Utekelezaji wa sheria za mikopo ya asilimia 10 unaacha maswali kuhusu uwazi, uwajibikaji na haki kwa walengwa



Na Maryam Nassor

Kwa zaidi ya miaka minne sasa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeendelea kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mfumo wa mikopo wa 4-4-2. Lengo lilikuwa wazi kupunguza umaskini, kuongeza ajira na kuwajengea wananchi uwezo wa kujitegemea kiuchumi.

Lakini pamoja na fedha kutengwa kila mwaka na taasisi husika kueleza kuwa mabilioni ya shilingi tayari yametolewa kwa wanufaika, bado mamia ya waombaji wanaendelea kusubiri kwa miaka miwili au zaidi bila kupata majibu ya uhakika kuhusu maombi yao.

Je, tatizo ni ukosefu wa fedha, udhaifu wa mfumo wa utekelezaji, au kutotekelezwa ipasavyo kwa sheria zilizoweka msingi wa mpango huu? Uchambuzi huu unatazama pengo kati ya matakwa ya sheria na hali halisi inayowakabili walengwa katika Wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja  na Zanzibar kwa ujumla.

Tatizo Linaonekana Wapi?

Kwa Semeni Bundala, mkazi wa Mahonda, safari za kufuatilia mkopo zimekuwa sehemu ya maisha yake kwa zaidi ya miaka miwili.

Anasema kikundi chake kilikamilisha masharti yote yaliyotakiwa, kikajaza fomu na kuwasilisha nyaraka zote, lakini kila walipofika Halmashauri waliambiwa wajisajili tena kwenye mfumo mpya wa kidijitali.

"Tumekuwa tukifuatilia mikopo hii kwa muda mrefu bila mafanikio,  Kila tukifika tunaambiwa tujisajili tena. Hadi leo hatujui tatizo ni nini," anasema.

Simulizi yake inafanana na za wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wengi wanaosema hawaelewi maombi yao yalipoishia, wala hawapati taarifa rasmi zinazoeleza sababu za kuchelewa.

Tatizo kuu si kwamba wananchi hawajaomba mikopo, bali wengi wao wanasema wametimiza masharti lakini bado hawajui lini watapata fedha au kama wamekubaliwa.

Sheria inasema Nini?

Msingi wa mpango huu umewekwa wazi katika sheria.

Kifungu cha 6 cha Sheria Na. 9 ya Mwaka 2023 kinaelekeza Serikali za Mitaa kuweka mazingira ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia programu mbalimbali za maendeleo.

Aidha, Kifungu cha 9 cha Sheria Na. 2 ya Mwaka 2022 kinaipa Mamlaka ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa programu za uwezeshaji ikiwemo mfumo wa mikopo wa 4-4-2.

Sheria pia imeweka mgawanyo mahsusi wa fedha hizo ambapo asilimia nne hutengwa kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.

Kwa tafsiri ya kisheria, wajibu haukuwa tu kutenga fedha, bali kuhakikisha fedha zinawafikia walengwa kwa misingi ya usawa, uwazi, uwajibikaji na kwa wakati.

Je, Sheria Inatekelezwa? Ushahidi wa Ukiukwaji Unaonyesha Nini?

Ingawa sheria imeweka wajibu huo, ushahidi uliokusanywa unaonyesha changamoto kadhaa katika utekelezaji wake.

Omar Nassor mkaazi wa Mahonda anasema wamekuwa wakielekezwa kujisajili upya kila mfumo mpya unapozinduliwa bila kupewa taarifa kuhusu maombi yao ya awali.

Anasema,Hakuna orodha inayopatikana kirahisi inayoonyesha nani ameidhinishwa, nani amekataliwa na kwa sababu zipi.

Kutokuwepo kwa taarifa hizi kunapunguza uwazi uliokusudiwa na sheria na kuwafanya waombaji waendelee kusubiri bila kujua hatima ya maombi yao.

Katika Shehia ya Mahonda pekee,Mwenyekiti wa vikundi vya wanawake  Semeni Bundala anasema kuna zaidi ya vikundi 24 vinavyosubiri mikopo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Kaskazini 'B', Jina Mohamed Haji, tangu mwaka 2022 ni vikundi 35 pekee vilivyopata mikopo katika wilaya hiyo.

Tofauti hii kati ya idadi ya wanaosubiri na wanaonufaika inaibua swali kuhusu kasi ya utekelezaji wa mpango huo.

Chanzo Kikuu cha Tatizo Ni Nini?

Uchambuzi wa taarifa kutoka kwa walengwa na taasisi unaonyesha kuwa tatizo halitokani na sababu moja pekee. Kwanza, maombi ni mengi kuliko fedha zinazoweza kutolewa kwa wakati mmoja.

 Mkurugenzi  wa Mitaji kutoka ZEEA  Kassim Haji  Mrisho   anasema , zaidi ya vikundi 100 bado havijapatiwa mikopo , kwa sababu mbali mbali ikiwemo,   wengi bado hawajaakizi vigezo vyao.

Anasema,  kuna sababu nyingi ambazo zinawafanya wananchi kutokupata mikopo hiyo kwa haraka ikiwemo  mabadiliko ya mifumo ya usajili, yameongeza urasimu kwa baadhi ya waombaji ambao hulazimika kuanza upya mchakato wa usajili.

Anasema, bado hakuna mfumo unaowapa wananchi taarifa za maendeleo ya maombi yao. Aidha anasema,  baadhi ya Halmashauri zimekuwa zikichelewa kuwasilisha asilimia 10 ya mapato yao kama sheria inavyotaka.

 kiwango kidogo cha urejeshaji wa mikopo kinapunguza uwezo wa mfuko kuwanufaisha waombaji wapya.

Kwa pamoja, sababu hizi zinaonekana kuchelewesha utekelezaji wa dhamira ya sheria.

Mamlaka Zinazowajibika

Kwa mujibu wa sheria, wajibu wa utekelezaji unagawanywa katika taasisi kadhaa.

Halmashauri zina jukumu la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani, kupokea na kuchambua maombi ya vikundi kabla ya kuyawasilisha ZEEA.

ZEEA ina jukumu la kufanya uchambuzi wa mwisho, kuidhinisha mikopo, kusimamia utoaji wa fedha pamoja na kufuatilia marejesho.

Aidha, viongozi wa ngazi za jamii wanapaswa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masharti ya mikopo na kusaidia kuhakikisha taarifa zinawafikia walengwa kwa wakati.

Endapo sehemu yoyote ya mfumo huu haitafanya kazi kwa ufanisi, mchakato mzima wa utoaji wa mikopo huathirika.

Mamlaka Zinajibu

Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Kaskazini 'B', Jina Mohamed Haji, anasema tangu mwaka 2022 vikundi 35 vimepatiwa mikopo, ambapo 27 ni vya wanawake, sita vya vijana na viwili vya watu wenye ulemavu.

Anasema hadi Machi 31 mwaka huu Halmashauri ilikuwa imewasilisha zaidi ya shilingi milioni 952 kwa ZEEA kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mitaji wa ZEEA, Kassim Haji Mrisho, anasema mamlaka hiyo imeshatoa zaidi ya shilingi bilioni tatu tangu mwaka 2022.

Kwa mujibu wake, tangu  mwaka 2022 kupitia mfumo wa 4-4-2,vikundi 20 vya vijana vimepatiwa mikopo yenye thamani ya shilingi  milioni 976, vikundi 55 vya wanawake vimepata zaidi ya shilingi bilioni 1.9 , huku vikundi 12 vya watu wenye ulemavu vikipata zaidi ya shilingi milioni  1.8.

Hata hivyo anakiri kuwa zaidi ya vikundi 100 bado havijapatiwa mikopo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokukamilisha baadhi ya vigezo na wingi wa maombi.

Pia anasema changamoto ya urejeshaji wa mikopo inaendelea kuathiri uwezo wa mfuko kuwafikia waombaji wapya.

Uchambuzi

Takwimu za serikali zinaonyesha mafanikio katika utoaji wa mikopo.

 Mchambuzi wa Maswala ya kisheria Zanzibar Almass Mohamed , anasema  simulizi za wananchi zinaonyesha kuwa bado kuna pengo kubwa kati ya takwimu hizo na hali halisi inayowakabili waombaji wengi.

 Anasema  ,Kama sheria ilikusudia kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa uwazi na kwa wakati, basi kuchelewa kwa maamuzi, kutokuwepo kwa mfumo wa kufuatilia maombi na ukosefu wa taarifa za mara kwa mara vinaonyesha kuwa utekelezaji bado una mapungufu.

Sheria haiishii katika kutenga fedha pekee; mafanikio yake hupimwa kwa uwezo wa mwananchi anayestahili kupata huduma bila urasimu usio wa lazima.

Anasema, Kwa maana hiyo, changamoto iliyopo inaonekana kuwa zaidi katika utekelezaji kuliko katika uwepo wa sheria.

 Aidha anasema ,Ili kuongeza uwajibikaji, taasisi zinazosimamia mpango huu zinapaswa kuchapisha mara kwa mara taarifa zinazoonyesha idadi ya maombi yaliyopokelewa, yaliyokubaliwa, yaliyokataliwa na sababu za maamuzi hayo.

“Hatua hiyo itapunguza malalamiko, kuongeza imani ya wananchi na kuimarisha uwazi katika matumizi ya fedha za umma” anasema.

Hitimisho

Mikopo ya asilimia 10 ni moja ya sera muhimu za kukuza uchumi jumuishi Zanzibar. Fedha zipo na sheria ipo.

Iwapo Serikali, Halmashauri na ZEEA zitaimarisha uwazi, kuharakisha uchambuzi wa maombi, kuboresha mifumo ya taarifa na kuhakikisha sheria inatekelezwa kwa usawa, mpango huu unaweza kufikia dhamira yake ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi.

       

No comments

Powered by Blogger.