Mikopo ya 4-4-2: Ufunguo wa kuinua makundi maalumu kiuchumi
Na Maryam Nassor
Asha, mkazi wa kijiji cha Mahonda, Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, alikuwa akitazama kwa huzuni kundi la wanawake wenzake wakizungumza kuhusu biashara zilizokuwa zikikua kwa kasi kupitia mikopo ya serikali.
Alikuwa na wazo zuri la kufungua biashara ya kusindika viungo vya asili, lakini kila aliposikia neno "mkopo wa serikali," aliamini fursa hiyo ni kwa ajili ya watu wenye fedha, wenye kufahamiana na viongozi, au waliosoma sana.
Hakuwahi kujua kuwa sheria na sera za serikali zilimtambua yeye kama mnufaika halali anayestahili fursa hiyo.
Miezi ilipita na biashara yake haikuanza. Wakati huohuo, vijana wengine kijijini waliendelea kukaa vibarazani wakisubiri ajira zisizopatikana, huku kundi la watu wenye ulemavu likiamini halina nafasi katika programu za maendeleo.
Baadaye, Asha alihudhuria kikao cha elimu ya umma kilichoeleza kuhusu mfumo wa mikopo ya asilimia 4-4-2. Hapo ndipo aligundua kuwa changamoto yake haikuwa ukosefu wa uwezo, bali uhaba wa taarifa na elimu ya haki za kisheria.
Hadithi ya Asha si ya kufikirika; ni picha halisi inayojirudia katika vijiji na shehia nyingi za Zanzibar, ambako wananchi wengi bado hawafahamu haki zao za kupata mikopo ya maendeleo inayotolewa kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa( Halmashauri).
Elimu ya kisheria ni zaidi ya kufahamu sheria
Almass Mohamed Mtaalamu wa utawala bora ,anaeleza kuwa elimu ya kisheria si kufahamu vifungu vya sheria pekee, bali ni kuwawezesha wananchi kutambua haki na wajibu wao, na namna ya kuzidai kupitia mifumo rasmi.
Anabainisha kuwa, Katika muktadha wa mikopo ya maendeleo, elimu hii huwasaidia wananchi kufahamu sifa za muombaji, masharti, namna ya kuunda vikundi, taratibu za maombi, wajibu wa halmashauri, na hatua za kuchukua endapo watanyimwa haki zao.
Bila elimu hii, sheria hata ziwe nzuri vipi, zitabaki kwenye maandishi bila kuwasaidia walengwa.
Mfumo wa "4-4-2" ni nini?
Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Kaskazini 'B', Jina Mohamed Haji,
anasema Mfumo wa 4-4-2 ni utaratibu wa kisheria unaozitaka Mamlaka za
Serikali za Mitaa kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya
kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba.
Mgawanyo huo uko hivi:
- Asilimia
4: Hutengwa kwa ajili ya wanawake.
- Asilimia
4: Hutengwa kwa ajili ya vijana.
- Asilimia 2: Hutengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Kwa mujibu wake, anasema Lengo kuu ni kuhakikisha makundi ambayo kwa muda mrefu yamekabiliwa na changamoto ya mitaji, yanawezeshwa kushiriki kikamilifu katika uzalishaji mali, kuongeza ajira, na kupunguza umaskini.
Mfumo huu unalenga kujenga usawa wa kiuchumi ili maendeleo yawafikie wananchi wa kawaida mijini na vijijini, badala ya kunufaisha watu wachache.
Kwa nini wananchi wengi hawajui haki zao?
Semeni Bungala Mwenyekiti wa kikundi cha wanawake shehia ya Mahonda, ansema Licha ya kuwepo kwa mfumo huu, wananchi wengi—hasa wanawake wa vijijini, vijana, na watu wenye ulemavu—bado hawajui kuwa wana haki ya kuomba mikopo hii.
Sababu kuu zinazochangia hali hii ni pamoja na:
- Uchache
wa kampeni za elimu kwa umma.
- Matumizi
ya lugha ngumu na ya kisheria katika nyaraka za serikali.
- Taarifa
kutofika maeneo ya pembezoni.
- Uelewa
mdogo wa sheria zinazosimamia mikopo hiyo.
- Dhana potofu kuwa mikopo hiyo ni kwa ajili ya watu wenye ushawishi wa kisiasa.
Kutokana na changamoto hizo, fedha zinazotengwa wakati mwingine hazifiki kwa jamii zilizokusudiwa, au vikundi vinashindwa kuomba kwa kukosa taarifa sahihi.
Elimu ya kisheria kuhusu mikopo inaleta uwajibikaji
Saleh Muharam, kijana na mkazi wa Mahonda, anabainisha kuwa wananchi wanapofahamu haki zao kuhusu mikopo hiyo, huanza kuwawajibisha viongozi wao.
Kwa mfano, wanakuwa na uwezo wa kuhoji:
- Je,
halmashauri imetenga fedha za 4-4-2 mwaka huu?
- Ni
vikundi vingapi vimefaidika na vigezo gani vimetumika?
- Kwa
nini baadhi ya waombaji walikataliwa?
- Je, fedha zinazorejeshwa zinasambazwa tena kutoa mikopo mingine?
Maswali haya huongeza uwazi, yanapunguza upendeleo, na kuimarisha matumizi sahihi ya fedha za umma.
Mfumo wa 4-4-2 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
Serikali ya Tanzania imeandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi jumuishi unaotegemea uzalishaji, teknolojia, ubunifu, na ushiriki wa wananchi wote.
Dira hii inasisitiza kukuza ajira kwa vijana, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika maendeleo, na kupunguza umaskini.
Kwa mantiki hiyo, mfumo wa mikopo ya 4-4-2 ni nyenzo muhimu ya kufikia malengo hayo.
Ikiwa wanawake watanzisha biashara, vijana wakapata mitaji ya ubunifu, na watu wenye ulemavu wakapewa nafasi sawa, taifa litakuwa na msingi imara wa uchumi shindani na jumuishi.
Makundi lengwa yanahitaji mbinu mahususi
- Wanawake wa vijijini: Wanakabiliwa na vikwazo vya umiliki wa mali na mitaji.
Semeni Bungala , anasema Elimu ya kisheria kuhusu mikopo itawasaidia kuelewa kuwa wana haki ya kuomba mikopo hii bila ubaguzi wa kijamii au kielimu, na kuwapa ujasiri wa kushiriki katika mikutano ya vijiji au shehia kufuatilia mapato ya maendeleo.
- Vijana:
Idadi kubwa ya vijana inahangaika kutafuta ajira badala ya kuwa waajiri
kupitia mitaji hii.
Mikopo ya 4-4-2 inaweza kuwasaidia kuanzisha biashara za kilimo cha kisasa, uvuvi, utalii, na ubunifu wa kidijitali.
- Watu wenye ulemavu: Abdalla Alawi, mtu mwenye ulemavu wa uziwi, anasema kuwa kwa miaka mingi kundi hili limekumbana na vikwazo vya mitaji.
Anasisitiza kuwa utengaji wa asilimia mbili ni hatua kubwa, lakini bila elimu hawataomba kwa sababu hawajui kama kuna fungu lao.
"Elimu hii inapaswa kuzingatia lugha rahisi, maandishi yanayosomeka, na mbinu zinazofikia watu wenye mahitaji mbalimbali," anasema Abdallah.
Nani anapaswa kutoa elimu hii?
Mkurugenzi wa Mitaji kutoka ZEEA, Kassim Miraji Haji anasema Jukumu la kutoa elimu ya haki za kisheria kuhusu mikopo hiyo si la serikali pekee. Linahitaji ushirikiano wa halmashauri, wizara husika, mashirika ya kiraia, vyombo vya habari, viongozi wa shehia, taasisi za kifedha, na viongozi wa dini au jamii.
Aidha anasema, Vyombo vya habari vina nafasi ya pekee ya kutafsiri lugha ya kisheria kuwa rahisi kupitia makala, vipindi vya redio, runinga, na majukwaa ya kidijitali.
Hitimisho
Sheria pekee haziwezi kuleta maendeleo ikiwa wananchi hawazifahamu.
Fedha zinaweza kutengwa na sera zinaweza kuandikwa, lakini bila elimu ya haki za kisheria, wananchi wengi watabaki watazamaji huku fursa zikiwapita.
Mfumo wa 4-4-2 una nguvu ya kubadili maisha ya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, lakini mafanikio yake yanategemea uelewa wa walengwa.
Ikiwa Tanzania inataka kufikia malengo ya Dira ya 2050, uwekezaji katika kuelimisha umma kuhusu haki zao za kisheria unapaswa kupewa uzito sawa na uwekezaji wa fedha za mikopo yenyewe.
Wananchi wakijua haki zao, watazidai; wakizidai,
watawajibisha viongozi; na uwajibikaji unapokuwepo, fedha huwafikia walengwa na
kuleta maendeleo ya kweli na endelevu.
Post a Comment