WANAHABARI OMAN, ZNZ KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KITAALUMA

Na Maryam Nassor

UJUMBE wa Chama cha Waandishi wa Habari kutoka Oman (OJA) umefika visiwani Zanzibar kwa ajili ya kushiriki kongamano na ziara maalum ya kikazi, yenye lengo la kubadilishana uzoefu, kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kitaaluma, pamoja na kutangaza fursa za utalii na uwekezaji kati ya Oman na Zanzibar.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip, Rais wa Chama cha Waandishi wa Habari Oman (OJA), Ahmed Ali Araimi, amesema wanahabari wana nafasi kubwa ya kutumia taaluma yao kama daraja la kuendeleza uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Oman na Zanzibar.

Amesema, wanahabari wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuangazia fursa za utalii, biashara, uwekezaji na urithi wa pamoja unaowaunganisha wananchi wa pande hizo mbili.

Amesema  kuwa, juhudi hizo zitaimarishwa kupitia kongamano litakalofanyika Oktoba 6 mwaka huu, likiwakutanisha zaidi ya wanahabari 40 kutoka Oman na Zanzibar kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kujadili namna vyombo vya habari vinavyoweza kuchangia katika kuimarisha mahusiano na fursa zilizopo kati ya pande hizo.

Rais huyo ,amesema nafasi ya wanahabari ni muhimu katika kuhakikisha uhusiano kati ya Oman na Zanzibar hauishii katika historia pekee, bali unaendelea kuwa na maana kwa kizazi cha sasa na kijacho kupitia taarifa na maudhui yanayojenga uhusiano na kuibua fursa.

Amesema, Oman na Zanzibar zina uhusiano uliodumu kwa miaka mingi kupitia biashara, utamaduni, dini, lugha na mwingiliano wa kifamilia, hivyo vyombo vya habari vinaweza kusaidia kuutangaza urithi huo na wakati huo huo kuibua fursa mpya kwa jamii za pande zote mbili.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Abdalla Mfaume, amesema kongamano hilo ni fursa muhimu ya kujenga mtandao wa kitaaluma kati ya wanahabari wa Oman na Zanzibar, huku likitoa nafasi ya kubadilishana uzoefu na kuangazia maeneo yenye fursa, ikiwemo utalii, biashara, sanaa, utamaduni na uwekezaji.

Amesema hatua nyingine inayotarajiwa ni kutiwa saini kwa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya OJA na ZPC, ambayo itawezesha kufanyika kwa mafunzo, ziara za kikazi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za pamoja.

Amesema, ushirikiano huo unalenga kuimarisha taaluma ya wanahabari na kutumia sekta ya habari kama nyenzo ya kukuza zaidi uhusiano wa Oman na Zanzibar.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ), Khairat Ali, amesema hatua hiyo ni nzuri kwa kuwa TAMWA ZNZ imekuwa ikiwawezesha waandishi wa habari kupitia mafunzo mbalimbali yanayolenga kuwaongezea ujuzi na uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema ushirikiano kati ya wanahabari wa Oman na Zanzibar utatoa fursa zaidi kwa waandishi kujifunza kutoka kwa wenzao na kuongeza uwezo wao kitaaluma.

Mkutano huo wa waandishi wa habari kutoka Oman na Zanzibar umeelezwa kuwa ni jukwaa muhimu la kujadili masuala mbalimbali na kubadilishana uzoefu, huku kongamano hilo likitarajiwa kufunguliwa rasmi Jumanne, Oktoba 6  ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa ni  Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar .

 

No comments

Powered by Blogger.