Watimiza masharti, lakini bado wanasubiri

Na Maryam Nassor
Zaidi ya mwaka mmoja umepita tangu Khadija Abdalla na wenzake wa kikundi
cha wanawake kutoka Shehia ya Mahonda, Wilaya ya Kaskazini 'B', Unguja, waanze
kufuatilia mkopo wa asilimia 10 unaotolewa kupitia mfumo wa 4-4-2.
Walisajili kikundi, wakafungua
akaunti ya benki na kukamilisha masharti yote yaliyowekwa wakiamini wangepata
mtaji wa kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali.
Badala yake, wameendelea kusubiri bila kujua lini watanufaika na mpango
huo.
Kila wanapofuatilia maombi yao, hupewa jibu lilelile:
"Jisajilini tena kwenye mfumo mpya wa kidijitali."
Kwa Khadija, majibu hayo yamekuwa yakijirudia kwa miezi mingi bila kupewa
taarifa zinazoonyesha hatua iliyofikiwa au sababu ya kuchelewa kwa mkopo.
"Tuna hamu ya kupata mkopo huu ili kuendeleza shughuli zetu za
ujasiriamali, Lakini mpaka leo bado hatujafanikiwa. Kila tunapoulizia
tunaambiwa tujisajili tena kwenye mfumo wa kidijitali badala ya ule wa awali wa
karatasi," anasema.
Simulizi yake si ya kipekee. Inaakisi hali inayowakabili wanawake, vijana
na watu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar ambao, licha ya
kutimiza masharti yote yaliyowekwa, bado hawajapatiwa mikopo wala maelezo
yanayoeleweka kuhusu maombi yao.
Maswali yanayohitaji majibu
Malalamiko ya wananchi yanaibua maswali muhimu. Mikopo hiyo inatolewa kwa
utaratibu gani? Ni nani anayestahili kunufaika? Kwa nini baadhi ya vikundi
hupata mikopo mapema huku vingine vikisubiri kwa muda mrefu bila maelezo ya
wazi?
Maswali hayo yanaonyesha umuhimu wa kuangalia kwa karibu utekelezaji wa
mpango huu na kama kweli unatimiza lengo lake la kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Mikopo ya asilimia 10 ni mpango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
unaolenga kuwawezesha wananchi kupitia sehemu ya mapato ya ndani ya
halmashauri. Kupitia mfumo wa 4-4-2, asilimia nne ya fedha hutengwa kwa
wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.
Lengo lake ni kuongeza mitaji kwa makundi hayo, kukuza ajira, kupunguza
umaskini na kuimarisha shughuli za uzalishaji mali.
Mpango huu umejengwa juu ya Sheria ya Serikali za Mitaa Na. 9 ya mwaka
2023 na Sheria ya Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) Na. 2
ya mwaka 2022, ambazo zinaelekeza halmashauri na ZEEA kusimamia utekelezaji wa
programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Hata hivyo, pamoja na msingi huo wa kisheria, simulizi za walengwa
zinaonyesha bado kuna pengo kati ya matarajio ya wananchi na utekelezaji wa mpango.
Kanuni za miongozo ya utoaji wa mikopo .
Kwa mujibu wa miongozo ya utekelezaji wa mikopo ya mfumo wa 4-4-2,
mgawanyo wa wanufaika unazingatia uwiano wa asilimia 40 kwa wanawake,
asilimia 40 kwa vijana na asilimia 20 kwa watu wenye ulemavu, kwa lengo la
kuhakikisha makundi hayo yanapata fursa sawa ya kupata mtaji wa kuanzisha au
kukuza shughuli za kiuchumi.
Mwongozo huo pia unaeleza kuwa mwombaji anatakiwa awe mzawa au mkazi
halali wa Zanzibar, awe ndani ya kundi husika, awe na shughuli ya kiuchumi au
mpango wa biashara unaotekelezeka, pamoja na kuwa tayari kurejesha mkopo kwa
mujibu wa masharti yaliyowekwa.
Hata hivyo, simulizi za baadhi ya waombaji zinaonyesha kuwa, licha ya
kukamilisha masharti hayo, bado wameendelea kusubiri kwa muda mrefu bila kupata
mrejesho wa kuridhisha kuhusu maombi yao.
Masharti yanayowakwamisha baadhi ya walengwa
Kwa watu wenye ulemavu, kuruhusiwa kuomba mikopo hata mtu mmoja mmoja kulionekana kuongeza fursa za
kunufaika. Hata hivyo, baadhi yao wanaona bado kuna masharti yanayowazuia.
Kassimu Mohamed, mkazi wa Mahonda mwenye ulemavu wa viungo, anasema
anatamani kupata mtaji wa kuanzisha biashara lakini anakwama kutokana na sharti
la kuwa tayari ana biashara kabla ya kupata mkopo.
"Nitaanzaje biashara wakati sina mtaji wala ajira? Kama kweli lengo
ni kutuwezesha kiuchumi, basi tupewe mtaji pamoja na mafunzo ili nasi tuweze
kujenga maisha yetu na familia zetu," anasema.
Kauli yake inaibua mjadala kuhusu iwapo masharti yaliyopo yanawafikia
walengwa waliokusudiwa. Kwa baadhi yao, uwezeshaji wa kweli unapaswa kuanza kwa
kuwasaidia wale wasio na mtaji wa kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Vijana nao wanasubiri
Changamoto zinazowakabili wanawake na watu wenye ulemavu zinaonekana pia
kwa vijana.
Omar Nassor anasema kikundi chao kilikamilisha taratibu zote za maombi,
lakini hadi sasa hakijapatiwa mkopo wala maelezo yanayowapa uhakika wa lini
watanufaika.
Anasema katika mazingira ambayo Serikali haiwezi kuwaajiri wananchi wote,
mikopo ya asilimia 10 inapaswa kuwa fursa ya kuwasaidia vijana kujiajiri badala
ya kuendelea kusubiri ajira rasmi.
"Tuko tayari kufanya biashara na kujikwamua kiuchumi, lakini kila
tunapofuatilia tunaambiwa tuendelee kusubiri kwa sababu mifumo haijakaa sawa.
Hali hii inatukatisha tamaa kwa sababu hatuna uhakika wa lini tutapata
mkopo," anasema.
Kauli yake inaonyesha kuwa changamoto kubwa si ukosefu wa nia ya kufanya
kazi, bali kutokuwa na uhakika wa lini ahadi ya uwezeshaji itageuka kuwa fursa
halisi.
Majibu ya mamlaka: Utekelezaji unaendelea
Malalamiko ya wananchi yanapowasilishwa kwa mamlaka, picha inayojitokeza
ni kwamba mpango wa mikopo unaendelea kutekelezwa na tayari umewanufaisha
baadhi ya walengwa.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Kaskazini 'B', Jina Mohamed Haji,
anasema tangu mwaka 2022 hadi sasa 2026 vikundi 35 vimepatiwa mikopo. Kati ya
hivyo, vikundi 27 ni vya wanawake, sita vya vijana na viwili vya watu wenye
ulemavu.
Anasema pia Halmashauri imewasilisha zaidi ya shilingi milioni 952 kwa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
Zanzibar (ZEEA) tokea mwaka 2024 hadi kufikia Machi 31 mwaka huu kwa ajili ya
kutekeleza mpango huo.
Hata hivyo, anakiri kuwa baadhi ya changamoto zimejitokeza, hususan
katika mifumo ya benki inayotumika kusimamia marejesho ya mikopo. Mara nyingi
huwa haiko hewani Kwa mujibu wake, hali
hiyo imechangia baadhi ya malalamiko kutoka kwa wanufaika na waombaji.
Kutokana na changamoto hizo, anashauri kuendelea kuboresha mfumo wa
usajili na utoaji wa huduma ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo na kuongeza
ufanisi wa program hiyo.
ZEEA yatoa taswira ya mafanikio
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mitaji kutoka ZEEA Kassim Miraji Haji, anasema mamlaka hiyo ilianzishwa kuratibu
programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia mafunzo na mikopo.
Anasema hadi sasa ZEEA imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi
bilioni tatu kupitia programu ya 4-4-2. Huku ikifanikiwa kukusanya bilioni nne
tokea mwaka 2022 ilipoanzishwa hadi sasa.
Kwa mujibu wake, anasema tangu
mwaka 2022 kupitia mfumo wa 4-4-2,vikundi 20 vya vijana vimepatiwa
mikopo yenye thamani ya shilingi milioni
976, vikundi 55 vya wanawake vimepata zaidi ya shilingi bilioni 1.9 , huku
vikundi 12 vya watu wenye ulemavu vikipata zaidi ya shilingi milioni 1.8.
Hata hivyo, tathimini ya mwaka
2024 ilibaini zaidi ya wananchi elfu
3796 wanufaika na program hiyo na
wamefanikiwa kuzalisha ajira. Wanawake
wakiwa 3262 , vijana wakiwa
534 huku watu wenye ulemavu wakiwa 263.
Anasema , zaidi ya vikundi 100
bado havijapatiwa mikopo hiyo kwa sababu mbali mbali ikiwemo, wengi bado hawajaakizi vigezo vyao kwa
kutokuwa na biashara.
Aidha anasema changamoto kubwa inayoiikabili ZEEA
ni urejeshaji wa mikopo. Huku akiitaja halmashauri inayofanya vibaya zaidi katika halmashauri zote za Zanzibar ni Mjini
Unguja kutokana na ucheleweshaji wa michango ya asilimia 10 ya mapato yake.
Anasema takwimu hizo zinaonyesha kuwa mpango huo unaendelea kuwafikia
walengwa na una uwezo mkubwa wa kubadili maisha ya wananchi endapo utasimamiwa
kwa ufanisi na kuwafikia wahitaji kwa wakati.
Tatizo haliko kwenye sheria
Kwa mujibu wa mtaalamu wa sheria kutoka Zanzibar, Almass Mohamed, anasema
changamoto kubwa haipo katika uwepo wa sheria, bali katika utekelezaji wake.
Anasema sheria zilizopo zimeweka msingi mzuri wa kuwawezesha wanawake,
vijana na watu wenye ulemavu, lakini mafanikio ya programu yatategemea uwazi,
usawa na uwajibikaji wa taasisi zinazozisimamia.
Kwa mtazamo wake, wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi kuhusu
masharti, vigezo vya kupata mikopo na hatua za maombi yao ili kuondoa
sintofahamu inayojitokeza.
"Serikali, halmashauri, ZEEA na wadau wote wana wajibu wa
kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inawafikia walengwa na kutimiza lengo la
kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujenga uchumi imara na
kuchangia maendeleo ya Zanzibar," anasema.
Uwazi utaongeza imani ya wananchi
Simulizi za Khadija Abdalla, Kassimu Mohamed na Omar Nassor zinaonyesha
matarajio makubwa ambayo wananchi wameyaweka kwenye mikopo ya asilimia 10.
Kwao, mpango huu ni fursa ya kujenga maisha bora kupitia ujasiriamali na
shughuli nyingine za uzalishaji mali.
Kwa upande mwingine, takwimu zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya
Kaskazini 'B' pamoja na ZEEA zinaonyesha kuwa tayari makundi kadhaa yamenufaika
na mpango huo. Hata hivyo, malalamiko ya baadhi ya waombaji yanaonyesha kuwa
bado kuna haja ya kuimarisha utoaji wa taarifa, kurahisisha mifumo ya maombi na
kuhakikisha waombaji wanapata mrejesho wa wakati kuhusu hatua za maombi yao.
Kuboresha maeneo hayo kutasaidia kujenga imani ya wananchi kwa programu
na kupunguza sintofahamu kuhusu namna mikopo inavyotolewa.
Uwajibikaji ndiyo kipimo cha mafanikio
Mikopo ya asilimia 10 ni fursa muhimu ya kuwawezesha wanawake, vijana na
watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa Zanzibar.
Uwepo wa sheria, taasisi na fedha ni msingi muhimu, lakini mafanikio yake
yatapimwa kwa uwezo wa mfumo kuwafikia walengwa kwa haki, uwazi na kwa wakati.
Wananchi wanahitaji kuona kuwa taratibu zilizowekwa zinafanya kazi kwa
ufanisi, maombi yao yanapatiwa majibu kwa wakati na changamoto zinazojitokeza
zinatatuliwa kwa uwazi. Hivyo ndivyo imani kwa programu itaongezeka na lengo la
kupunguza umaskini kupitia uwezeshaji wa kiuchumi litafikiwa.
Kwa kuendelea kuboresha mawasiliano, kurahisisha mifumo ya maombi na
kuimarisha uwajibikaji wa taasisi zinazosimamia mpango huu, mikopo ya asilimia
10 inaweza kuendelea kuwa chachu ya maendeleo jumuishi na kuwasaidia wananchi
wengi zaidi kujenga uchumi imara na maisha yenye tija Zanzibar.
Post a Comment