CADiR YAWAWEZESHA WANACHAMA 294 WA KIJALUBA KUANZA SAFARI YA KUJITEGEMEA KIUCHUMI
WANACHAMA 294 wa vikundi vya KIJALUBA iSAVE, wakiwemo watu 148 wenye ulemavu, wameanza kutumia ujuzi na fursa walizopata kupitia Program ya CADiR katika kuanzisha na kuimarisha shughuli za uzalishaji zinazolenga kuongeza kipato na kupunguza utegemezi.
Wanachama hao, wakiwemo wanawake 202 na wanaume 92, wamejengewa uwezo katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji kulingana na mahitaji na fursa walizobainisha kupitia tathmini ya mahitaji.
Akitoa Habari hizi Afisa mkuu wa Miradi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar ( TAMWA ZNZ) Zaina Mzee amesema , Uwezeshaji huo umejikita katika kuwawezesha wanachama kujifunza shughuli za kujipatia kipato na kutumia fursa na uwezo walionao katika kujitegemea kiuchumi ambapo wanachama 106 walifundishwa kuhusu usindikaji wa nafaka, 82 ufugaji wa kuku, 30 ufugaji wa nyuki, 26 kilimo cha mbogamboga, 20 utengenezaji wa batiki,18 uokaji wa mikate, na 13 walipata mafunzo ya ushonaji.
Amesema ,Msingi wa mafunzo hayo ulitokana na tathmini ya mahitaji ya mafunzo ya shughuli za kujipatia kipato iliyofanywa kwa wanachama 1,275 kwa Unguja na Pemba, wakiwemo wanawake 864 na wanaume 411. Tathmini hiyo ilisaidia kubainisha shughuli mbalimbali ambazo washiriki waliona zina uwezo wa kuwaongezea kipato, ikiwemo ufugaji wa kuku, biashara ndogondogo, ufugaji wa nyuki, kilimo cha mbogamboga, ushonaji, utengenezaji wa batiki, upambaji na uchoraji wa piko, utengenezaji wa sabuni na vipodozi pamoja na uuzaji wa vyakula.
Amesema kuwa, Baada ya mafunzo hayo, baadhi ya wanachama wameanza kutumia ujuzi walioupata kuzalisha bidhaa mbalimbali, zikiwemo batiki, unga wa lishe, mikoba ya ukili, bidhaa za mwani, sabuni, mafuta ya mwani, mashuka na bidhaa nyingine zinazotokana na shughuli zao za kiuchumi. Hii inaashiria hatua ya kutoka katika kujenga uwezo hadi kutumia ujuzi huo katika shughuli zinazoweza kuzalisha kipato.
Aidha amesema kuwa, Katika hatua za kuwaunganisha na masoko, baadhi ya wanachama wamepata fursa ya kushiriki katika maonesho mbalimbali, yakiwemo Maonesho ya mwaka huu ya Nanenane yaliyofanyika Kizimbani Unguja, Tamasha la Kizimkazi na Tamasha la Fahari ya Zanzibar lililofanyika Kisonge Unguja. Kupitia maonesho hayo, wameweza kutambulisha bidhaa zao kwa wateja, kukutana na wajasiriamali wengine, kujifunza zaidi namna ya kuboresha bidhaa na kujenga mahusiano yanayoweza kufungua fursa zaidi za kibiashara.
“Tunafurahi kupata fursa hii ya kuonyesha bidhaa tunazozalisha kupitia vikundi vyetu vya KIJALUBA, tunaamini fursa hii ni mwanzo mzuri wa kujiimarisha zaidi kiuchumi, kuongeza uzalishaji na kukuza biashara zetu,” alisema Nasra Nahoza ambae ni mwanachama wa Kikundi cha Mzuri Tupo kutoka Wilaya ya Kusini, Unguja.
Kwa upande wake, Fatma Abdalla Issa, mwanachama wa Kikundi cha Jembe Kazi kutoka Chake Chake, Pemba, alisema ilikuwa ni mara yake ya kwanza kushiriki katika maonesho makubwa kama Nanenane, jambo lililompa fursa ya kukutana na wateja wapya pamoja na wajasiriamali wengine na kujifunza namna ya kuboresha bidhaa ili kufikia masoko makubwa zaidi.
KIJALUBA iSAVE ni mfumo wa vikundi jumuishi wenye wanachama 30 katika kila kikundi, wakiwemo watu wenye ulemavu 15, wazazi au walezi wa watoto wenye ulemavu 10, pamoja na watu watano wasio na ulemavu. Kupitia mfumo huu, wanachama huweka akiba kwa pamoja na kupata mikopo inayoweza kutumika kama mtaji wa kuanzisha au kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.
Vikundi vya KIJALUBA iSAVE vimeanzishwa na kuendelezwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Pamoja ya Kutetea Haki za Watu Wenye Ulemavu (Collective Actions for Disability Rights – CADiR) kupitia eneo la uwezeshaji wa kiuchumi inayotekelezwa kwa ushirikiano na NAD Zanzibar, SHIJUWAZA, ZANAB na TAMWA Zanzibar
.Imetolewa na:Kitengo cha Mawasiliano TAMWA ZNZ.
Post a Comment