SERIKALI IWEKE WAZI RATIBA YA KUWASILISHA MSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI ZANZIBAR - ZAMECO
NA MARYAM NASSOR
KAMATI
ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) inaishauri Serikali
kuharakisha taratibu za kuuwasilisha Barazani Mswada wa Huduma za Habari
Zanzibar ili ujadiliwe na kuwa sheria, mswada ambao umekuwa ukipigwa dana ,dana
kwa zaidi ya miaka kumi sasa.
Sheria za Habari zimepitwa na wakati, na zinapatikana
katika vipande vipande vikiwemo katika Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti
na Vitabu Na. 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 7 ya mwaka
1997, Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar Na. 7 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa
marekebisho na Sheria Na. 1 ya mwaka 2010, Sheria Na. 6 ya Baraza la
Wawakilishi ya mwaka 2022 na Sheria ya Kufuta Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya mwaka
1984 na Kutunga Sheria ya Uchaguzi ya 2017 na Mambo Yanayohusiasa na Hayo
Sheria
hizi zimezipa nguvu kubwa taasisi za Serikali ikiwemo kusajili na kufungia
vyombo vya habari kinyume na maelekezo ya demokrasia yanayosisitiza
ushirikishaji na utawala bora wa sheria.
Taarifa
kwamba Mswada huo, upo tayari na unatarajiwa kufikishwa Barazani zilianza kusikika
tokea Balozi Mahmoud Thabit Kombo alipokuwa Waziri wa Habari mwaka 2015. Mei
2023 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari, aliyekuwa Waziri wa
Habari; Bi Tabia Maulid Mwita alitangaza kuwa Mswada huo ulishakamilika kwa asilimia
80 mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe Dkt.
Hussein Mwinyi.
Naye
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt.Riziki Pembe wakati wa kikao
chake cha kwanza na wadau wa sekta ya Habari cha tarehe 28 Januari 2026 aliwaambia
waandishi wa Habari kuwa anatarajia kuuwasilisha Barazani Mswada wa sheria hiyo
ifikapo Septemba mwaka huu.
Hadi
sasa, Bajeti ya Wizara ya Habari ya 2026/27 imeshapitishwa na kugusia tu
kutayarisha sera, sheria na kanuni mbali mbali zinazojumuisha Wizara hiyo, lakini
haikuzungumzia kwa upekee juu ya mswaada wa Sheria ya Habari Zanzibar.
ZAMECO
imefuatilia kwa karibu mjadala uliofanyika katika Kikao cha 11 cha
Mkutano wa Tatu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kilichoanza Mei 6, 2026, ambao
utamalizika rasmi baada ya kukamilisha shughuli zake za bajeti.
Wakati
wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Habari, Wawakilishi kadhaa waliitaka Serikali
kueleza kwa uwazi lini sheria hiyo itawasilishwa rasmi Barazani.
Wajumbe
waliochangia walionesha kutoridhishwa na ucheleweshaji wa muda mrefu wa sheria
hiyo, huku mmoja wao akisema: “Sheria
ya habari imefikia wapi? Waandishi wa habari wamesema mpaka wamechoka, sheria
imekuwa ikitolewa ahadi tu italetwa Barazani lakini ni hadithi tu haifiki,
miaka imekuwa mingi.” Mhe. Jaku Hashim Ayoub, Mwakilishi jimbo la Paje.
"Sheria
ya habari imekuwa ikiahidiwa kwa muda mrefu kuwasilishwa Barazani, lakini hadi
sasa bado haijafikishwa. Tunahitaji kuambiwa wazi ni lini hasa Serikali italeta
sheria hiyo katika Baraza la Wawakilishi ili tuweze kuijadili na kuifanyia
maamuzi. Wananchi na wadau wa sekta ya habari wanastahili kupata majibu ya
uhakika badala ya kuendelea kusikia ahadi zinazojirudia." Prof. Omar
Fakih, Mwakilishi wa Jimbo la Pandani
ZAMECO
inawapongeza, wawakilishi wote ambao kwa dhati kabisa wamepokea kilio cha muda
mrefu cha wadau wa habari na kukifikisha kilio hicho ndani ya Baraza la
Wawakilishi kwa weledi mkubwa.
Ni
wazi kuwa, sheria ya huduma za habari ikipitishwa haitawalinda waandishi wa
habari pekee bali jamii kwa ujumla na kuharakisha maendeleo ya nchi kiuchumi,
kisiasa na kijamii kwa vile itasimamia uongozi bora ikiwemo mapambano dhidi ya
rushwa, haki, usawa, uwazi na uwajibikaji.
“Sheria ya sasa imepitwa na wakati na
inahitaji maboresho ya haraka ili kuendana na maendeleo ya sekta ya habari na
teknolojia”, Mhe. Seif Hamad (Jimbo la Ole) na Mhe. Said Ali Mbarouk (Jimbo la
Gando), ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Habari mwaka 2010, walisisitiza.
Michango hiyo ya Wawakilishi inaonesha, uelewa
mkubwa kuhusu mchango wa sekta ya habari na zinaakisi sauti na matarajio ya
wadau wengi wa habari sababu sheria hiyo italinda haki ya kutoa taarifa, kupata
taarifa na uhuru wa kujieleza ambazo ni haki za msingi za binadamu kama
zilivyoainishwa katika mikataba mingi ya kimataifa, kikanda na kitaifa. Hii ni pamoja na;
Ibara
ya 19 ya Azimio la Kimataifa la Haki za Binaadamu (UDHR), Ibara ya 9 ya Mkataba
wa Afrika wa Haki za Binaadamu na Watu (ACHPR), Mkataba wa Kimataifa wa Haki za
Kiraia na Kisiasa (ICCPR), pamoja na Katiba ya Zanzibar na Tanzania.
Kamati
pia imebaini kuwa, pamoja na umuhimu wa maboresho ya sheria, bado kuna
changamoto zinazowakabili waandishi wa habari katika utekelezaji wa majukumu
yao. Miongoni mwa changamoto hizo ni mazingira yasiyoridhisha ya kufanyia kazi waandishi
wanaoripoti shughuli za Baraza la Wawakilishi, jambo ambalo lilielezwa na
baadhi ya wajumbe kuwa linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
ZAMECO
inaamini kuwa, kuboresha mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari ni sehemu
muhimu ya kuimarisha taaluma ya habari, kuongeza ubora wa taarifa zinazowafikia
wananchi na kuwezesha vyombo vya habari kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi
zaidi.
Kamati
inaona kuwa, Zanzibar yenye maendeleo, uwazi na usawa inahitaji mazingira
salama ya kisheria na kiutendaji yatakayowezesha waandishi wa habari na vyombo
vya habari kutekeleza wajibu wao kwa uhuru, weledi na bila vitisho. Aidha,
uandishi wa habari za uchunguzi unapaswa kupewa nafasi na ulinzi wa kutosha
kutokana na mchango wake katika kufichua ukweli, kulinda rasilimali za umma na
kuimarisha uwajibikaji.
ZAMECO
inaiomba tena, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuharakisha mchakato wa
kukamilisha na kuwasilisha Mswada huo Septemba mwaka huu kama ilivyoahidiwa
ambapo inaamini kuwa Sheria ya Huduma za Habari itajenga mfumo wa kisheria
unaokwenda sambamba na mabadiliko ya kidijitali, unaolinda uhuru wa habari,
unaokuza uwajibikaji na unaochangia maendeleo ya sekta ya habari nchini. Wakati
huo huo, Kamati inawahimiza waandishi wa habari kuendelea kuzingatia maadili ya
taaluma yao, ikiwemo uadilifu, usahihi, uwajibikaji na uzingatiaji wa maslahi
ya umma.
ZAMECO
inajumuisha mashirika yanayojihusisha na masuala ya habari, waandishi wa
habari, wahariri, pamoja na Mtandao ya utetezi wa
haki za binaadamu nchini.
IMETOLEWA NA:
Chama Klabu ya Waandishi
wa Habari Zanzibar (ZPC),
Cha Waandishi
wa Habari Wanawake
Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ),
Waandishi
wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA),
Baraza
la Habari Tanzania, Zanzibar (MCT, ZNZ),
Mtandao
wa Watetezi wa Haki za Binadamu
Tanzania, Zanzibar (THRDC,
ZNZ).
Post a Comment