MIMBA ZA UTOTONI ZINAENDELEA KUWANYIMA WASICHANA NDOTO ZAO.

 Ukosefu wa elimu ya Afya ya uzazi inachangia kwa kiasi kikubwa  kuongezeka kwa mimba za utotoni hasa maeneo ya  vijijini.

Na Maryam Nassor

Kila mwaka,  wasichana milioni  21 wenye umri wa  kati  ya miaka 15 hadi 19 wanapata ujauzito katika nchi zinazoendelea

Kwa  mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani ( WHO)  ya mwaka 2020 inaonesha  asilimia kubwa , ya  matukio hayo hutokea katika nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara  ambako viwango vya uzazi kwa wasichana  na wanawake vinazidi kuwa juu.

 Kwa hapa  Tanzania, takwimu  zinaonesha kuwa tatizo la mimba za utotoni bado linaendelea kuwa changamoto kubwa, inayowakabili wasichana wengi nchini. Kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Afya na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS-MIS) ya mwaka 2015/2016,.

Takribani asilimia 27 ya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 tayari walikuwa wameanza kuzaa au walishawahi kupata ujauzito, hali inayochangia kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaoacha shule na kukosa fursa za kutimiza ndoto zao za maisha.

 Kwa mujibu wa UN Women ,katika ripoti yake ya mwaka 2025 kuhusu haki za wasichana balehe duniani, mimba za utotoni zinaendelea kuwa moja ya vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya mtoto wa kike, kwani huwanyima wasichana haki ya elimu, afya bora na ushiriki  duni katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.,

 Shirika hilo, linaeleza kuwa wasichana wanaopata ujauzito katika umri mdogo wako katika hatari kubwa ya umaskini, ukatili wa kijinsia pamoja na kupata  changamoto za afya ya uzazi.

 Kwa  hapa Zanzibar , Katika baadhi ya maeneo ya vijijini, wasichana wengi wamejikuta wakiacha masomo kutokana na ujauzito wa mapema, huku wengine wakikumbana na changamoto za kiafya, kisaikolojia na hata kutengwa na jamii.

 Akizungumza na  mwandishi wa Makala hii , msichana  mdogo Amina (si jina lake halisi), mwenye umri wa miaka 16 kutoka kijiji cha Matemwe  wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja , anasema maisha yake yalibadilika ghafla baada ya kupata ujauzito akiwa mwanafunzi wa kidato cha pili   mwaka 2024.

“Nilikuwa nina ndoto ya  kuwa muuguzi, lakini baada ya kupata mimba nililazimika kuacha shule. Marafiki waliniacha na hata baadhi ya ndugu walinitenga ,” anasimulia  kwa huzuni.

Amina anasema ,hakuwahi kupata elimu ya kutosha kuhusu afya ya uzazi, jambo ambalo linaonekana kuwa chanzo kikubwa cha tatizo kwa  wasichana  wengi hasa wa vijijini.

Kesi nyingine ni ya Zainabu (si jina lake halisi), msichana  mwenye miaka 15 kutoka Nungwi, ambaye alipata ujauzito baada ya kushawishiwa na mwanamme aliyemuahidi kumsaidia mahitaji yake ya skuli.

“Nilikubali kwa sababu nyumbani hali ilikuwa ngumu ,Sikujua kama mwisho wake ungekuwa hivi ,” anasema kwa masikitiko.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Matemwe  Mkoa wa Kaskazini Unguja, Makame Sheha Mdacho, tatizo hilo limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka.

 Anasema, baadhi ya wanafunzi wa kike hushindwa kuendelea na masomo kutokana na mazingira magumu ya kifamilia pamoja na ukosefu wa elimu sahihi ya afya ya uzazi.

Anasema kuwa, maeneo ya Matemwe vijana wadogo  wa kiume wanamiliki dola, ( pesa za kimarekani) kutokana na kuimarika kwa shughuli za kiutalii ,  hivyo imekuwa rahisi kuwarubuni Watoto wakike  hasa wanafunzi ambao hawajajielewa na bado  wako shuleni.

“ Skuli zimekuwa zikijaribu kutoa elimu ya maadili na afya ya uzazi kwa wanafunzi , lakini bado juhudi zaidi zinahitajika kutoka  kwa wazazi na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha Watoto wakike wanafikia ndoto zao za kielimu” amesema.

Nuru Abdalla,  mzazi kutoka  Shehia ya Matemwe Kusini  anasema,  mabadiliko ya teknolojia pamoja na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yamechangia kuongezeka kwa mimba za utotoni.

 Anasema kuwa,  baadhi ya watoto hutumia simu bila uangalizi, hali inayowafanya kujiingiza katika mahusiano yasiyofaa mapema.

“Tunajaribu kuwaelekeza watoto wetu lakini mazingira ya sasa ni magumu Tunahitaji ushirikiano mkubwa  wa pamoja kati ya wazazi na viongozi wetu wa Serikali ,” anasema.

Kwa upande wake Shinuna Said Mtaalamu  wa Afya ya Uzazi  kutoka Hospitali ya Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’Unguja anasema mimba za utotoni zina madhara makubwa kiafya kwa wasichana wadogo.

Anasema  kuwa, wasichana wenye umri mdogo wako katika hatari kubwa ya kupata matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua ukizingatia viungo vyao bado havijakomaa.

“Miili yao bado haijakomaa vizuri kubeba mimba, wengine hupata upungufu wa damu, Presha ya mimba au hata matatizo wakati wa kujifungua,” anasema.

Aidha, ameeleza kuwa baadhi ya wasichana hupata msongo wa mawazo kutokana na kukataliwa na familia au jamii baada ya kupata ujauzito .

Mtaalamu huyo , anaeleza  umuhimu wa  kuwapa wasichana elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi, kuwajengea mazingira salama ya kujifunzia pamoja na kuwawezesha kiuchumi wazazi kunaweza kusaidia kupunguza tatizo hilo.

 Naye, Afisa wa Ustawi wa Jamii kutoka Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja Tatma Adam  anasema juhudi mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa ili kupunguza tatizo hilo, ikiwemo kutoa elimu kwa jamii, kuwasaidia watoto waliopata changamoto pamoja na kushirikiana na taasisi mbalimbali za kiraia.

 Anasema ,tatizo la mimba za utotoni linaendelea kuwa changamoto kubwa inayohitaji hatua za haraka. Bila juhudi za pamoja, wasichana wengi wataendelea kunyimwa haki yao ya elimu na fursa za kutimiza ndoto zao.

Sheikh Nahoda Haji kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja, anasema jamii ina wajibu wa kuhakikisha watoto wanapata malezi bora pamoja na mafunzo ya maadili tangu wakiwa wadogo.

“Mtoto wa kike anahitaji kulindwa na kupewa nafasi ya kutimiza ndoto zake, kwani  elimu ni msingi wa maisha yake ya sasa na  baadaye,” anasema.

Aidha, amehimiza kuacha kuwanyanyapaa wasichana waliopata ujauzito na badala yake kuwapa msaada wa kisaikolojia na kijamii ili waweze kuendelea na maisha yao na kuendelea na masomo yao.

 Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ )  ni Asasi inayotetea haki za wanawake na watoto ,  Afisa Programu  wa kupambana  na Ukatili  na  Unyanyasaji  wa Mwanamke na Mtoto wa kike (VAWG)  Asya Hakim   amesisitiza   umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi kwa wanawake  na wasichana pamoja na kuimarisha malezi ya watoto.

Afisa huyo amesema kuwa, lengo la mradi huo ni kuwajengea uwezo waandishi wa Habari kuripoti  matukio mbali mbali ya udhalilishaji hasa vijijini ambako bado wanajamii hawana uwelewa na mwamko wa kuyaripoti.

 Mradi huo,  wa ‘ Tunaweza Pamoja ’ unaotekelezwa na UN Women kwa kushirikiana na  TAMWA ZNZ ambao umefadhiliwa na  Norway chini ya mpango wa Pamoja wa umoja wa Mataifa, unaolenga  kujenga jamii yenye  usawa na isiyovumilia ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

No comments

Powered by Blogger.