MABADILIKO YA TABIANCHI YANAVYOATHIRI BEI YA SAMAKI ZANZIBAR: JAMII INA WAJIBU WA KULINDA RASILIMALI ZA BAHARI

Kupanda kwa joto la bahari na kuharibika kwa mazingira ya mazalia ya samaki kunaweza kuathiri uzalishaji, kipato cha wavuvi na upatikanaji wa kitoweo kwa wananchi.

Na Maryam Nassor

Kwa muda mrefu, samaki wamekuwa sehemu muhimu ya chakula na maisha ya wananchi wengi wa Zanzibar, hususan wanaoishi katika maeneo ya mwambao ambao hutegemea rasilimali za bahari kwa chakula, kipato na shughuli za kiuchumi.

Katika kipindi cha hivi karibuni, kupanda kwa bei ya samaki kumeanza kuwa changamoto kwa familia nyingi, hasa zile zenye kipato cha chini ambazo zinategemea samaki kama chanzo muhimu cha protini katika milo yao ya kila siku.

Baadhi ya wananchi wanalazimika kubadili aina ya kitoweo kutokana na kushindwa kumudu bei ya samaki wakubwa, huku dagaa wakigeuka kuwa miongoni mwa machaguo yanayoweza kununuliwa kwa gharama nafuu zaidi.

Hali hiyo inaibua umuhimu wa jamii kuelewa uhusiano uliopo kati ya mabadiliko ya tabianchi, afya ya mazingira ya bahari, shughuli za uvuvi na upatikanaji wa chakula.

Mabadiliko ya tabianchi si suala linalohusu hali ya hewa pekee, bali yanaweza kuathiri maisha ya kila siku ya wananchi kupitia mabadiliko katika mifumo ya uzalishaji wa chakula, uchumi na upatikanaji wa rasilimali za asili.

Kwa upande wa bahari, ongezeko la joto la maji, mabadiliko ya mikondo ya bahari na kuharibika kwa mazingira ya matumbawe ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuathiri makazi, mazalia na usambazaji wa samaki.

Utafiti uliochapishwa katika jarida la kisayansi kuhusu mazingira na uvuvi Zanzibar unaonesha kuwa mabadiliko hayo ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuathiri upatikanaji na uzalishaji wa samaki.

Aidha, taarifa iliyochapishwa na gazeti la The Citizen Machi 13, 2025, inaeleza kuwa Uchumi wa Buluu Zanzibar unakabiliwa na hatari zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo kupanda kwa kina cha bahari, mmomonyoko wa fukwe na matukio ya hali mbaya ya hewa.

Hivyo, kulinda mazingira ya bahari ni hatua muhimu katika kuhakikisha rasilimali za baharini zinaendelea kutoa manufaa kwa jamii ya sasa na vizazi vijavyo.

MABADILIKO YA BAHARI YANAATHIRI MAISHA YA WANANCHI

Athari za mabadiliko ya mazingira ya bahari zinaonekana pia katika maisha ya wananchi wanaotegemea samaki kama chakula na chanzo cha kipato.

Fadhili Abdallah, mkazi wa Mkokotoni, Unguja, anasema kupanda kwa bei ya samaki kumeifanya familia yake kupata changamoto katika kumudu kitoweo hicho licha ya Serikali kuendelea kuimarisha Uchumi wa Buluu.

"Kiukweli, licha ya Serikali kuimarisha Uchumi wa Buluu, kitoweo kimekuwa bei kubwa kwa mwananchi wa kawaida. Hatuwezi tena kumudu kula samaki, tunaambulia kula dagaa tonge," anasema.

Anaeleza kuwa hali hiyo inawaathiri wanawake ambao katika familia nyingi wana jukumu kubwa la kupanga matumizi ya fedha za nyumbani na kuhakikisha familia zinapata chakula.

Kwa upande wake, Mtumwa Omar kutoka Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, anasema upatikanaji wa samaki na uwezo wa wananchi kuununua umebadilika ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Anasema kupanda kwa gharama za mahitaji mengine ya nyumbani kunafanya familia nyingi kushindwa kutenga fedha za kutosha kununua samaki.

"Awali, watu wa Kaskazini walikuwa wanakula samaki kwa wingi, lakini kwa sasa hali ni tofauti. Ukishanunua mahitaji mengine ya chakula kama mchele na nazi, inakuwa vigumu tena kutoa shilingi 5,000 mpaka  20,000  kununua samaki ambao wakati mwingine hawatoshi kwa familia nzima. Mwishowe unaishia kula mboga au dagaa," anasema.

Uzoefu huo unaonesha kuwa mabadiliko ya gharama za chakula yanaweza kuathiri uchaguzi wa lishe katika kaya, hasa zile zinazotegemea kipato cha kila siku.

WAVUVI NAO WANAKABILIWA NA CHANGAMOTO ZA MAZINGIRA YA BAHARI

Wakati wananchi wakikabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei ya samaki, wavuvi nao wanakabiliwa na mabadiliko yanayoathiri shughuli zao za kila siku.

Makame Vuai Juma, mvuvi kutoka Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja, anasema baadhi ya wavuvi wanalazimika kwenda maeneo yenye kina kirefu cha bahari kutafuta samaki kutokana na mabadiliko ya mazingira ya bahari.

Anasema ongezeko la joto la maji linaweza kuathiri upatikanaji wa baadhi ya samaki katika maeneo ya karibu na mwambao.

"Mabadiliko ya tabianchi yamepelekea kwenda kuvua kina kirefu cha bahari kutokana na joto kuongezeka baharini, hali inayosababisha samaki kutopatikana kwa urahisi katika maji ya karibu na mwambao," anasema.

Hata hivyo, anabainisha kuwa ongezeko la mahitaji ya samaki kutokana na kukua kwa shughuli za utalii katika maeneo ya Kaskazini Unguja nalo linachangia kupanda kwa bei ya kitoweo hicho.

Maelezo hayo yanaonesha kuwa bei ya samaki haiathiriwi na sababu moja pekee. Mabadiliko ya mazingira ya bahari, gharama za uvuvi, mahitaji ya soko na mfumo wa usambazaji vinaweza kuchangia hali ya upatikanaji na bei ya samaki.

Anasema kuwa,  muhimu jamii kuelewa kuwa kukabiliana na changamoto hiyo kunahitaji hatua zinazozingatia mazingira na uchumi wa wananchi.

TAKWIMU ZA UVUVI NA UMUHIMU WA KUZIELEWA

Pamoja na malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya samaki, takwimu za Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar zinaonesha kuwa uzalishaji wa samaki katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ uliongezeka kutoka tani 5,437 mwaka 2022 hadi tani 8,525 mwaka 2023.

Aidha, thamani ya samaki waliovuliwa katika wilaya hiyo iliongezeka kutoka shilingi bilioni 34.875 mwaka 2022 hadi shilingi bilioni 59.408 mwaka 2023.

Takwimu hizo zinaonesha ongezeko la uzalishaji na thamani ya samaki, lakini ni muhimu jamii kuelewa kuwa kuongezeka kwa uzalishaji hakumaanishi moja kwa moja kuwa kila mwananchi atanufaika kwa kupata samaki kwa bei nafuu.

Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Haji Abdallah, anasema pamoja na ongezeko la uzalishaji, bei ya samaki bado iko juu kutokana na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hiyo.

Anasema mabadiliko ya mazingira ya bahari ni miongoni mwa mambo yanayochangia wavuvi kulazimika kwenda maeneo yenye kina kirefu kutafuta samaki.

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa boti za kisasa kwa wavuvi ili kuimarisha shughuli zao, lakini wananchi wa kawaida bado wanakabiliwa na changamoto ya kumudu bei ya samaki.

"Kutokana na kupanda kwa bei ya samaki, wakati mwingine ni bora kununua kilo ya nyama ya ng’ombe kwa sababu ni rahisi kuliko samaki. Mahitaji ya samaki yamekuwa makubwa kutokana na uwepo wa hoteli kubwa za watalii, hivyo wananchi wa kawaida wanashindwa kuhimili bei hiyo," anasema.

Aidha, anasema uwepo wa hoteli nyingi katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ umeongeza mahitaji ya samaki, huku baadhi ya boti za uvuvi zikiuza samaki moja kwa moja kwa hoteli hizo.

Hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuimarisha mfumo wa usambazaji wa samaki ili kuhakikisha wananchi wa kawaida wanapata fursa ya kunufaika na rasilimali za bahari.

UCHUMI WA BULUU UNAHITAJI KWENDA SAMBAMBA NA UHIFADHI WA BAHARI

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuwekeza katika kuimarisha Uchumi wa Buluu kupitia sekta ya uvuvi, utoaji wa vifaa vya kisasa, ujenzi wa masoko ya samaki na kuongeza uwezo wa wavuvi kufanya shughuli zao kwa tija.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika kueleza mafanikio ya Serikali, alitaja utoaji wa zaidi ya boti 1,000 kwa ajili ya kusaidia shughuli za uvuvi na kilimo cha mwani, hatua iliyonufaisha takribani watu 32,000.

Jitihada hizo zinalenga kuongeza uzalishaji, kupanua fursa za ajira na kuimarisha kipato cha wananchi wanaotegemea rasilimali za bahari.

Aidha, katika maelezo yake kuhusu kuimarisha Uchumi wa Buluu Oktoba 2025, Rais Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kujenga masoko ya kisasa ya samaki na kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya baharini ili kuongeza manufaa kwa wananchi.

Hata hivyo, uwekezaji katika sekta ya uvuvi unahitaji kuambatana na mikakati ya kuhifadhi mazingira ya bahari ili rasilimali hizo ziendelee kupatikana kwa muda mrefu.

Bahari yenye afya ni muhimu kwa maisha ya viumbe vya majini, ustawi wa wavuvi na usalama wa chakula kwa jamii.

JAMII INAWEZA KUFANYA NINI KULINDA RASILIMALI ZA BAHARI?

Kulinda bahari si jukumu la Serikali na wataalamu wa mazingira pekee. Kila mwananchi ana nafasi ya kuchangia katika kuhakikisha mazingira ya bahari yanakuwa salama.

Afisa  Uvuvimii wilaya ya Kaskazini Unguja Haji Abdallah anasema   jamii inapaswa kushiriki katika kulinda na kurejesha mikoko.  Kwani ina umuhimu mkubwa katika mazingira ya pwani na hutoa maeneo muhimu ya kujificha na kukua kwa baadhi ya viumbe vya baharini.

Anasema  wananchi wanapaswa kushirikiana katika kuhifadhi matumbawe na kuepuka shughuli zinazoweza kuyaharibu. Matumbawe ni sehemu muhimu ya mazingira ya bahari na hutoa makazi kwa aina mbalimbali za viumbe vya majini.

Aidha anasema kuwa, wavuvi wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu za uvuvi endelevu, ikiwemo kuepuka njia haramu zinazoweza kuharibu mazalia ya samaki na kupunguza rasilimali za bahari.

“ Ni  muhimu kuimarisha tafiti na mifumo ya ukusanyaji wa takwimu za uvuvi katika kila wilaya ili kufuatilia mabadiliko ya uzalishaji, aina za samaki wanaopatikana, mwenendo wa bei na changamoto zinazowakabili wavuvi” ameshauri .

 

No comments

Powered by Blogger.