Ripoti ya SWIL yaonesha Wanawake Wamepiga Hatua Katika Uongozi
Na Maryam Nassor
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ)
kimewakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya wanawake na uongozi kujadili
ripoti ya tathmini ya mradi wa Kuwawezesha Wanawake katika Uongozi (SWIL),
unaotarajiwa kumalizika mwezi Desemba mwaka huu.
Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka TAMWA ZNZ, Mohamed Khatib Mohamed,
amesema mradi huo umepata mafanikio
makubwa katika kuwawezesha wanawake
kushiriki na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Amesema wakati mradi huo ulipoanza, wanawake walikabiliwa na vikwazo
mbalimbali vilivyowazuia kushiriki kikamilifu katika uongozi, ikiwemo
changamoto za sera, ukosefu wa elimu kuhusu masuala ya uongozi pamoja na mifumo
dume ambayo yalikuwa ni kizuizi kikubwa.
Mohamed amesema kwa sasa ushiriki wa wanawake katika uongozi umefikia
asilimia 38, hatua ambayo, licha ya kutofikia uwiano unaotarajiwa,
inaonesha maendeleo ikilinganishwa na hali iliyokuwepo kabla ya utekelezaji wa
mradi.
“Na hili limetokana na elimu kubwa tunayoitoa kupitia waandishi wa habari
tunaowapa mafunzo na hatimaye kuyafikisha katika jamii na kuwaelimisha wanaume
kuondokana na mfumo dume,” amesema.
Amesema tathmini hiyo imeonesha umuhimu wa kuendelea kushirikiana na
vyama vya siasa, hasa katika kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuwajengea uwezo
wa kushiriki katika uongozi.
Kwa mujibu wa Mohamed, madhumuni ya tathmini ya mwisho ya mradi yalikuwa kubaini kiwango ambacho SWIL umeweza kufikia matokeo yaliyokusudiwa, kwa kulinganisha takwimu za mwisho wa mradi na matokeo ya tathmini ya awali pamoja na malengo yaliyowekwa katika Mfumo wa Matokeo wa Mradi.
Kwa upande wake, mshiriki wa tathmini hiyo kutoka Chama cha ACT
Wazalendo, Halima Ibrahim, amesema ni muhimu mradi huo unapomalizika
kuwepo kwa mradi mwingine utakaoendeleza kazi iliyofanywa na SWIL.
Amesema mradi huo umewasaidia wanawake kujenga uwezo, kujiamini na kupata
hamasa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya vyama vyao na katika
maeneo yao.
“Kupitia mradi huu mimi ni mnufaika nambari moja ambaye nimefaidika na mafunzo mbalimbali ya uongozi na kunijengea ujasiri wa kugombea nafasi mbalimbali za ndani ya chama lakini pia katika jimbo. Hivyo tunaomba miradi kama hii iendelee,” amesema Halima.
Naye Diwani wa Wadi ya Kihinani, Salama Masinga, amesema kupitia
mradi wa SWIL amepata mafunzo mbalimbali yaliyomsaidia kupata ujasiri wa
kugombea nafasi za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
Amesema mradi huo umeleta mafanikio kwa wanawake, kwani baadhi yao hapo
awali walikuwa hawana ujasiri wa kujitokeza hadharani na kugombea nafasi za
uongozi.
Salama amesema, wanawake kwa sasa
wameongezeka ujasiri wa kushiriki katika ushindani wa nafasi za uongozi pamoja
na wanaume.
Kwa upande wake, Mtekelezaji Mwenza wa Mradi wa SWIL kutoka Jumuiya ya
Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Mwanaisha Mustafa Makame, amesema
kupitia mradi huo wameweza kuchambua sera na sheria mbalimbali zinazoweza kuwa
kikwazo kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi.
Amesema pamoja na mradi wa SWIL kumalizika, juhudi za kuwawezesha
wanawake kiuchumi zitaendelea ili kusaidia kuondoa vikwazo vinavyowakabili
wanawake katika safari yao ya kushiriki katika uongozi.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mshauri Elekezi, Richard Ulugumu,
amesema mkutano huo ulilenga kutoa tathmini ya kina kuhusu ufanisi wa mradi,
matumizi bora ya rasilimali, mchango wake katika mabadiliko, umuhimu, uendelevu
pamoja na kuweka kumbukumbu ya mafunzo yaliyopatikana wakati wa utekelezaji.
Amesema tathmini ya mwisho ya mradi ilifanyika katika wilaya zote 11 za
Zanzibar, ikihusisha kipindi cha utekelezaji kuanzia Januari 2024 hadi Agosti
2026, katika maeneo ya Unguja na Pemba.
Richard amesema tathmini ya awali iliyofanyika mwaka 2024 ilibaini
kiwango cha chini cha kujiamini miongoni mwa wanawake, hali ambayo kwa kiasi
kikubwa ilihusishwa na mila, desturi na mifumo ya kijamii inayotawaliwa na
mfumo dume.
“Tathmini ya awali ya mwaka 2024 ilibaini kiwango cha chini cha kujiamini
miongoni mwa wanawake, ambacho kwa kiasi kikubwa kilihusishwa na mila, desturi
na mifumo ya kijamii inayotawaliwa na mfumo dume,” amesema.
Mkutano huo wa tathmini uliwakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya
wanawake na uongozi, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, washirika wa mradi
pamoja na wahamasishaji jamii, kujadili
rasimu ya tathmini ya Mradi wa SWIL unaotarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2026.
Post a Comment