TAMWA ZNZ YAZINDUA MRADI WA W- LEAD KUZIBA PENGO LA UONGOZI WA WANAWAKE VIJANA ZANZIBAR.

NA MARYAM NASSOR 

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), kimezindua rasmi  programu ya ( Wanawake Viongozi kwa Ajili ya Usawa, Uwajibikaji na Demokrasia)Women Leaders for Equality, Accountability and Democracy (W-LEAD) unaolenga kuimarisha nafasi za uongozi na ushiriki wa wanawake, hususan wanawake vijana na wanawake wenye ulemavu, katika mifumo ya kidemokrasia na kuweza kushika nafasi mbali mbali za maamuzi.

  Akizindua Program hiyo,  Mkurugenzi  wa TAMWA ZNZ  Nairat Abdullah Ali  amesema  licha ya  wanawake  kuongoza kwa idadi  ya watu  kwa asilimia  51, kwa mujibu wa  Sensa ya watu na  Makaazi ya mwaka 2022, uwakilishi wao katika nafasi za uongozi bado ni mdogo kwa  asilimia 38 ukilinganisha na wanaume.

Amesema kuwa, Hali hii inatokana na changamoto za kihistoria na sababu mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni ambazo kwa miaka mingi zimewaweka wanawake na wasichana nyuma katika kupata fursa sawa za uongozi, ushiriki wa kisiasa na kufanya maamuzi.

 “ TAMWA ZNZ Kupitia Program hii tutatoa mafunzo ya uongozi kwa  wanawake 100 yanayolenga kuchangia kupunguza pengo hili kwa kuwawezesha wanawake, hususan wanawake vijana na wanawake wenye ulemavu, kujenga uwezo wa uongozi, kujiamini na kushiriki kikamilifu katika mifumo ya kidemokrasia na nafasi za maamuzi” amesema  Mkurugenzi Nairat.

Aidha amesema kuwa, Program hii inaendana na ahadi za kimataifa, kikanda na kitaifa ambazo Tanzania na Zanzibar zimeridhia kuhusu kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, ikiwemo Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Haki za Wanawake Barani Afrika (Maputo Protocol) ya mwaka 2003 pamoja na Ajenda ya Afrika tunayoitaka ya 2063 (Agenda 2063), ambazo zinazitaka nchi wanachama kuhakikisha wanawake na wanaume wanashiriki kwa usawa katika uongozi na mifumo ya maamuzi, ikiwa ni pamoja na kufikia uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50 katika vyombo vya maamuzi .

Naye, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka TAMWA ZNZ, Mohamed Khatib Mohamed amesema ,Baada ya mafunzo hayo ,wanawake vijana 60 wataunganishwa na taasisi mbali mbali za umma, sekta binafsi na asasi za kiraia kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo (practical exposure) masuala ya uongozi, usimamizi na utawala bora.

 Amesema , Kupitia uzoefu huo wa moja kwa moja, washiriki watapata fursa ya kushiriki katika michakato ya kufanya maamuzi, kujifunza mbinu za utatuzi wa changamoto za kiuongozi, kuimarisha stadi za mawasiliano na kujenga mitandao ya kitaaluma itakayowawezesha kujiamini na kujiandaa kuchukua nafasi za uongozi katika jamii na taasisi mbalimbali.

 Amesema kuwa, Kampeni za usawa wa kijinsia na mabadiliko ya mienendo ya kijamii, zaidi ya wananchi 100,000 wanatarajiwa kufikiwa na kuhamasishwa kuunga mkono ushiriki sawa wa wanawake na wanaume katika uongozi ili kukuza usawa wa kijinsia na kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.

 Aidha amesema kuwa, Katika kuimarisha mazingira wezeshi ya wanawake, pragramu hii  itaziwezesha asasi tano za kiraia na vyama vitatu vya siasa kuandaa na kutekeleza sera na mifumo inayozingatia usawa wa kijinsia.

 Viile vile, watetezi wa haki za wanawake 60 watajengewa uwezo wa kufuatilia, kuripoti na kushughulikia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake.

 Aidha ameeleza kuwa, TAMWA ZNZ  itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari na  vyombo vya habari kama washirika muhimu katika kuhamasisha usawa wa kijinsia na kuibua masuala ya wanawake na uongozi, ambapo jumla ya waandishi wa  habari 30 watajengewa uwezo wa kuripoti kwa weledi masuala ya wanawake na uongozi.

Kwa upande wake, Mratibu wa  Mradi huo kutoka Jumuiya ya watu wasioona Zanzibar (ZANAB) Rukia Saleh Ali,amesema wamejipanga kutekeleza mradi huo, kwa lengo la kuwawezesha wanawake vijana kujiamini ili kuwa viongozi wazuri baadaye.

Mradi wa W-LEAD unatekelezwa na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na Jumuiya ya wasiona  (ZANAB), State University of Zanzibar (SUZA) na Zanzibar University kwa   unafadhiliwa wa Umoja wa Ulaya kupitia mpango wa Ushiriki wa Wanawake na Vijana katika Demokrasia (Women and Youth Democratic Engagement – WYDE) na utatekelezwa kuanzia 2026 mpaka 2027.

Kauli mbiu ya Program ni: “Building a Zanzibar where women and men participate equally in shaping democratic and inclusive societies.” "Kujenga Zanzibar ambayo wanawake na wanaume wanashiriki kwa usawa katika kuunda na kuendeleza jamii zenye demokrasia na ujumuishi kwa wote."


No comments

Powered by Blogger.