MABADILIKO YA TABIANCHI YAPANDISHA BEI YA SAMAKI
Kupanda kwa joto la bahari na kuharibika kwa mazingira ya mazalia ya samaki kunaweza kuathiri uzalishaji, kipato cha wavuvi na upatikanaji wa kitoweo kwa wananchi.
Na Maryam Nassor
Kwa muda mrefu, samaki wamekuwa sehemu muhimu ya chakula na maisha ya wananchi wengi wa Zanzibar, hususan wanaoishi katika maeneo ya mwambao ambao hutegemea rasilimali za bahari kwa chakula, kipato na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Katika kipindi cha hivi karibuni, kupanda kwa bei ya samaki kumeanza kuwa changamoto kwa familia nyingi, hasa zile zenye kipato cha chini ambazo zinategemea samaki kama chanzo muhimu cha protini katika milo yao ya kila siku.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi wanalazimika kubadili aina ya kitoweo kwa kuchagua vyakula wanavyoweza kumudu, huku dagaa wakigeuka kuwa miongoni mwa machaguo yanayopatikana kwa gharama nafuu zaidi.
Hali hiyo inaibua maswali kuhusu mustakabali wa rasilimali za bahari na uhusiano wake na maisha ya wananchi, hususan wakati dunia ikiendelea kukabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Mabadiliko ya tabianchi si suala linalohusu ongezeko la joto na mabadiliko ya misimu pekee, bali yana athari katika mifumo ya uzalishaji wa chakula, uchumi na upatikanaji wa rasilimali za asili.
Kwa upande wa bahari, ongezeko la joto la maji, mabadiliko ya mikondo ya bahari na kuharibika kwa mazingira ya matumbawe ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuathiri makazi, mazalia na usambazaji wa samaki.
Utafiti uliochapishwa katika jarida la kisayansi kuhusu mazingira na uvuvi Zanzibar unaonesha kuwa mabadiliko hayo ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuathiri upatikanaji na uzalishaji wa samaki.
Aidha, taarifa iliyochapishwa na gazeti la The Citizen Machi 13, 2025, inaeleza kuwa Uchumi wa Buluu Zanzibar unakabiliwa na hatari zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo kupanda kwa kina cha bahari, mmomonyoko wa fukwe na matukio ya hali mbaya ya hewa.
Hali hiyo inaonesha kuwa kulinda bahari si suala la kuhifadhi mazingira pekee, bali ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na rasilimali hizo kwa chakula, kipato na maendeleo ya kiuchumi.
MABADILIKO YA BAHARI YANAATHIRI MAISHA YA WANANCHI
Athari za mabadiliko ya mazingira ya bahari zina umuhimu wa kuangaliwa kwa karibu kutokana na utegemezi wa wananchi wengi wa Zanzibar kwa rasilimali hizo.
Kwa baadhi ya familia, samaki si kitoweo cha kawaida tu, bali ni sehemu ya lishe na utamaduni wao wa chakula. Hivyo, kupanda kwa bei yake kunaweza kuathiri uwezo wa kaya kupata chakula chenye virutubisho muhimu.
Fadhili Abdallah, mkazi wa Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, anasema kupanda kwa bei ya samaki kumeifanya familia yake kupata changamoto katika kumudu kitoweo hicho licha ya Serikali kuendelea kuimarisha Uchumi wa Buluu.
"Kiukweli, licha ya Serikali kuimarisha Uchumi wa Buluu, kitoweo kimekuwa bei kubwa kwa mwananchi wa kawaida. Hatuwezi tena kumudu kula samaki, tunaambulia kula dagaa tonge," anasema.
Anaeleza kuwa hali hiyo inawaathiri zaidi wanawake ambao katika familia nyingi wana jukumu kubwa la kupanga matumizi ya fedha za nyumbani na kuhakikisha familia zinapata chakula.
Kwa upande wake, Mtumwa Omar kutoka Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, anasema upatikanaji wa samaki na uwezo wa wananchi kuununua umebadilika ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Anasema kupanda kwa gharama za mahitaji mengine ya nyumbani kunafanya baadhi ya familia kushindwa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kununua samaki.
"Awali, watu wa Kaskazini walikuwa wanakula samaki kwa wingi, lakini kwa sasa hali ni tofauti. Ukishanunua mahitaji mengine ya chakula kama mchele na nazi, inakuwa vigumu tena kutoa shilingi 5,000 mpaka 20,000 kununua samaki ambao wakati mwingine hawatoshi kwa familia nzima. Mwishowe unaishia kula mboga au dagaa," anasema.
Uzoefu wa wananchi hao unaonesha namna mabadiliko ya gharama za chakula yanavyoweza kuathiri uchaguzi wa lishe katika kaya, hasa zile zinazotegemea kipato cha kila siku.
Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kuwa kupanda kwa bei ya samaki hakusababishwi na mabadiliko ya tabianchi pekee. Mahitaji ya soko, gharama za uvuvi, usafirishaji na mfumo wa usambazaji pia vina nafasi katika mwenendo wa bei.
WAVUVI NAO WANAKABILIWA NA CHANGAMOTO ZA MAZINGIRA YA BAHARI
Wakati wananchi wakikabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei ya samaki, wavuvi nao wanakabiliwa na mabadiliko ya mazingira yanayoweza kuathiri shughuli zao za kila siku.
Makame Vuai Juma, mvuvi kutoka Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja, anasema baadhi ya wavuvi wanalazimika kwenda maeneo yenye kina kirefu cha bahari kutafuta samaki kutokana na mabadiliko ya mazingira ya bahari.
Anasema, ongezeko la joto la maji linaweza kuathiri upatikanaji wa baadhi ya samaki katika maeneo ya karibu na mwambao.
"Mabadiliko ya tabianchi yamepelekea kwenda kuvua kina kirefu cha bahari kutokana na joto kuongezeka baharini, hali inayosababisha samaki kutopatikana kwa urahisi katika maji ya karibu na mwambao," anasema.
Hata hivyo, anabainisha kuwa ongezeko la mahitaji ya samaki kutokana na kukua kwa shughuli za utalii katika maeneo ya Kaskazini Unguja nalo linachangia kupanda kwa bei ya kitoweo hicho.
Maelezo hayo yanaonesha kuwa changamoto ya upatikanaji na bei ya samaki ina sura mbalimbali zinazohitaji kuangaliwa kwa pamoja.
Mabadiliko ya mazingira ya bahari yanaweza kuathiri maeneo ya uvuvi, huku gharama za shughuli hizo na ongezeko la mahitaji ya soko vikiongeza changamoto kwa wavuvi na wananchi wanaotegemea samaki.
Anasema , kuna umuhimu wa kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu uhusiano kati ya afya ya bahari, shughuli za uvuvi na usalama wa chakula.
TAKWIMU ZA UVUVI NA UMUHIMU WA KUZIELEWA
Pamoja na malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya samaki, takwimu za Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar zinaonesha kuwa uzalishaji wa samaki katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ uliongezeka kutoka tani 5,437 mwaka 2022 hadi tani 8,525 mwaka 2023.
Aidha, thamani ya samaki waliovuliwa katika wilaya hiyo iliongezeka kutoka shilingi bilioni 34.875 mwaka 2022 hadi shilingi bilioni 59.408 mwaka 2023.
Takwimu hizo zinaonesha ongezeko la uzalishaji na thamani ya samaki, lakini ongezeko hilo halimaanishi moja kwa moja kuwa kila mwananchi atanufaika kwa kupata samaki kwa bei nafuu.
Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Haji Abdallah, anasema pamoja na ongezeko la uzalishaji, bei ya samaki bado iko juu kutokana na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hiyo.
Anasema mabadiliko ya mazingira ya bahari ni miongoni mwa mambo yanayochangia wavuvi kulazimika kwenda maeneo yenye kina kirefu kutafuta samaki.
Anaeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa boti za kisasa kwa wavuvi ili kuimarisha shughuli zao, lakini wananchi wa kawaida bado wanakabiliwa na changamoto ya kumudu bei ya samaki.
"Kutokana na kupanda kwa bei ya samaki, wakati mwingine ni bora kununua kilo ya nyama ya ng’ombe kwa sababu ni rahisi kuliko samaki. Mahitaji ya samaki yamekuwa makubwa kutokana na uwepo wa hoteli kubwa za watalii, hivyo wananchi wa kawaida wanashindwa kuhimili bei hiyo," anasema.
Aidha, anasema uwepo wa hoteli nyingi katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ umeongeza mahitaji ya samaki, huku baadhi ya boti za uvuvi zikiuza samaki moja kwa moja kwa hoteli hizo.
Hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usambazaji na biashara ya samaki ili kuhakikisha wananchi wa kawaida wanapata fursa ya kunufaika na rasilimali za bahari.
Kwa msingi huo, ni muhimu takwimu za uzalishaji wa samaki ziende sambamba na taarifa kuhusu upatikanaji wa samaki katika masoko, mwenendo wa bei na uwezo wa wananchi kuzinunua.
UCHUMI WA BULUU UNAHITAJI KWENDA SAMBAMBA NA UHIFADHI WA BAHARI
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuwekeza katika kuimarisha Uchumi wa Buluu kupitia sekta ya uvuvi, utoaji wa vifaa vya kisasa, ujenzi wa masoko ya samaki na kuongeza uwezo wa wavuvi kufanya shughuli zao kwa tija.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika kueleza mafanikio ya Serikali, alitaja utoaji wa zaidi ya boti 1,000 kwa ajili ya kusaidia shughuli za uvuvi na kilimo cha mwani, hatua iliyonufaisha takribani watu 32,000.
Jitihada hizo zinalenga kuongeza uzalishaji, kupanua fursa za ajira na kuimarisha kipato cha wananchi wanaotegemea rasilimali za bahari.
Aidha, katika maelezo yake kuhusu kuimarisha Uchumi wa Buluu Oktoba 2025, Rais Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kujenga masoko ya kisasa ya samaki na kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya baharini ili kuongeza manufaa kwa wananchi.
Hata hivyo, pamoja na uwekezaji huo, kuna umuhimu wa kuhakikisha maendeleo ya sekta ya uvuvi yanaambatana na mikakati madhubuti ya kuhifadhi mazingira ya bahari.
JAMII INA WAJIBU WA KULINDA RASILIMALI ZA BAHARI
Kulinda bahari si jukumu la Serikali na wataalamu wa mazingira pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi, wavuvi, wafanyabiashara wa samaki na jamii kwa ujumla.
Kila mmoja ana nafasi ya kuchangia katika kuhakikisha mazingira ya bahari yanahifadhiwa ili kuendeleza upatikanaji wa samaki kwa sasa na vizazi vijavyo.
Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Haji Abdallah, anasema jamii inapaswa kushiriki katika kulinda na kurejesha mikoko kutokana na umuhimu wake katika mazingira ya pwani.
Anaeleza kuwa mikoko hutoa maeneo muhimu ya kujificha na kukua kwa baadhi ya viumbe vya baharini, hivyo uharibifu wake unaweza kuathiri mifumo ya maisha ya viumbe hao.
Aidha, anasema wananchi wanapaswa kushirikiana katika kuhifadhi matumbawe na kuepuka shughuli zinazoweza kuyaharibu, kwa kuwa ni sehemu muhimu ya makazi ya aina mbalimbali za viumbe wa baharini.
Anasisitiza pia umuhimu wa wavuvi kuzingatia sheria na taratibu za uvuvi endelevu, ikiwemo kuepuka njia haramu zinazoweza kuharibu mazalia ya samaki na kupunguza rasilimali za bahari.
“Ni muhimu kuimarisha tafiti na mifumo ya ukusanyaji wa takwimu za uvuvi katika kila wilaya ili kufuatilia mabadiliko ya uzalishaji, aina za samaki wanaopatikana, mwenendo wa bei na changamoto zinazowakabili wavuvi.” Anashauri .
Anasema jamii inapaswa kuimarisha ushiriki wake katika shughuli za usafi wa fukwe, upandaji na utunzaji wa mikoko, pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu vitendo vinavyoharibu mazingira ya bahari.
Anasema kuwa, Ni muhimu kuelewa kuwa kila taka inayotupwa baharini, kila eneo la mikoko linaloharibiwa na kila kitendo kinachoharibu mazingira ya matumbawe kinaweza kuongeza changamoto katika mifumo ya maisha ya viumbe wa baharini.
Anasema , Kulinda bahari ni kulinda chakula, kipato na maisha ya wananchi Rasilimali za bahari si urithi wa kizazi kimoja, bali ni tunu inayopaswa kuhifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Post a Comment