BEI YA NDOTO : JINSI MSAADA WA MASOMO ULIVYOMWINGIZA MAYASA KWENYE MAAMBUKIZO YA VVU.
Maryam Nassor
"NILIDHANI ninajitafutia njia ya kuendelea na masomo na kujenga maisha yangu ya baadaye, sikujua kuwa nilikuwa najisogeza kwenye hatari kubwa zaidi maishani mwangu."
Hayo ni maneno ya Mayasa Amour (si jina lake halisi), mwenye umri wa miaka 30, mhitimu wa Shahada ya Kwanza ya Mawasiliano ya Umma na mkazi wa Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Akiwa ameketi kwa utulivu huku sauti yake ikionyesha majonzi, Mayasa anasimulia safari yake ya machungu iliyoishia kumwingiza katika maambukizo ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
"Nikiwa mwaka wa pili chuoni, uchumi wa familia yetu ulidorora baada ya baba yangu kufariki dunia. Nilijikuta sina uhakika kama ningeweza kumaliza masomo yangu ya elimu ya juu. Siku moja nilipokuwa nikitembea, nilikutana na mwanaume mwenye umri unaokaribiana na wa baba yangu. Aliniahidi kunisaidia," anasimulia.
Anasema msaada huo ulianza kwa kulipiwa ada za masomo na gharama nyingine za maisha. Kadiri muda ulivyokwenda, ukaribu wao uliongezeka na hatimaye wakaanza kuishi pamoja kama mume na mke bila kufahamu hali za afya zao.
"Baada ya miezi kadhaa, nikiwa mwaka wa mwisho wa masomo, nilipata ujauzito. Nilipoenda hospitalini kwa ajili ya vipimo vya kawaida vya ujauzito, ndipo nilipogundulika kuwa na maambukizo ya Virusi vya Ukimwi," anasema kwa huzuni.
Mayasa anasema alipomweleza mwanaume huyo kuhusu matokeo ya vipimo, alidai kuwa hakufahamu chochote kuhusu maambukizo hayo. Aidha, alimweleza kuwa mke wake wa kwanza alikuwa amefariki miezi mitatu kabla ya wao kukutana, ingawa hakujua alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa gani.
"Baada ya hapo nilirejea kijijini kwetu nikiwa na
majuto makubwa. Nilijiuliza kwa nini nilikubali kuingia katika mahusiano na mtu
aliyenizidi umri kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya kutaka kusaidiwa kumaliza
masomo yangu," anasema.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Ukimwi Zanzibar ya mwaka 2023/2024, kiwango cha maambukizo ya VVU Zanzibar ni asilimia 0.4 ya wakazi wote, kiwango ambacho bado kipo chini ya asilimia moja.
Taarifa hiyo ,inaonesha kuwa Mkoa wa Kusini Unguja unaongoza kwa kiwango cha juu cha maambukizo kwa asilimia 0.8, ukifuatiwa na Mkoa wa Kaskazini Unguja wenye asilimia 0.7.
Mkurugenzi wa Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC), Ahmed Mohamed Khatib, anasema bado kuna haja ya kuongeza juhudi katika mapambano dhidi ya maambukizo ya VVU, hususan miongoni mwa vijana.
Anasema kuwa , vijana wengi wanaendelea kujihusisha na tabia hatarishi zinazochochea maambukizo, jambo linalohitaji kuimarishwa kwa elimu kuhusu kinga dhidi ya VVU pamoja na kuondoa unyanyapaa kwa wanaoishi na maambukizo hayo.
"Jitihada za hali na mali zinahitajika katika kupambana na Ukimwi. Sambamba na hilo, jamii inapaswa kuendelea kuelimishwa kuachana na unyanyapaa, huku vijana wakihimizwa kujiepusha na tabia hatarishi," amesema Khatib.
Ameeleza kuwa, baadhi ya wasichana waliopo vyuo vikuu
huambukizwa VVU kutokana na kuingia katika mahusiano na watu waliowazidi umri,
ambao mara nyingi huwasaidia kulipia ada za masomo na mahitaji mengine ya
maisha.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya Ukimwi Zanzibar, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ukimwi Zanzibar, Dk. Ali Salim Ali, amesema kuwa mwaka 2025 jumla ya watu 105,786 walipimwa VVU.
Kati yao, wanawake walikuwa 58,397 sawa na asilimia 55, huku wanaume wakiwa 47,397 sawa na asilimia 45.
Amesema watu 79,526 sawa na asilimia 75 walipimwa Unguja, wakati 26,230 sawa na asilimia 25 walipimwa Pemba. Kati ya waliopimwa, watu 697 sawa na asilimia 0.7 waligundulika kuwa na maambukizo ya VVU.
Alibainisha kuwa kati ya waliogundulika kuwa na maambukizo, wanawake walikuwa 466 sawa na asilimia 67 na wanaume 231 sawa na asilimia 33. Kundi la umri wa miaka 25 hadi 49 ndilo lililoongoza kwa maambukizo, likichangia asilimia 71 ya visa vyote vilivyogunduliwa.
Aidha, amesema juhudi za kuzuia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto zimeendelea kuzaa matunda. Hadi Septemba mwaka huo 2025, wajawazito 53,706 walihudhuria kliniki, ambapo 53,031 sawa na asilimia 99 walipimwa VVU. Kati yao, wajawazito 98 waligundulika kuwa na maambukizo, sawa na asilimia 0.5.
Kwa upande wa watoto, amesema watoto 362 walifanyiwa kipimo cha DNA-PCR na watoto wawili waligundulika kuwa na maambukizo, sawa na asilimia 0.5.
MCHANGO WA WAADU
Mshauri wa Programu na Afisa Mwakilishi wa UNAIDS Zanzibar, Dk. George Anthony, amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya Ukimwi kutokana na uwepo wa sera thabiti na ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto kwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya maambukizo, ambapo viwango vya maambukizo vinafikia kati ya asilimia 11 na 19.
Ameeleza kuwa safari ya kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030 inahitaji hatua madhubuti, ikiwemo kuimarisha mifumo ya ndani ya kugharamia huduma za VVU na kuongeza uwekezaji wa kitaifa katika sekta ya afya.
SAUTI ZA WANAOISHI NA VVU
Akisoma risala ya watu wanaoishi na VVU, Sara Abdi Mwita amesema kutokana na changamoto za ufadhili, jamii hiyo inaomba Serikali kutenga fedha za dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV) kupitia bajeti ya Serikali ili kuhakikisha huduma hizo zinakuwa endelevu.
Naye Asha Subeti (si jina lake halisi), ambaye anaishi na VVU, amesema wamefarijika kuona juhudi zinazoendelea kufanyika, lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan upungufu wa rasilimali za kifedha.
AHADI YA SERIKALI
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika Desemba 1 mwaka 2025, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Ahmed Abdullah, amesema kwa zaidi ya miongo mitatu Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kudhibiti maambukizo ya VVU, huku kiwango cha maambukizo kikibaki chini ya asilimia moja.
Amesema kuwa , tafiti zinaonesha kuwa mwaka 2025 asilimia 0.4 ya wakazi wa Zanzibar, sawa na watu 10,256, wanaishi na VVU.
Aidha, amesema maambukizo mapya yamepungua kutoka watu 362 mwaka 2020 hadi watu 211 mwaka 2025, huku idadi ya vifo vinavyohusishwa na Ukimwi ikishuka kutoka 230 hadi 115 katika kipindi hicho.
Amehakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itaendelea
kuimarisha sera, kuongeza bajeti ya dawa na vifaa vya kupimia VVU, pamoja na
kuendeleza mapambano dhidi ya unyanyapaa ili kufikia lengo la kutokomeza Ukimwi
ifikapo mwaka 2030.
MWISHO

Post a Comment