VIWANJA 300 KUREJESHWA SERIKALINI KATIKA SHEHIA TATU ZA MAKUNDUCHI KWA KUTOKUENDELEZWA

NA MARYAM NASSOR

ZAIDI ya viwanja 300 vilivyotolewa kwa wananchi wa maeneo ya Tasani, Mzuri na Kiongoni, Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja,  vinatarajiwa kurejeshwa Serikalini kutokana na kutoviendeleza kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi namba 12 ya mwaka 1992.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara maalum ya kutembelea viwanja hivyo, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi Zanzibar , Mussa Kombo Bakar, amesema baadhi ya wananchi walipewa viwanja hivyo kwa ajili ya makaazi  tangu mwaka 2000  hadi sasa havijaendelezwa.

Amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi namba 12 ya mwaka 1992, wananchi wanaopewa ardhi wanatakiwa kuviendeleza ndani ya kipindi cha miaka miwili, na wakishindwa kufanya hivyo viwanja hivyo vinaweza kurejeshwa Serikalini.

Aidha amesema kuwa , jukumu la Kamisheni hiyo ni kutembelea maeneo hayo na kuandaa ripoti kwa Serikali ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa, akieleza kuwa Waziri mwenye dhamana ya Ardhi amepewa mamlaka ya kufuta hati au mikataba ya ukodishaji wa ardhi kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar.

“Sisi kama wataalamu wa ardhi jukumu letu ni kuipatia Serikali taarifa ili iweze kuchukua hatua za kufuta hati hizo na kuwapatia wananchi wengine au taasisi zinazohitaji ardhi hiyo,” amesema Katibu Mtendaji huyo.

Ameeleza kuwa ,zoezi hilo la kutembelea viwanja limeanza rasmi, kwa kuvitembelea viwanja vya shehia ya Tasani, Mzuri na Kiungoni ambavyo vilitolewa kwa  zaidi ya  miaka 25 vikiwa bado havijajengwa makaazi hadi sasa.

Aidha, amefafanua kuwa tafsiri ya kuendeleza kiwanja ni kujenga makaazi ya kuishi, na si kujenga uzio pekee kama baadhi ya wananchi wanavyofanya.

Naye Katibu wa Sheha wa Mzuri, Makunduchi,  Mohamed Issa amesema amelipokea vyema agizo hilo na ameahidi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuendeleza viwanja walivyopewa.

Hata hivyo, amesema changamoto kubwa inayojitokeza ni kwamba baadhi ya wamiliki wa viwanja hivyo hawaishi katika maeneo husika, jambo linalofanya iwe vigumu kuwafikia kwa urahisi.

Top of Form

Bottom of Form

 

No comments

Powered by Blogger.