W-LEAD: MAFUNZO YAWAJENGEA WANAWAKE VIJANA UJASIRI WA KUINGIA KATIKA UONGOZI ZANZIBAR

Awamu ya pili  inaendelea  kuwajengea uwezo wanafunzi wa vyuo vikuu na viongozi vijana wa vyama vya siasa kushiriki katika nafasi za uongozi na kufanya maamuzi.

Na Maryam Nassor

Hapo awali, kusimama mbele ya wanafunzi wenzake na kuomba kura ili agombee nafasi ya uongozi chuoni ilikuwa hatua ngumu kwa Kauthari Ngwali, mwanafunzi wa Zanzibar University (ZU). Licha ya kuwa na ndoto ya kuwa kiongozi, hakuwa na ujasiri wa kutosha kujitokeza na kuwania nafasi hiyo.

Anasema aliacha nafasi nyingi za uongozi zimpite bila ya kugombea kwa sababu ya kukosa ujasiri wa kusimama na kugombea nafasi za uongozi na  kuacha ndoto yake ya kuwa kiongozi ikiwa inadidimia.

Lakini mtazamo wake umeanza kubadilika baada ya kushiriki mafunzo ya W-LEAD yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ), kwa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu, zikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Zanzibar University (ZU).

Kupitia mafunzo hayo, Kauthari  anasema amepata maarifa na ujasiri mpya unaompa matumaini ya kushiriki katika uongozi, si tu akiwa chuoni, bali hata katika nafasi nyingine za uongozi ndani ya jamii.

Anasema kabla ya mafunzo hayo alikuwa na shauku ya kuwa kiongozi, lakini hofu ya kujitokeza mbele ya watu na kueleza dhamira yake ilikuwa kikwazo kikubwa.

“Nawashukuru sana TAMWA-ZNZ kwa kunifungulia njia ya uongozi na kunipa ujasiri. Hapo awali nilipenda kuingia katika uongozi, lakini nilikosa ujasiri wa kujitokeza na kuomba kura kwa wanafunzi wenzangu,” anasema Kauthari.

Anasema kuwa ,  mafunzo hayo yamemsaidia kutambua kuwa uongozi si nafasi inayopaswa kuachwa kwa watu wenye uzoefu mkubwa pekee, bali hata vijana wa kike wanaweza kujiandaa na kushiriki katika michakato ya kufanya maamuzi tangu wanapokuwa vyuoni.

Kwa sasa, anasema yuko tayari kujitokeza kuwania nafasi za uongozi anapopata fursa, akiwa na uelewa mpana zaidi kuhusu majukumu na sifa zinazohitajika kwa kiongozi.

Mabadiliko hayo yanaonesha namna uwekezaji katika maarifa na ujenzi wa uwezo unavyoweza kumsaidia mwanamke kijana kuvuka hofu na kuanza kuona uongozi kama fursa inayoweza kufikiwa.

Kutoka kuwa mwanachama hadi kutambua uwezo wa kuongoza

Si Kauthari  pekee aliyepata mtazamo mpya kuhusu uongozi kupitia mafunzo hayo.

Nafda Ali Hassan, mwanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Wilaya ya Mjini, ni miongoni mwa wanawake walionufaika na programu ya W-LEAD.

Kabla ya kushiriki mafunzo hayo, Nafda alikuwa na dhamira ya kushiriki katika shughuli za kijamii na uongozi, lakini alihitaji kuongeza maarifa kuhusu misingi ya uongozi, majukumu ya viongozi na namna ya kushiriki katika michakato ya kufanya maamuzi.

Anasema mafunzo hayo yamemsaidia kutafakari uwezo wake, kutambua nafasi aliyonayo kama mwanamke na kuelewa umuhimu wa kujitokeza katika nafasi zinazoweza kumwezesha kushawishi mabadiliko ndani ya jamii.

Kwa Nafda, mafunzo hayo hayakuwa darasa la kawaida, bali yalikuwa fursa ya kujitambua na kupata mwanga mpya kuhusu nafasi ya mwanamke katika uongozi.

Uzoefu wa Nafda na Kauthari  unaonesha kuwa wakati mwingine changamoto inayowazuia wanawake kushiriki katika uongozi si ukosefu wa uwezo, bali ni kukosa maarifa, kujiamini na mazingira yanayowawezesha kutambua na kutumia uwezo wao.

Kwa nini TAMWA-ZNZ imewekeza katika wanawake wa vyuoni?

Meneja wa Mawasiliano wa TAMWA-ZNZ, Sophia Ngalapi, anasema uamuzi wa taasisi hiyo kushirikiana na SUZA na ZU kuwaandaa wanafunzi wa kike kushiriki katika uongozi umetokana na umuhimu wa kujenga kizazi cha wanawake viongozi tangu wakiwa katika hatua za awali za elimu ya juu.

Anasema vyuo vikuu ni maeneo muhimu ya kuandaa viongozi wa baadaye kwa kuwa vinawakutanisha vijana wenye mitazamo, uwezo na ndoto mbalimbali.

Kwa mujibu wake, kuwapatia wanafunzi wa kike maarifa ya uongozi wakiwa vyuoni kunawasaidia kujenga msingi wa kujiamini, uwajibikaji na ushiriki katika michakato ya kufanya maamuzi.

Aidha, anasema ushirikiano huo unalenga kupanua fursa za wanawake kupata elimu ya uongozi na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika nafasi mbalimbali za maamuzi.

“Lengo si kuwaandaa wanawake kugombea nafasi za kisiasa pekee, bali pia kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi katika taasisi, mashirika, asasi za kiraia, vyama vya siasa na maeneo mengine ya kijamii na kiuchumi,” anasema Sophia.

Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Nairat Abdullah Ali, amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wanawake kushiriki katika uongozi na michakato ya kufanya maamuzi, akitambua kuwa ushiriki wao ni sehemu muhimu ya kujenga jamii yenye usawa na maendeleo jumuishi.

“ Uwekezaji katika wanawake vijana ni mkakati wa muda mrefu unaolenga kuandaa viongozi watakaoweza kushiriki katika kutatua changamoto za jamii na kuchangia maendeleo” anasema Mkurugenzi.

Takwimu zaonesha umuhimu wa kuongeza wanawake katika uongozi

Umuhimu wa programu kama W-LEAD unaonekana zaidi tunapochunguza idadi ya wanawake katika jamii na nafasi walizonazo katika vyombo mbalimbali vya uongozi Zanzibar.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), Zanzibar ilikuwa na wakazi 1,889,773.

Kati yao, wanawake walikuwa 974,281, sawa na asilimia 51.6 ya wakazi wote, huku wanaume wakiwa 915,492, sawa na asilimia 48.4.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa wanawake ni zaidi ya nusu ya wakazi wa Zanzibar, hali inayosisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanapata fursa za kushiriki katika uongozi na kufanya maamuzi yanayohusu maendeleo ya jamii.

Hata hivyo, idadi hiyo haijaakisi kikamilifu uwakilishi wao katika baadhi ya nafasi za uongozi.

Kwa mujibu wa takwimu za nafasi za uongozi Zanzibar za Machi 2024 zilizowasilishwa katika taarifa ya Taifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Wanawake, Amani na Usalama, wanawake walikuwa sita kati ya mawaziri 18, sawa na asilimia 33.

Katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wanawake walikuwa 29 kati ya wajumbe 79, sawa na asilimia 37.

Aidha, wanawake walikuwa madiwani 98 kati ya madiwani 211, sawa na asilimia 46, huku nafasi za masheha zikiwa na wanawake 79 kati ya masheha 388, sawa na takribani asilimia 20.

Takwimu hizi zinaonesha kuwa pamoja na hatua zilizopigwa katika baadhi ya maeneo, bado kuna umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, hasa katika ngazi za jamii na taasisi mbalimbali.

Hivyo, programu ya W-LEAD inakuja kama moja ya hatua zinazolenga kupunguza pengo hilo kwa kuwaandaa wanawake vijana kupitia elimu, mafunzo na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika uongozi.

W-LEAD: Kutoka maarifa hadi vitendo

Ili kuhakikisha mafunzo hayabaki kuwa maarifa ya darasani pekee, programu ya W-LEAD imeweka mkazo pia katika kuwapa washiriki fursa za kujifunza kwa vitendo.

Afisa wa Ufuatiliaji na Tathmini wa TAMWA-ZNZ, Muhamed Hatibu, anasema programu hiyo imejikita katika kujenga uelewa, kujiamini na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi.

Anasema katika mpango wa mafunzo ya siku nne katika awamu ya pili ya program  hiyo , jumla ya vijana 50 walilengwa kunufaika, wakiwemo 30 kutoka Unguja na 20 kutoka Pemba.

Aidha, anasema washiriki 20 watakaoonesha uwezo mzuri wanatarajiwa kupata nafasi za kujifunza kwa vitendo katika taasisi mbalimbali.

Kwa mujibu wake, hatua hiyo inalenga kuhakikisha washiriki wanapata nafasi ya kutumia maarifa waliyoyapata darasani katika mazingira halisi ya kazi na uongozi.

Anasema TAMWA-ZNZ pia itafanya ufuatiliaji wa maendeleo ya washiriki baada ya mafunzo ili kubaini idadi ya wanawake watakaoanza kushika nafasi za uongozi, kushiriki katika michakato ya kufanya maamuzi au kuanzisha mipango inayowawezesha wanawake wengine.

“ Ufuatiliaji huo ni muhimu katika kupima matokeo ya programu, kwa kuwa mafanikio yake hayapaswi kupimwa kwa idadi ya wanawake waliohudhuria mafunzo pekee, bali pia mabadiliko yatakayojitokeza katika ushiriki wao wa uongozi baada ya mafunzo” amesema Mohamed .

Uwekezaji wa leo, viongozi wa kesho

Safari za Nafda na  Kauthari  zinaonesha namna mafunzo ya uongozi yanavyoweza kuwa mwanzo wa mabadiliko katika maisha ya wanawake vijana.

Kwa Kauthari , aliyekuwa akishindwa kujitokeza kuomba kura chuoni, sasa anaona uwezekano wa kuwania nafasi za uongozi. Kwa Nafda, mafunzo hayo yamemsaidia kutambua zaidi uwezo wake na umuhimu wa kushiriki katika kuleta mabadiliko ndani ya jamii.

Hizi ni hatua zinazoweza kuonekana kuwa ndogo, lakini zina umuhimu mkubwa katika kujenga kizazi cha wanawake watakaokuwa tayari kushiriki katika maamuzi yanayogusa maisha yao na jamii kwa ujumla.

Hata hivyo, ili matokeo ya W-LEAD yawe endelevu, ni muhimu ushirikiano kati ya TAMWA-ZNZ, SUZA, ZU na wadau wengine uendelee kuimarishwa.

 

No comments

Powered by Blogger.