilingi bilioni 59.408 mwaka
2023.
Takwimu hizo zinaonesha ongezeko la uzalishaji na thamani ya samaki,
lakini ongezeko hilo halimaanishi moja kwa moja kuwa kila mwananchi atanufaika
kwa kupata samaki kwa bei nafuu.
Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Haji Abdallah, anasema
pamoja na ongezeko la uzalishaji, bei ya samaki bado iko juu kutokana na
changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hiyo.
Anasema mabadiliko ya mazingira ya bahari ni miongoni mwa mambo
yanayochangia wavuvi kulazimika kwenda maeneo yenye kina kirefu kutafuta
samaki.
Anaeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa boti za
kisasa kwa wavuvi ili kuimarisha shughuli zao, lakini wananchi wa kawaida bado
wanakabiliwa na changamoto ya kumudu bei ya samaki.
"Kutokana na kupanda kwa bei ya samaki, wakati mwingine ni bora
kununua kilo ya nyama ya ng’ombe kwa sababu ni rahisi kuliko samaki. Mahitaji
ya samaki yamekuwa makubwa kutokana na uwepo wa hoteli kubwa za watalii, hivyo
wananchi wa kawaida wanashindwa kuhimili bei hiyo," anasema.
Aidha, anasema uwepo wa hoteli nyingi katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’
umeongeza mahitaji ya samaki, huku baadhi ya boti za uvuvi zikiuza samaki moja
kwa moja kwa hoteli hizo.
Hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usambazaji na
biashara ya samaki ili kuhakikisha wananchi wa kawaida wanapata fursa ya
kunufaika na rasilimali za bahari.
Kwa msingi huo, ni muhimu takwimu za uzalishaji wa samaki ziende sambamba
na taarifa kuhusu upatikanaji wa samaki katika masoko, mwenendo wa bei na uwezo
wa wananchi kuzinunua.
UCHUMI WA BULUU UNAHITAJI KWENDA
SAMBAMBA NA UHIFADHI WA BAHARI
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuwekeza katika kuimarisha
Uchumi wa Buluu kupitia sekta ya uvuvi, utoaji wa vifaa vya kisasa, ujenzi wa
masoko ya samaki na kuongeza uwezo wa wavuvi kufanya shughuli zao kwa tija.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali
Mwinyi, katika kueleza mafanikio ya Serikali, alitaja utoaji wa zaidi ya boti
1,000 kwa ajili ya kusaidia shughuli za uvuvi na kilimo cha mwani, hatua
iliyonufaisha takribani watu 32,000.
Jitihada hizo zinalenga kuongeza uzalishaji, kupanua fursa za ajira na
kuimarisha kipato cha wananchi wanaotegemea rasilimali za bahari.
Aidha, katika maelezo yake kuhusu kuimarisha Uchumi wa Buluu Oktoba 2025,
Rais Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kujenga masoko ya kisasa ya samaki na
kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya baharini ili kuongeza manufaa kwa
wananchi.
Hata hivyo, pamoja na uwekezaji huo, kuna umuhimu wa kuhakikisha
maendeleo ya sekta ya uvuvi yanaambatana na mikakati madhubuti ya kuhifadhi
mazingira ya bahari.
JAMII INA WAJIBU WA KULINDA RASILIMALI
ZA BAHARI
Kulinda bahari si jukumu la Serikali na wataalamu wa mazingira pekee,
bali ni wajibu wa kila mwananchi, wavuvi, wafanyabiashara wa samaki na jamii
kwa ujumla.
Kila mmoja ana nafasi ya kuchangia katika kuhakikisha mazingira ya bahari
yanahifadhiwa ili kuendeleza upatikanaji wa samaki kwa sasa na vizazi vijavyo.
Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Haji Abdallah, anasema
jamii inapaswa kushiriki katika kulinda na kurejesha mikoko kutokana na umuhimu
wake katika mazingira ya pwani.
Anaeleza kuwa mikoko hutoa maeneo muhimu ya kujificha na kukua kwa baadhi
ya viumbe vya baharini, hivyo uharibifu wake unaweza kuathiri mifumo ya maisha
ya viumbe hao.
Aidha, anasema wananchi wanapaswa kushirikiana katika kuhifadhi matumbawe
na kuepuka shughuli zinazoweza kuyaharibu, kwa kuwa ni sehemu muhimu ya makazi
ya aina mbalimbali za viumbe wa baharini.
Anasisitiza pia umuhimu wa wavuvi kuzingatia sheria na taratibu za uvuvi
endelevu, ikiwemo kuepuka njia haramu zinazoweza kuharibu mazalia ya samaki na
kupunguza rasilimali za bahari.
“Ni muhimu kuimarisha tafiti na mifumo ya ukusanyaji wa takwimu za uvuvi
katika kila wilaya ili kufuatilia mabadiliko ya uzalishaji, aina za samaki
wanaopatikana, mwenendo wa bei na changamoto zinazowakabili wavuvi.” Anashauri .
Anasema jamii inapaswa kuimarisha
ushiriki wake katika shughuli za usafi wa fukwe, upandaji na utunzaji wa
mikoko, pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu vitendo vinavyoharibu
mazingira ya bahari.
Anasema kuwa, Ni muhimu kuelewa kuwa kila taka inayotupwa baharini, kila
eneo la mikoko linaloharibiwa na kila kitendo kinachoharibu mazingira ya
matumbawe kinaweza kuongeza changamoto katika mifumo ya maisha ya viumbe wa
baharini.
Anasema , Kulinda bahari ni
kulinda chakula, kipato na maisha ya wananchi Rasilimali za bahari si urithi wa
kizazi kimoja, bali ni tunu inayopaswa kuhifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya
sasa na vijavyo.

Post a Comment