WAJASIRIAMALI WAILALAMIKIA HOSPITALI YA OCCUPATION HEALTH UNITY KUHUSU VIPIMO VYA TYPHOID
Na Maryam Nassor
WAJASIRIAMALI kisiwani
Unguja wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuifuatilia kwa karibu
Hospitali ya Occupation Health Unity iliyopo Mazizini, kufuatia malalamiko
kuhusu huduma za vipimo vya afya vinavyotolewa, kuwa na wasiwasi , hususan vipimo vya ugonjwa wa Typhoid.
Wakizungumza na
waandishi wa habari huko Magomeni Jitini Unguja, baadhi ya wajasiriamali
walidai kuwa majibu ya vipimo wanavyopewa hospitalini hapo hutofautiana na yale
wanayopata katika hospitali nyengine.
Mjasiriamali Maryam Ali
Mussa, alisema alifika hospitalini hapo kwa ajili ya kupima afya ili aweze
kuwasilisha cheti katika Baraza la Manispaa kwa ajili ya kupata kitambulisho
cha ujasiriamali.
Alisema, baada ya
kujitambulisha kuwa ni mjasiriamali wa kuuza supu, aliambiwa alipe shilingi
53,000 kwa ajili ya vipimo vya magonjwa manne ikiwemo homa ya ini A na B, mkojo
pamoja na Typhoid.
Maryam alisema kuwa, baada ya vipimo hivyo alielekezwa
kurejea nyumbani huku majibu yakitumwa kupitia simu yake ya mkononi.
“Nilitumiwa majibu
kwenye simu na kwenye cheti hicho kuliandikwa ‘Positive’. Sikufahamu maana
yake, lakini baada ya kuona hivyo nilipatwa na mshtuko na kuzimia kwa sababu
nilipima magonywa manne nikihofia yote ninayo , na nilipopata fahamu nilijikuta
nipo Hospitali ya Mafunzo ya Kilimani,” alisema Maryam.
Alisema kuwa ,alipofikishwa Hospitali ya Mafunzo
wazazi wake walisema afanyiwa vipimo
tena na majibu yalionesha kuwa hakuwa na ugonjwa wowote.
Alieleza kuwa , yeye
pamoja na ndugu zake walirejea tena katika Hospitali ya Occupation Health Unity
kuuliza sababu ya tofauti ya majibu hayo.
Aidha alisema kuwa ,mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo
alimueleza kuwa vipimo vyao vilionesha ana Typhoid, hivyo alitakiwa kutumia
dawa kwa muda wa siku 14 na kurejea tena kupima kwa gharama ya shilingi 15,000
ili aweze kupatiwa cheti cha kuwasilisha halmashauri kwa ajili ya kupata
kitambulisho cha ujasiriamali.
Naye mzazi wa
mjasiriamali huyo, Amana Suleiman, alisema ni vyema Serikali ikaingilia kati
suala hilo kwani wana hofu kuwa baadhi ya wagonjwa wanaandikiwa kuwa na maradhi
ili warejee tena hospitalini hapo kwa ajili ya vipimo vingine na kuongeza
gharama hawana hayo maradhi.
Alisema kuwa ,wajasiriamali wengi wanaokwenda kupima
katika hospitali hiyo huambiwa wana Typhoid, lakini wanapopima katika hospitali
nyingine hukutwa hawana maradhi hayo.
“Tunaiomba Serikali yetu sikivu ilifuatilie suala hili ili kupata ufumbuzi, kwani tunahisi baadhi ya watoa huduma katika hospitali hiyo hawafuatii maadili ya taaluma zao,” alisema Amana.
Naye Farid Jabir Mjasiriamali wa Chakula, alisema alienda kupima kituo hicho maarufu kama Kituo cha Covid akaandikiwa kuwa ana ugonywa wa Typhoid lakini hakutumia dawa yoyote, aliporudi mara ya pili kupima akaambiwa amepona na hana ugonywa huo.
" Mimi niliporudi mara ya pili kupima baada ya siku 14 nililipa elfu 15,000 na kufanya vipimo nikaonekana nimepona Typhoid lakini cha kushangaa sikuwahi kutumia dawa nilizoandikiwa nikanunuwe nikaonekana nimepona hapo ndipo nikaanza kutilia wasi wasi kituo hichi" anasema Farid.
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa kutoka Hospitali ya Occupation Health Unity, Zainab Abubakar, alisema ni kweli wakati mwingine hutokea tofauti ya majibu kati ya hospitali hiyo na hospitali nyingine.“Ni kweli huwa tunapokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wateja wetu wanaokuja kufanya vipimo kwa ajili ya shughuli za ujasiriamali. Wakati mwingine hupima hapa na kuonekana wana maradhi, lakini wanapokwenda hospitali nyingine hukutwa hawana,” alisema Zainab.



Post a Comment