Sheria Zipo, Utekelezaji Wakwamisha Ushiriki wa Wanawake Katika Uongozi Zanzibar

NA MARYAM NASSOR

MRATIBU wa Watetezi wa Mtandao wa Haki za Binadamu Zanzibar, Suleiman Muyuni Baitan, amesema kuwa licha ya kuwepo kwa sheria, kanuni na dira mbalimbali za maendeleo zinazolenga kuimarisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, bado utekelezaji wake haujaridhisha.

Alisema hayo, katika Afisi za Mufti Mombasa wakati akiwasilisha ripoti ya Mapungufu ya kisheria na kiutendaji yanayohusu haki za Wanawake na Ushiriki wao katika uongozi na michakato ya kidemokrasia.

Baitan alisema kuwa, sheria nyingi zilizowekwa kwa ajili ya kumuwezesha mwanamke kushiriki katika uongozi bado hazitekelezwi ipasavyo, Alitolea mfano Sheria ya Halmashauri inayotaka wanawake wawe angalau asilimia 40 katika baadhi ya nafasi za uongozi, lakini kiwango hicho bado hakijafikiwa.

Alisema kuwa , Utafiti waliofanya ulilenga kuchunguza sheria, taratibu na kanuni mbalimbali ili kubaini namna zinavyomsaidia mwanamke kushiriki kikamilifu katika kugombea na kushika nafasi za uongozi.

Aidha, alisema utafiti huo umeibua haja ya kufanya maboresho ya baadhi ya sheria pamoja na kusimamia utekelezaji wa sheria zilizopo, kwani Zanzibar ina sheria nyingi nzuri zinazolenga kuwawezesha wanawake kuwa viongozi.

"Tuna sheria na sera zenye maudhui mazuri, lakini changamoto kubwa ipo katika utekelezaji wak,. Sheria nyingi zilizopo hazilazimishi mamlaka husika kuhakikisha kiwango maalum cha wanawake kinafikiwa katika nafasi za uongozi, wala hazielezi hatua zinazopaswa kuchukuliwa endapo kiwango hicho hakitafikiwa," alisema Baitan.

Aliongeza kuwa, Katiba kupitia Ibara ya 12 na 13 inaelekeza kuhusu usawa wa kijinsia, lakini bado kuna haja ya kujiuliza kama masharti hayo yanatekelezwa kwa vitendo.

Alisema taasisi yao, itaendelea kutoa elimu kwa jamii na kuiomba Serikali kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sheria zilizopo pamoja na mikataba ya kikanda na kimataifa, ikiwemo CEDAW na SADC, ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa SWIL kutoka ZAFELA, Mwanaisha Mustafa Makame, alisema lengo la kikao hicho lilikuwa kuwasilisha ripoti hiyo kwa wadau mbalimbali ili kujadili yaliyobainishwa na kuanza kuyafanyia kazi.

Alisema ripoti hiyo, imeonesha mapungufu mbalimbali katika baadhi ya sheria zilizopo, ikiwemo sheria zinazohusiana na gharama za uchaguzi ambazo zimekuwa kikwazo kwa wanawake wengi wanaotaka kugombea nafasi za uongozi.

Naye Kiongozi wa Wanawake wa Chama cha ACT-Wazalendo, Halima Ibrahim, alisema wanawake bado wanakumbana na vikwazo vingi katika harakati za kutafuta nafasi za uongozi na kuwataka wadau kushirikiana katika kuweka mazingira salama na yenye usawa kwa wote.

Alisema kuwa,  wanawake wengi wana hamasa ya kugombea nafasi za uongozi, lakini hukumbwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa rasilimali za kifedha za kugharamia kampeni na shughuli za uchaguzi.

Kikao hicho cha uwasilishaji wa Ripoti ya Mapungufu ya Kisheria na Kiutendaji kimeandaliwa na Chama cha Wanasheria  Wanawake Zanzibar ( ZAFELA)  na  kiliwakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa Vyama vya Siasa, Maafisa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia, kwa lengo la kujadili changamoto zilizobainishwa na kutafuta suluhisho litakalowezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi na michakato ya kidemokrasia.

MWISHO

Top of Form

 

Bottom of Form

 

No comments

Powered by Blogger.