WATENDAJI TAMWA ZNZ WAPATIWA MAFUNZO YA USALAMA WA KISAIKOLOJIA
NA MARYAM NASSOR
WATENDAJI wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar
(TAMWA ZNZ) wamepatiwa mafunzo kuhusu usalama na ustawi wa kisaikolojia,
yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kutambua na kujikinga dhidi ya athari za
kisaikolojia zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa Chama hicho,
Tunguu Unguja yamelenga kuwapa washiriki uelewa wa namna ya kutunza
afya yao ya kisaikolojia, kutambua dalili za changamoto za kihisia zinazoweza
kujitokeza katika mazingira ya kazi pamoja na kuwasaidia wenzao wanapopitia
hali ngumu.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na Afisa Programu wa TAMWA ZNZ, Khairat Ali, kufuatia mafunzo ya wakufunzi (TOT) kuhusu usalama na ulinzi wa waandishi wa habari aliyoyapata kupitia Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Khairat alisema waandishi wa habari
na watendaji wa vyombo vya habari hukutana na mazingira mbalimbali yenye
changamoto, ikiwemo taarifa zenye msongo wa mawazo, hivyo kuna umuhimu wa kuwa
na uelewa wa namna ya kulinda ustawi wao wa kisaikolojia.
Alisema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uelewa kuhusu usalama wa waandishi wa habari na kuhakikisha watendaji wanakuwa na uwezo wa kutambua athari zinazoweza kujitokeza katika mazingira ya kazi na kuchukua hatua zinazofaa mapema.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Zaina Mzee, alisema mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa umuhimu wa kutambua hali yake ya kisaikolojia na kutafuta msaada pale anapopitia changamoto zinazoweza kuathiri utendaji wake wa kazi.
Kwa upande wake, Salim Ameir, alisema mafunzo hayo yamempa uelewa mpya kuhusu umuhimu wa kuwajali na kuwasaidia wafanyakazi au watu wengine wanapopitia kipindi kigumu, akisisitiza kuwa mazingira bora ya kazi yanahitaji ushirikiano na kuelewana.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yanatarajiwa kuwawezesha watendaji wa TAMWA ZNZ
kuimarisha usalama na ustawi wao wa kisaikolojia, huku wakitumia maarifa
waliyoyapata katika mazingira ya kazi na kuwasaidia wengine wanaoweza kukutana
na changamoto mbalimbali za kisaikolojia.
Post a Comment