Mafunzo ya CADiR Yaanza Kuzaa Matunda , Kaskazini 'B' Unguja
Na Salim Ameir
Mafunzo ya kilimo cha mbogamboga
yanayotolewa kupitia Mradi wa CADiR chini ya Mpango wa Uwezeshaji Kiuchumi
(EEP), yameanza kuzaa matunda kwa baadhi ya vikundi vya Kijaluba katika Wilaya
ya Kaskazini Unguja.
Hayo yamebainika katika ziara ya kutembelea vikundi viwili vya Kijaluba,
ambavyo ni Kikundi cha Jitihada cha Kidanzini na Kikundi cha Tuwezeshwe
cha Kiombamvua, ambapo wanufaika wameanza kutumia ujuzi walioupata kupitia
mafunzo hayo kuanzisha kilimo cha mbogamboga kama shughuli ya kuongeza kipato.
Akizungumza wakati wa ziara ya kuangalia maendeleo ya kikundi chao,
Mwenyekiti wa Kikundi cha Jitihada cha Kidanzini, Fatma Mohamed Hamdu,
amesema kikundi hicho kinatumia eneo la ekari moja kulima mazao mbalimbali ya
mbogamboga.
Amesema mazao yanayolimwa ni pamoja na mchicha, pilipili boga na pilipili
za mwendokasi, huku hadi sasa takribani nusu ekari ya eneo hilo ikiwa tayari
imelimiwa.
Hata hivyo, amesema changamoto kubwa inayowakabili wanachama wa kikundi hicho ni ukosefu wa mfumo wa uhakika wa umwagiliaji, jambo linaloweza kuathiri uzalishaji na maendeleo ya shughuli zao za kilimo.
Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi cha Tuwezeshwe cha Kiombamvua, Raya
Massoud Mohamed, amesema kikundi hicho kinatumia eneo la takribani nusu
ekari kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga na tayari kimeanza kuvuna baadhi ya
mazao.
Amesema mazao yaliyokwishaanza kuvunwa ni pamoja na mchicha na bamia,
hali ambayo imewapa wanachama hamasa na mwamko wa kuendelea kufanya kazi kwa
bidii ili kuinua uchumi wao pamoja na familia zao.
“Kwa sasa tumeanza kuvuna baadhi ya mazao yetu, yakiwemo mchicha na
bamia. Hii ni hatua nzuri kwa wanakikundi kwa sababu imeanza kuwajengea mwamko
wa kufanya kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wao na familia zao,” amesema Raya.
Katika ziara hiyo, timu iliyotembelea kikundi hicho pia ilifanikiwa
kununua baadhi ya mbogamboga zilizokuwa tayari zimevunwa.
Hatua hiyo inaonesha kuwa wanufaika wa mafunzo hayo wameanza kuvuka
kutoka hatua ya kupata maarifa pekee na kuingia katika uzalishaji halisi
unaoweza kuwaongezea kipato na kuimarisha maisha yao.
Pamoja na mafanikio hayo, changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya
umwagiliaji bado inaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa vikundi hivyo.
Mmoja wa wanachama wa kikundi hicho, Amina Juma, amesema wanachama
hulazimika kutumia madumu kusafirisha maji hadi mashambani, hali inayosababisha
kazi kubwa na kutumia muda mwingi.
Amesema changamoto hiyo ni kubwa zaidi kwa baadhi ya wanachama wenye
ulemavu, ambao hupata ugumu wa kusafirisha maji kwa mikono kwenda katika maeneo
ya kilimo.
Kutokana na hali hiyo, vikundi hivyo vimeomba kusaidiwa kupata mabomba ya
kusafirisha maji, vifaa rahisi vya umwagiliaji pamoja na jenereta ndogo za
kusukuma maji.
“Mahitaji haya yakipatiwa ufumbuzi, yanaweza kusaidia kupunguza kazi
kubwa inayofanywa na wanachama katika kusafirisha maji kwa mikono na kuwezesha
kilimo kufanyika kwa ufanisi zaidi,” amesema Amina.
Akizungumzia maendeleo ya vikundi hivyo, Afisa Miradi kutoka TAMWA ZNZ, Zaina
Mzee, amesema hatua zilizofikiwa zinaonesha kuwa mafunzo yanayotolewa
kupitia Mradi wa CADiR-EEP yameanza kugeuka kuwa shughuli halisi za kiuchumi
kwa wanufaika.
Amesema kupitia mafunzo hayo, wanufaika wameanza kutumia maarifa na ujuzi
walioupata kuanzisha shughuli za kilimo zinazoweza kuwapatia kipato na
kuchangia katika kuimarisha uchumi wa familia zao.
Zaina amesema , kuwepo kwa
miundombinu bora ya umwagiliaji kunaweza kusaidia vikundi hivyo kuongeza
uzalishaji wa mbogamboga, kupanua maeneo yao ya kilimo na hatimaye kuongeza
kipato cha wanachama.
Amesema kuwa, Mafanikio yanayoanza kujitokeza katika vikundi vya Jitihada
cha Kidanzini na Tuwezeshwe cha Kiombamvua yanaonesha umuhimu wa kuunganisha
mafunzo ya ujuzi na uwezeshaji wa vitendo.
Aidha amesema kuwa ,changamoto ya maji na ukosefu
wa vifaa vya umwagiliaji vinaendelea kuhitaji ufumbuzi ili kuhakikisha juhudi
na maarifa yaliyopatikana kupitia mafunzo hayo yanageuzwa kuwa uzalishaji
mkubwa na endelevu.
Kwa sasa, hatua ya vikundi hivyo kuanza kulima na kuvuna mazao ni ishara
ya matumaini kwamba mafunzo ya CADiR-EEP yanaendelea kuwa na mchango katika
kuwajengea wanufaika uwezo wa kutumia fursa zilizopo kuimarisha uchumi wao.
Post a Comment