Mtaala wa Uongozi Vyuo Vikuu: Njia Mpya ya Kuwajengea Wanawake Ujasiri wa Kushika Madaraka


Na Maryam Nassor

Kwa muda mrefu, wanawake wengi wenye uwezo na sifa za kuwa viongozi wameendelea kubaki nyuma katika kushiriki kikamilifu kwenye nafasi za maamuzi. Ingawa wanawake wamepiga hatua katika elimu, biashara, siasa na ajira, bado uwakilishi wao katika baadhi ya nafasi za juu za uongozi unaendelea kuwa mdogo.

Changamoto ya kutokujiamini, ukosefu wa maarifa kuhusu uongozi na siasa, mitazamo hasi ya jamii pamoja na mazingira yasiyo rafiki kwa wanawake wanaotamani kugombea nafasi za uongozi ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchangia hali hiyo.

 hatua ya kuandaa mtaala maalumu wa kozi za uongozi kwa wanawake na wasichana katika vyuo vikuu inaonekana kuwa mwanzo wa safari mpya ya kuwaandaa viongozi wanawake mapema kabla hawajaingia kikamilifu katika jamii na ulimwengu wa kazi.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ), kwa kushirikiana na Jumuiya ya Watu Wasioona Zanzibar (ZANAB), Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) pamoja na wadau wengine, wameanza mchakato wa kuandaa rasimu ya mtaala wa mafunzo ya uongozi kwa wanawake na wasichana.

Mtaala huo unatarajiwa kutumika katika kutoa kozi fupi za uongozi chuoni, kwa lengo la kuwajengea wanawake maarifa, uwezo na ujasiri wa kushiriki katika nafasi mbalimbali za maamuzi.

Kuandaa viongozi kabla ya kuingia kwenye uwanja wa maamuzi

Akifungua kikao cha awali cha kujadili rasimu ya mtaala huo kilichofanyika katika Kampasi ya SUZA Tunguu, kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Dk. Said Juma alisema bado kuna pengo kubwa la uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi katika taasisi mbalimbali.

Alisema mtaala huo utakuwa muhimu katika kuwasaidia wanawake kupata maarifa na ujasiri unaohitajika ili kujitokeza, kuongoza na kugombea nafasi mbalimbali.

“Naamini kozi hii ni muhimu na itasaidia kupunguza pengo kubwa lililopo katika nafasi za uongozi kwa wanawake nchini,” alisema Dk. Said.

Kwa mtazamo wake, vyuo vikuu vina nafasi muhimu  katika kuandaa viongozi wa baadaye. Hivyo, kuwapa wanafunzi wanawake mafunzo ya uongozi wakati wakiwa bado chuoni kunaweza kuwasaidia kuingia katika maisha ya kazi na huduma za umma wakiwa tayari kushiriki katika maamuzi.

Alisema hatua hiyo pia inaunga mkono jitihada za kufikia usawa wa kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

Kutoka darasani hadi kwenye nafasi za uongozi

Kwa wanafunzi wanawake, kozi maalumu ya uongozi inaweza kuwa zaidi ya kupata cheti baada ya kumaliza mafunzo. Inaweza kuwa jukwaa la kujifunza namna ya kuzungumza mbele ya watu, kufanya maamuzi, kushughulikia changamoto, kujenga mitandao na kujiamini.

Mwanafunzi  Asha Mohamed  kutoka  SUZA,  anasema mafunzo ya aina hiyo yanaweza kuwasaidia wanafunzi wanawake kuondokana na hofu ya kujitokeza katika nafasi mbalimbali za uongozi.

“Wanafunzi wengi wanawake tuna uwezo mkubwa, lakini wakati mwingine tunakosa ujasiri wa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi. Kozi kama hii inaweza kutusaidia kujifunza namna ya kujiamini na kueleza uwezo wetu,” anasema.

Anasema wanawake wengi huanza kuogopa uongozi kabla hata hawajajaribu kugombea, jambo ambalo linaweza kusababishwa na mazingira ya kijamii na dhana kwamba baadhi ya nafasi za uongozi zinawafaa zaidi wanaume.

Kwa upande wake, mwanafunzi mwingine wa kike, Mariam Ali, alisema vyuo vikuu vinapaswa kuwa sehemu ya kuwalea viongozi wanawake kwa vitendo na si kusubiri wanafunzi wamalize masomo ndipo waanze kutafuta mafunzo ya uongozi.

“Tunapokuwa chuoni tunapata elimu ya taaluma zetu, lakini pia tunahitaji kujifunza uongozi, mawasiliano na namna ya kushiriki katika maamuzi. Hii inaweza kutusaidia hata katika kugombea nafasi za serikali za wanafunzi na baadaye kwenye jamii,” anasema.

Anasema kupitia mafunzo hayo, wanawake wanaweza kujifunza kuwa kushika nafasi ya uongozi si suala la jinsia, bali kunahitaji uwezo, maarifa, maadili, uwajibikaji na utayari wa kuhudumia jamii.

W-LEAD na safari ya kuwajengea wanawake uwezo

Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Nairat Abdullah Ali, anasema mtaala huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa W-LEAD unaotekelezwa kwa kushirikiana na ZANAB.

 Anasema kuwa, Lengo la mradi huo ni kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi na maamuzi.

Anasema uzoefu wa utekelezaji wa mradi umeonesha umuhimu wa kuanza kuwajengea uwezo wanawake katika taasisi za elimu ya juu, kwa kuwa vyuo vikuu ndiyo sehemu zinazowaandaa viongozi wa baadaye.

“Katika uchaguzi uliopita tumeona uwakilishi wa wanawake katika nafasi za udiwani ukiongezeka kwa asilimia 25, jambo ambalo halikuwahi kushuhudiwa katika miaka ya nyuma,” anasema Nairat.

 Ameongeza  kuwa, Hatua ya kuandaa mtaala wa  uongozi  katika vyuo vikuu inaweza kusaidia kuhakikisha mafunzo hayo hayaishii kwa kundi moja la wanawake, bali yanaendelea kuwafikia vizazi tofauti vya wanafunzi.

Kozi fupi yenye manufaa ya muda mrefu

Meneja wa Kitengo cha Mawasiliano wa TAMWA ZNZ, Sophie Ngalapy, alipendekeza kozi hiyo iendelee kutolewa kama mafunzo ya muda mfupi yanayolenga kuwajengea washiriki uwezo wa kujiamini, kuongoza na kugombea nafasi mbalimbali.

Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Msingi na Mafunzo ya Uongozi  kutoka SUZA, Abdul Rahman Khamis, alisema kozi hiyo inapendekezwa kufundishwa kwa muda wa wiki mbili na wahitimu watatunukiwa vyeti vinavyotambuliwa rasmi.

 Anasema , kwa awamu ya kwanza, kozi hiyo inatarajiwa kutolewa bila malipo kwa walimu na wanafunzi wa SUZA kabla ya kupanuliwa kwa wananchi wengine wenye uhitaji wa mafunzo hayo.

Anasema kuwa,  mafunzo hayo yanapaswa kujumuisha maeneo muhimu kama vile maadili ya uongozi, ujasiri, mawasiliano, utatuzi wa migogoro, usimamizi wa rasilimali, uongozi wa kisiasa, utetezi wa masuala ya jamii na namna ya kushiriki katika michakato ya uchaguzi.

Mikataba ya kikanda na kimataifa

Jitihada za kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi zinaungwa mkono pia na mikataba na makubaliano mbalimbali ya kimataifa na kikanda.

Miongoni mwa nyaraka muhimu ni Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW), unaosisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vinavyowazuia wanawake kushiriki katika maisha ya kisiasa na  kiuongozi.

 Azimio na Jukwaa la Utekelezaji la Beijing la mwaka 1995 liliweka msisitizo mkubwa katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika mamlaka na kufanya maamuzi.

Katika ngazi ya kimataifa, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan Lengo la Tano kuhusu usawa wa kijinsia, yanahimiza kuhakikisha wanawake wanapata fursa kamili na sawa za kushiriki katika uongozi na maamuzi katika maisha ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wa Afrika, Itifaki ya Maputo na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu kuhusu Haki za Wanawake barani Afrika vinaweka msisitizo katika kulinda na kukuza haki za wanawake, ikiwemo haki ya kushiriki katika maisha ya kisiasa na michakato ya maamuzi.

Malengo ya usawa wa kijinsia yaliyowekwa katika mifumo mbalimbali ya maendeleo ya Afrika yanaendelea kuhimiza nchi kuongeza uwakilishi wa wanawake katika taasisi za maamuzi.

Kwa hiyo, mtaala wa kozi za uongozi kwa wanawake katika vyuo vikuu unaweza kuwa sehemu ya utekelezaji wa vitendo wa ahadi hizo za kitaifa, kikanda na kimataifa.

Kujumuisha wanawake wenye ulemavu

Mkurugenzi wa ZANAB, Rukia Saleh Ali, alisema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha wanawake vijana, wakiwemo wenye ulemavu, wanapata fursa sawa za kushiriki katika mafunzo hayo.

Alisisitiza umuhimu wa kuweka mazingira jumuishi na rafiki kwa watu wenye ulemavu ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.

Hili ni eneo muhimu, kwani wanawake wenye ulemavu wanaweza kukumbana na changamoto za aina mbili—ubaguzi wa kijinsia na vikwazo vinavyotokana na mazingira yasiyo rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Mwanafunzi mwenye ulemavu, Zainab Salum, alisema mafunzo ya uongozi yanapaswa kupatikana kwa wanafunzi wote bila kujali hali zao.

“Wanawake wenye ulemavu  tuna ndoto na uwezo wa kuwa viongozi. Tukipata mazingira rafiki na mafunzo sahihi, tunaweza kushiriki katika nafasi za uongozi kama wengine,” alisema.

Kupima matokeo ya mafunzo

Mtaalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa TAMWA ZNZ, Mohamed Hatib Mohamed, anasema mradi wa W-LEAD umefikia asilimia 90 ya utekelezaji na tayari umefanikiwa kuwajengea uwezo wanawake viongozi na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Ansema kupitia utekelezaji wa mtaala huo katika chuo cha  SUZA na Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) , wanatarajia kuona ongezeko la wanawake wenye uwezo, sifa na kujiamini kushika nafasi za uongozi.

“Changamoto kubwa iliyokuwepo ni wanawake wengi kutokujiamini kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. Kupitia mradi huu tunawajengea uwezo ili wajitokeze kwa wingi kushiriki katika maamuzi,” anasema Mohamed.

Aidha aliishauri SUZA kuweka mfumo wa takwimu wa kufuatilia idadi ya wanawake watakaopata mafunzo hayo na maendeleo yao baada ya mafunzo.

 Anasema, Hatua hiyo inaweza kusaidia kupima kama wahitimu wa kozi hiyo wanaanza kugombea nafasi za serikali za wanafunzi, uongozi wa kijamii, taasisi za kiraia, vyama vya siasa na nafasi nyingine za maamuzi.

Uongozi unaanza kwa kuamini uwezo wako

Kwa ujumla, mtaala wa kozi za uongozi kwa wanawake katika vyuo vikuu unaweza kuwa daraja muhimu kutoka elimu ya kawaida kuelekea uongozi wa vitendo.

Kuanzisha kozi maalumu za uongozi katika taasisi za elimu ya juu kunaweza kuwapa wanafunzi wanawake maarifa na ujasiri wa kutambua kuwa nao wana nafasi katika meza za maamuzi.

Iwapo mtaala huo utatekelezwa kwa ufanisi, kwa mazingira jumuishi na kwa kufuatiliwa kwa matokeo yake, unaweza kusaidia kuzalisha kizazi kipya cha wanawake viongozi—wanawake ambao hawatasubiri kuitwa kwenye nafasi za maamuzi, bali watakuwa tayari kujitokeza, kugombea na kuongo

No comments

Powered by Blogger.