VIKWAZO VINAVYOWARUDISHA NYUMA WANAWAKE KUTOFIKIA USAWA WA KIJINSIA KATIKA UONGOZI
Na Maryam Nassor
Licha ya ongezeko la wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi, safari ya kufikia uwiano wa 50 kwa 50 kati ya wanawake na wanaume
katika nafasi za maamuzi bado inaonekana kuwa ndefu.
Kwa miaka mingi, wanawake wamehamasishwa kujitokeza, kujiamini na
kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi. Mafunzo yametolewa, sera
zimewekwa na taasisi mbalimbali zimeendelea kutekeleza programu za kuwawezesha
wanawake. Hata hivyo, takwimu zinaendelea kuibua swali kubwa: ikiwa wanawake
wanajitokeza na kujitoa kugombea, kwa nini bado hawafikii uwiano wa 50/50?
Takwimu za nafasi za uongozi zinaonesha picha ya matumaini kwa upande
mmoja, lakini changamoto kubwa kwa upande mwingine.
Katika nafasi za uteuzi na uongozi wa kiutawala, wanawake
wanashikilia takribani asilimia 40, sawa na wanawake 865 kati ya
viongozi 2,186.
Hata hivyo, hali ni tofauti katika nafasi za uongozi zinazopatikana
kupitia uchaguzi. Katika kipindi cha 2025–2030, wanawake ni 35 kati
ya viongozi 210, sawa na asilimia 17, ikilinganishwa na asilimia 18
katika kipindi cha 2020–2025.
Kwa ujumla, ukijumlisha nafasi za uteuzi, kiutawala na zile
zinazopatikana kupitia uchaguzi, wanawake wanashikilia takribani asilimia 38
ya nafasi za uongozi, huku wanaume wakiendelea kuwa wengi kwa asilimia 62.
Hapo ndipo swali kubwa linapoibuka: Kwa nini wanawake wengi
wanajitokeza kugombea na kujitoa kuingia katika uwanja wa kisiasa, lakini bado
wanashindwa kufikia uwiano wa 50/50 katika nafasi za uongozi?
Kwa wanawake waliowahi kuingia katika uwanja wa ushindani wa kisiasa,
jibu linaonekana kuwa ni mchanganyiko wa changamoto za kiuchumi, mitazamo ya
kijamii, mazingira ya kisiasa na mfumo wa ushindani wenyewe.
Kujitokeza pekee haitoshi
Nadhira Ali Haji kutoka Chama cha ADC ni miongoni mwa wanawake
walioamua kujitokeza na kuingia katika uwanja wa kuwania nafasi za uongozi. Mwaka
2025 aligombea ubunge jimbo la Malindi mkoa wa Mjini Unguja.
Nadhira anasema kuwa, mwanamke anapoamua kugombea hukutana na
mazingira tofauti na yale yanayowakabili wagombea wanaume. Mbali na kuwa na
sera, maono na uwezo wa kuwashawishi wananchi, mwanamke hulazimika pia
kupambana na mitazamo ya jamii inayotilia shaka uwezo wake wa kuongoza.
Anasema, Changamoto kubwa, katika baadhi ya maeneo, jamii bado inaendelea
kuiona siasa na uongozi kama eneo linalowafaa zaidi wanaume.
“ Hali hiyo inaweza kumfanya mwanamke anayejitokeza kugombea kupimwa kwa
vigezo tofauti. Badala ya wananchi kuangalia uwezo wake, sera anazozitetea na
maono aliyonayo kwa jamii, wakati mwingine hujikuta akitathminiwa kupitia
maisha yake binafsi, familia yake au namna anavyoishi” anasema Nadhra.
Kwa mantiki hiyo, kujitokeza kwa wanawake wengi kugombea ni hatua muhimu,
lakini kujitoa pekee hakutoshi ikiwa mazingira ya ushindani hayatoi fursa sawa
kwa wanawake na wanaume.
Gharama za siasa na ukosefu wa
rasilimali
Laila Abubakar kutoka chama cha NCCR Mageuzi ni miongoni mwa wanawake waliojitokeza kuwania
nafasi ya urais katika chama hicho mwaka
2025 lakini hawakufanikiwa kushinda.
Anasema, Kwa wanawake wengi,
changamoto ya kiuchumi imeendelea kuwa miongoni mwa vikwazo vikubwa katika
safari ya kisiasa.
Anasema, Kampeni zinahitaji fedha
kwa ajili ya usafiri, mawasiliano, mikutano na shughuli mbalimbali za kuwafikia
wapiga kura. Kwa mwanamke asiye na uwezo mkubwa wa kiuchumi, gharama hizi
zinaweza kuwa kikwazo kikubwa.
“ Wanawake wengi huingia katika ushindani wa kisiasa wakiwa na rasilimali
chache, hali inayoongeza pengo kati yao na wagombea wenye uwezo mkubwa wa
kifedha” anasema.
Mwanamke anaweza kuwa tayari kugombea na kuwa na uwezo wa kuongoza,
lakini maandalizi ya kisiasa, uwezo wa kupata rasilimali na mazingira ya
ushindani vinaweza kuamua kwa kiwango kikubwa safari yake.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) kinaeleza kuwa wanawake wanaotamani
kuingia katika uongozi hukabiliana na changamoto mbalimbali, zikiwemo vikwazo
vya kifedha, kampeni za kuwachafua kisiasa, mfumo wa kisiasa unaotawaliwa zaidi
na wanaume pamoja na mitazamo hasi ya jamii.
Mitazamo ya jamii bado ni kikwazo
Kwa Amana Suleiman kutoka chama cha UPPD, anasema kujitokeza kwa mwanamke kugombea nafasi ya
uongozi ni jambo linalohitaji ujasiri mkubwa.
Anasema , Ingawa wanawake
wameendelea kupiga hatua katika elimu, biashara na maeneo mbalimbali ya
kijamii, bado kuna sehemu ya jamii inayobeba fikra kwamba mwanamke anapaswa
kubaki zaidi katika majukumu ya familia kuliko kushiriki kikamilifu katika
siasa.
Aidha, majukumu ya malezi na kazi za nyumbani yanaweza kupunguza muda na
nafasi ya mwanamke kushiriki katika shughuli za kisiasa.
Anasema kuwa, Changamoto nyingine
ni lugha na mashambulizi yanayoweza kuelekezwa kwa wanawake wanaojitokeza
katika uwanja wa kisiasa. Hali hiyo inaweza kuwakatisha tamaa baadhi ya
wanawake, hasa wale wanaoingia kwa mara ya kwanza katika ushindani wa uchaguzi.
Anaeleza kuwa, kushindwa kwa baadhi ya wanawake waliogombea
hakumaanishi kuwa hawakuwa na uwezo wa kuongoza. Badala yake, kuna haja ya
kuangalia kwa kina mazingira ambayo wanawake wanayakuta wanapoamua kuingia
katika uwanja wa ushindani wa kisiasa.ili kusaidia kuviondosha
vikwazo hivyo.
Takwimu zinaonesha pengo kubwa
Tofauti kati ya nafasi za uteuzi na zile zinazopatikana kupitia uchaguzi
zinaonesha wazi changamoto iliyopo.
Katika nafasi za kiutawala na uteuzi, wanawake wamefikia karibu asilimia 40.
Kwa mfano, wanawake ni asilimia 56 ya Naibu Mawaziri, asilimia 40 ya
Makatibu Wakuu, asilimia 38 ya Majaji na asilimia 42 ya Wajumbe
wa Kamati za Shehia.
Lakini katika nafasi zinazopatikana kupitia uchaguzi, uwakilishi wa
wanawake umebaki katika kiwango cha asilimia 17.
Pengo hili linaibua picha muhimu. Inaonekana wanawake wanaweza kupata
mafanikio makubwa zaidi pale ambapo kuna sera, mifumo na maamuzi yanayozingatia
usawa wa kijinsia.
Changamoto kubwa zaidi inaonekana katika ushindani wa moja kwa moja wa
uchaguzi, ambako mwanamke hukutana uso kwa uso na vikwazo vya kiuchumi,
mitazamo ya jamii na mazingira ya kisiasa.
Hii inaonesha kuwa suala la kuongeza idadi ya wanawake katika uongozi
haliwezi kuachwa kwenye hamasa pekee. Kunahitajika mazingira yanayowawezesha
wanawake kushindana kwa haki na usawa.
Mikataba ya kikanda na kimataifa
inasema nini?
Mapambano ya kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika uongozi
hayapo Zanzibar pekee. Ni sehemu ya ajenda kubwa ya kikanda na kimataifa.
Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hususan Lengo
la 5.5, yanazitaka nchi
kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu na kwa ufanisi katika maamuzi na
kupata fursa sawa za uongozi katika maisha ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Barani Afrika, Itifaki ya Maputo, hususan Ibara ya 9, inasisitiza
umuhimu wa ushiriki sawa wa wanawake katika maisha ya kisiasa na michakato ya
maamuzi.
Itifaki hiyo inazitaka nchi kuchukua hatua chanya za kuongeza ushiriki na
uwakilishi wa wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi.
Kwa upande wa ukanda wa Kusini mwa Afrika, SADC, kupitia mikakati
yake ya jinsia na maendeleo, imeendelea kusisitiza umuhimu wa kufikia
uwakilishi sawa wa wanawake na wanaume katika nafasi za maamuzi.
Lengo ni kuhakikisha wanawake wanapata nafasi kubwa zaidi ya kushiriki
katika maamuzi yanayoathiri maisha ya wananchi.
Makubaliano haya yanaonesha wazi kuwa ushiriki wa wanawake katika uongozi
si suala la kuwapa upendeleo, bali ni jambo la haki, usawa na maendeleo
jumuishi.
Jamii haiwezi kusema imefikia maendeleo kamili ikiwa kundi kubwa la
wananchi wake halipati nafasi sawa ya kushiriki katika kufanya maamuzi.
SWIL yajenga ujasiri na kuandaa
wanawake kwa uongozi
Katika kukabiliana na changamoto hizo, TAMWA ZNZ, kupitia Mradi wa
Strengthening Women in Leadership (SWIL), kinaendelea kuchukua hatua za
kuwajengea wanawake uwezo na kuwahamasisha kushiriki katika uongozi.
Kupitia Afisa Programu wa Mradi wa SWIL, Khairat Ali anaeleza kuwa mradi huo unalenga kuongeza
ushiriki na ushawishi wa wanawake katika michakato ya kidemokrasia na nafasi
mbalimbali za maamuzi.
Anasema, Miongoni mwa shughuli
zinazotekelezwa ni kuwapatia wanawake mafunzo ya uongozi, ushiriki wa
kidemokrasia, kuwajengea uwezo wa kujiamini na kuhamasisha jamii kuondoa
mitazamo inayowazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa.
Mradi huo pia unatekelezwa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali,
zikiwemo ZAFELA, JUWAUZA na PEGAO, kwa lengo la kuhakikisha wanawake
kutoka makundi tofauti, wakiwemo wanawake wenye ulemavu, wanapata nafasi ya
kushiriki katika uongozi.
Kwa mujibu wa Khairat, katika mwaka 2025 programu ya SWIL iliwafikia
wanawake wengi waliokuwa na matarajio ya kuingia katika uongozi, huku mamia
wakiteuliwa na vyama vyao kugombea nafasi mbalimbali.
Aidha anasema kuwa , Juhudi hizo zinaonesha umuhimu
wa kuendelea kujenga kundi kubwa la wanawake wenye uwezo, maarifa na utayari wa
kuwania nafasi za maamuzi.
Wanaume nao wanapaswa kuwa sehemu ya
mabadiliko
Kufikia uwiano wa 50/50 si jukumu la wanawake pekee.
Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, Machano Othman Said, anaeleza
kuwa wanaume wana nafasi kubwa ya kuunga mkono ushiriki wa wanawake katika
uongozi kwa kubadilisha mitazamo na kusaidia kuondoa vikwazo vinavyowazuia
wanawake kushiriki kwa uhuru.
Anaeleza kuwa jamii haiwezi kufikia maendeleo endelevu ikiwa zaidi ya
nusu ya wananchi wake hawapati nafasi sawa ya kushiriki katika maamuzi.
“Wanawake wanapaswa kupewa nafasi ya kuongoza kwa sababu wana uwezo,
maarifa na uzoefu unaohitajika katika kutatua changamoto za jamii,”
anasisitiza.
Safari ya 50/50 bado inaendelea
Mchambuzi wa Maswala ya siasa na Uongozi Zanzibar Almass Mohamed anasema, takwimu za uongozi kwa wanawake ni sehemu ya picha pana ya wanawake
wanaojitokeza kuvunja ukuta wa kihistoria wa ushiriki mdogo wa wanawake katika
siasa na uongozi.
Anasema, Takwimu za asilimia 38 ya wanawake katika nafasi za uongozi
kwa ujumla zinaonesha kuwa hatua zimepigwa. Lakini asilimia 17 pekee
katika nafasi zinazopatikana kupitia uchaguzi ni ishara kwamba bado kuna
kazi kubwa ya kufanya.
Post a Comment