Elimu Yaiwezesha Jamii Kutambua na Kuripoti Udhalilishaji Zanzibar
Na Salum Ameir
Mabadiliko chanya katika kuzuia na
kupambana na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto yameanza kuonekana
katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, huku jamii ikionyesha kuongezeka kwa
uelewa wa kutambua vitendo vya ukatili, kutoa taarifa na kuchukua hatua dhidi
ya vitendo hivyo.
Mabadiliko hayo yamebainika katika Mkutano wa Tathmini wa Mradi wa
“Tunaweza Pamoja”, unaotekelezwa na TAMWA Zanzibar kwa ufadhili wa UN Women
kupitia mradi wa Kukomesha Ukatili Dhidi ya Wanawake na Wasichana (EVAWG).
Mkutano huo uliofanyika Gamba, Wilaya ya Kaskazini A, uliwakutanisha
wadau 29 kutoka wilaya mbalimbali za Zanzibar, wakiwemo viongozi wa dini,
Masheha, Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals), wanachama wa GBV Network,
Mamalishe, Waratibu na waendesha bodaboda.Wadau hao walitathmini mafanikio
yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza pamoja na hatua zinazohitajika ili
kuendeleza mapambano dhidi ya udhalilishaji.
Watoto waanza kutambua udhalilishaji
Katika Shehia ya Fukuchani, Wilaya ya Kaskazini A, Sheha wa eneo hilo, Haji
Mohamed Juma, alisema elimu iliyotolewa imeanza kuwajengea watoto uwezo wa
kutambua vitendo vya udhalilishaji na kutoa taarifa.
Alisema, baadhi ya watoto wenye umri wa miaka sita, saba na minane tayari
wameanza kuelewa viashiria vya udhalilishaji na kuwa na ujasiri wa kutoa
taarifa wanapobaini vitendo visivyofaa.
“Watoto wawili walinifuata na kunipa taarifa kuhusu mtoto mwenzao kwamba
anafanya vitendo vibaya kwa mtoto mwenzake. Nilifuatilia na kubaini kuwa ni
kweli. Hii inaonyesha kuwa watoto wana uelewa wa kutambua udhalilishaji na
viashiria vyake,” alisema Haji.
Alisema, elimu hiyo inapaswa kuanza kutolewa tangu ngazi ya chekechea ili
kuwajengea watoto msingi wa kujilinda na kutambua mazingira yasiyo salama.
Wasichana mahotelini wajengewa uelewa
Mabadiliko mengine yameonekana miongoni mwa wasichana wanaofanya kazi
katika sekta ya hoteli.
Asia Fadhil Makame msaidizi wa
Sheria wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, alisema elimu aliyopata kupitia
TAMWA Zanzibar imemsaidia kuwafikia wasichana wanaofanya kazi katika hoteli na
kuwaelimisha kuhusu haki zao na namna ya kuripoti udhalilishaji.
Alisema, baadhi ya wasichana wamekuwa wakikabiliwa na vitisho vya kufutwa
kazi kwa sababu hawana mikataba, huku wengine wakishinikizwa kutoa rushwa ya
ngono ili waendelee na ajira.
“Tumeweza kutembelea mahotelini na kugundua wasichana wengi wanafanyiwa
vitisho vya kufutishwa kazi kwa sababu hawana mikataba. Wengine huombwa rushwa
ya ngono ili waendelee na kazi,” alisema Asia.
Aidha alisema kuwa , elimu hiyo imewasaidia baadhi ya wasichana kutambua
kuwa vitendo hivyo ni udhalilishaji, kujua namna ya kuripoti na kuchukua hatua
dhidi ya mazingira yasiyo salama kazini.
Wanawake wavuvi wapata mazingira
salama
Katika Shehia ya Kinduni, Wilaya ya Kaskazini B, mabadiliko yameonekana
pia miongoni mwa wanawake wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi.
Mratibu wa Shehia hiyo, Bahati Juma Chumu, alisema elimu
iliyotolewa imewasaidia wanawake hao kuchukua tahadhari zaidi wanapoingia
baharini.
Alisema kuwa ,wanawake hao
walishauriwa kutumia vipolo wanapoingia baharini ili kujisitiri na kupunguza
uwezekano wa miili yao kuonekana kutokana na nguo kulowa.
“Mara nyingi maeneo ya bandarini, kina mama wanapoingia baharini kufuata
samaki, nguo zao hulowa sana na kupelekea maumbile ya miili yao kuonekana,
hivyo ni rahisi kudhalilishwa aidha kwa maneno au vitendo,” alisema Bahati.
Alisema ushauri huo umepokelewa na wanawake hao na umechangia kuwafanya
wajisikie salama na huru zaidi wanapofanya shughuli zao.
Uelewa waongezeka kwa Mamalishe
Katika maeneo ya masoko, Yumna Nassor Ali, ambaye ni Mamalishe,
alisema elimu kuhusu udhalilishaji imeleta mabadiliko katika mtazamo wa jamii
kuhusu wanawake wanaofanya biashara ya chakula.
Alisema dhana kwamba Mamalishe wanahusishwa na biashara ya miili imekuwa
ikichangia unyanyapaa dhidi yao, lakini elimu imeanza kubadili mitazamo hiyo.
“Imezoeleka kwamba Mamalishe wanauza chakula na kuuza miili yao, lakini
sasa hivi maeneo mengi ya masokoni uelewa kuhusu masuala ya udhalilishaji
umekuwa mkubwa sana,” alisema Yumna.
Alisema, kuongezeka kwa uelewa kumewasaidia wanawake hao kujitambua,
kujiheshimu na kuelewa haki zao wanapokabiliwa na vitendo vya udhalilishaji.
Watoto Nungwi waanza kutoa taarifa
Huko Shehia ya Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Nachumu Rashid Haji
alisema watoto wameanza kuwa na uelewa wa kutambua mazingira ambayo yanaweza
kuwaweka katika hatari.
Alitoa mfano wa tukio ambapo baadhi ya watoto walipewa zawadi na mtu kutoka
jamii ya Kimasai, huku mmoja wao akiondoka naye.
Nachumu alisema watoto hao walitoa taarifa kuhusu tukio hilo, jambo
alilolieleza kuwa ni ishara ya kuongezeka kwa uelewa wao kuhusu usalama na
mazingira yasiyofaa.
“Watoto wa skuli walikuja kunifuata na kusema kwamba wamepewa zawadi na
Mmasai, lakini mmoja kati yao aliondoka na Mmasai huyo,” alisema Nachumu.
Alisema tukio hilo lilifuatiliwa na kutoa umuhimu wa jamii kuwa macho na
kuhakikisha watoto wanafundishwa namna ya kutambua mazingira hatarishi na kutoa
taarifa mapema.
Viongozi wa dini muhimu katika mapambano
Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa wadau, Lucy Tesha, Mtaalamu wa
Programu wa EVAWG kutoka UN Women, alisema viongozi wa dini wana nafasi muhimu
katika kuelimisha jamii kutokana na ushawishi wao katika masuala ya mienendo na
maadili.
“Ninaamini viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa katika jamii, hasa
katika masuala ya mienendo na tamaduni, na hivyo ni rahisi kuweza kushughulikia
masuala ya udhalilishaji katika jamii katika ngazi zote,” alisema Lucy.
Alisema ushirikishwaji wa viongozi wa dini pamoja na makundi mengine ya
jamii unaweza kusaidia kufikisha ujumbe wa kupinga udhalilishaji kwa watu wengi
zaidi.
TAMWA Zanzibar: Watoto kutoa taarifa
ni mafanikio
Kwa upande wake, Mohamed Khatib Mohammed, Afisa wa Ufuatiliaji na Tathmini TAMWA Zanzibar, alisema uwezo wa watoto wadogo kutambua na kuripoti vitendo vya ukatili ni miongoni mwa matokeo muhimu ya mradi.
“Matokeo haya ni muhimu sana kwetu, hasa kuona watoto wenye umri wa miaka
sita na saba sasa wanaweza kuelewa ukatili na udhalilishaji wa kijinsia na hata
kuripoti matukio hayo kwa walezi wao,” alisema Mohamed.
Alisema mafanikio hayo yanaonyesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa
jamii, hususan watoto, wazazi, viongozi wa jamii na makundi mengine yenye
ushawishi.
Hatua zaidi zahitajika
Mohammed alisema, Mkutano huo ulisisitiza umuhimu wa kuendeleza elimu na uhamasishaji
katika jamii ili kuhakikisha mabadiliko yaliyopatikana yanaendelea kuwa
endelevu.
Alisema kuwa , pamoja na hatua zilizopigwa, bado kuna umuhimu wa
kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa, kuongeza uelewa wa haki, kuwajengea uwezo
watoto na wanawake, pamoja na kuhakikisha waathirika wa udhalilishaji wanapata
msaada na ulinzi unaohitajika.
" Kwa ujumla, uzoefu kutoka Fukuchani, Kinduni, Nungwi na maeneo mengine
unaonyesha kuwa elimu ya jamii inaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuzuia
udhalilishaji " alisema .
Kuanzia watoto wanaojifunza kutoa taarifa, wanawake wanaojua haki zao
kazini, hadi viongozi wa jamii wanaochukua hatua, mabadiliko hayo yanaonyesha kuwa
mapambano dhidi ya udhalilishaji yanahitaji ushiriki wa jamii nzima na
kuendelea kwa elimu katika ngazi zote.
Mkutano huo uliofanyika Gamba, Wilaya ya Kaskazini A, uliwakutanisha
wadau 29 kutoka wilaya mbalimbali za Zanzibar, wakiwemo viongozi wa dini,
Masheha, Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals), wanachama wa GBV Network,
Mamalishe, Waratibu na waendesha bodaboda. ambapo Wadau hao walitathmini mafanikio
yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza pamoja na hatua zinazohitajika ili
kuendeleza mapambano dhidi ya udhalilishaji.
Post a Comment