WANAFUNZI WA IITMZ KUNUFAIKA NA MAFUNZO YA VITENDO KUPITIA USHIRIKIANO NA VIGOR

Na Mwatima Issa – IITMZ

Taasisi ya Teknlojia ya India Madras Kampasi ya Zanzibar (IITMZ) inaendeleza kutimiza lengo lake la kuhitimisha wataalamu wanaokubalika katika soko la ajira la Kimataifa, Hayo yameibuka katika kikao cha mazungumzo ya pamoja kilichofanyika baina ya uongozi wa IITMZ na kampuni ya Vigor Group of Campanies kilichofanyika katika ofisi za Vigor Migombani mapema wiki hii.

Akizunguma katika kikao hicho Mkuu wa Taaluma wa Taasisi ya IITMZ Prof. Suresh Akhihebbal amesema itakuwa ni jambo jema wanafunzi wa IITMZ kutumia taaluma yao ya Akili Unde na Uhandisi wa viwanda kwa kuwa sehemu wa uzalishaji katika miradi mbalimbali  inayosimamiwa na kuendeshwa na  Kampuni ya VIGOR hasa ikizingatiwa kuwa wamefikia hatua ya kutoa mchango wao wa moja kwa moja katika soko la ajira.

Ameendeza kwa kusema kuwa, kwa sasa wanafunzi ya IITMZ wameanza kutumika katika taasisi mbalimbali kusaidia katika uendeshaji na uzalishaji wa mifumo ikiwa ndio sehemu kubwa ya taaluma yao kadhalika kuibua miradi kadhaa yenye tija katika katika taasisi hizo. Aidha amethibithisha kua  hayo hujitokeza katika mafunzo ya vitendo wanayoshiriki kila wakati wa mapumziko yao ya muhula wa masomo ya darasani.

Prof. Suresh ameithibitishia VIGOR kuwa mbali na vijana hao kubakiwa na muda mfupi tu hadi kuhitimu mafunzo yao ya Shahada ya kwanza ya miaka minne ifikapo mwezi Julai mwaka 2027, IITMZ itahakikisha wanatumia elimu waliyoipata kuleta mchango chanya katika maendeleo ya jamii, sekta ya teknolojia na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Amesema taasisi hiyo itaendelea kuwajengea uwezo wa kitaaluma, ubunifu na uongozi ili wawe wataalamu wenye ushindani wa kimataifa na wenye uwezo wa kutoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali za kisasa.

Naye Mtendaji Mkuu, wa Mradi wa ONIRIA kupitia Kampuni ya VIGOR Yulia Baystrukova ameonesha furaha yake ya wasaa wa mazungumzo hayo na IITMZ na kusema fursa ya uwasilishaji wa  shughuli za uzalishaji viwandani pamoja na dira ya uwekezaji wa mradi wa ONIRIA  uliofanyika katika kikao hicho ni ya matumaini.

Amesema ‘Tumefurahishwa sana na majadiliano yaliyofanyika, ambayo yameonesha uwepo wa nafasi kubwa ya kujenga ushirikiano wa muda mrefu na wenye manufaa kati ya IITM Zanzibar na VIGOR Group katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, ubunifu na teknolojia”.

Aidha  Baystrukova amethibisha,  kujenga na kuendeleza ushirikiano huu unaolenga kutoa fursa muhimu ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi kupitia uelewa wa moja kwa moja wa shughuli halisi za uzalishaji viwandani, mifumo ya uzalishaji, usafirishaji wa bidhaa, udhibiti wa ubora pamoja na michakato mbalimbali ya viwandani, hususan kwa programu za Uhandisi wa Kemikali na taaluma nyingine zinazohusiana.

Wakati huo huo, amethibitisha ushiriki wa tukio la IITMZ la linalotarajiwa kufanyika fanyika tarehe 9 Juni pamoja na wawakilishi kutoka viwanda na taasisi mbalimbali za uzalishaji. Tukio hilo litakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya uzalishaji na viwanda linalenga  kuzindua programu mpya ya Shahada ya Sayansi katika masuala ya Uhandisi wa Michakato ya Kemikali (BS in Chemical Process Engineering) katika Kampasi ya IITM Madras Zanzibar.

Lengo la tukio hili ni kuwasilisha vipengele muhimu vya programu hiyo pamoja na kupokea maoni na mapendekezo kuhusu maeneo mbalimbali yanayohusiana nayo. Aidha, tukio hilo litapambwa na mada mbalimbali zitakazowasilishwa na viongozi kutoka sekta za viwanda na taaluma za kitaaluma.

Kikao hicho cha mashirikiano ya kiutendaji kimebainisha vipengele vya kimashirikiano katika kuendeleza utendaji kazi wa pamoja wa IITMZ na Kampuni ya VIGOR. Maeneo hayo ni uendeshaji wa ziara za viwandani kwa ajili ya kuwajengea wanafunzi uzoefu wa moja kwa moja katika mazingira halisi ya uzalishaji, pamoja na programu za udhamini wa elimu na mafunzo maalum kwa viongozi na wataalamu.

Aidha, ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha shughuli za michezo na maendeleo ya kijamii, huku pia ukitoa nafasi za mafunzo kwa vitendo (internships) na kukuza ubunifu kupitia miradi ya pamoja kati ya sekta ya elimu na viwanda.

               

Watendaji wa Taasisi ya Teknlojia ya India Madras Kampasi ya Zanzibar (IITMZ) wakifatilia uwasilishaji wa Taarifa ya za uendeshaji wa Miradi mbalimbali inayosimamiwa na kuendeshwa na Kampuni ya VIGOR Group of Companies kufuatia ziara fupi iliyofanywa na viongozi hao wa IITMZ katika ofisi za kampuni hiyo huko Migombani mapema wiki hii.

 

No comments

Powered by Blogger.