Mikopo ya asilimia 10 yawanufaisha wachache

 

Na Maryam Nassor

Kwa zaidi ya miaka miwili, Semeni Bundala ameendelea kufika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini 'B' akiwa na matumaini ya kupata mkopo wa asilimia 10 uliotengwa kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi.

Kila safari anarudi na majibu yale yale.

Badala ya kupata mkopo, anaelekezwa kujisajili tena katika mifumo mipya ya maombi, licha ya kwamba kikundi chake kilishawahi kujaza fomu za karatasi na kutimiza masharti yote yaliyowekwa.

"Tumekuwa tukifuatilia mikopo hii kwa muda mrefu bila mafanikio. Kila tunapofika Halmashauri tunaelekezwa kujisajili kwenye mifumo mbalimbali. Hadi leo hatujui tatizo ni nini," anasema.

Semeni si peke yake.

Malalamiko kama yake yanaendelea kusikika kutoka kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Kaskazini 'B', hali inayoibua maswali kuhusu uwazi, usawa na uwajibikaji katika utekelezaji wa mfumo wa mikopo ya asilimia 10 unaotekelezwa kwa utaratibu wa 4-4-2.

Sheria ipo, lakini walengwa bado wanalalamika

Kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria Na. 9 ya Mwaka 2023, Serikali za Mitaa zina wajibu wa kuweka mazingira ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mipango mbalimbali ya maendeleo.

Aidha, Kifungu cha 9 cha Sheria Na. 2 ya Mwaka 2022 kinaipa Mamlaka ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) jukumu la kusimamia na kuratibu programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayogawanywa kwa mfumo wa asilimia 4 kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.

Sheria hizo zilitungwa kuongeza fursa za kiuchumi, kukuza ajira na kuinua kipato cha wananchi.

Kwa mujibu wa miongozo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kila halmashauri inapaswa kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo hiyo.

Lakini uchunguzi huu unaonesha kuwa utekelezaji wake bado unaibua maswali.

Walengwa wanasema hawafikii fursa

Semeni anasema kikundi chake kilitimiza masharti yote, ikiwemo kuwa na wanachama saba, kusajili kikundi na kuwa na vitambulisho vinavyotakiwa.

Hata hivyo, hadi sasa hakijapata mkopo.

Anasema katika Shehia ya Mahonda pekee kuna zaidi ya vikundi 24 vilivyosajiliwa, lakini bado havijapata mikopo.

Kwa upande wake, Fatma Said, mkazi wa Mahonda mwenye ulemavu wa viungo, anasema fedha zinazotengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu haziwafikii walengwa kama ilivyokusudiwa.

Kwa mujibu wake, utekelezaji wa mgawanyo wa 4-4-2 hauonekani kufanyika kikamilifu, jambo linalowafanya watu wenye ulemavu kushindwa kupata asilimia mbili iliyotengwa kwa mujibu wa mfumo huo.

"Kutokupata mikopo hii kunaturudisha nyuma kiuchumi. Wengi wetu hatuna ajira na tulitegemea mikopo hii kuanzisha au kukuza shughuli za kujiongezea kipato," anasema.

Changamoto kama hiyo pia inamkumba Khatib Mohamed, Katibu wa Kikundi cha Vijana.

Anasema amekuwa akifuatilia mkopo huo kwa muda mrefu bila mafanikio, huku akielekezwa mara kwa mara kujisajili katika mifumo mbalimbali.

"Biashara yangu ya ufugaji wa kuku ilikufa kutokana na kukosa mtaji. Nilitegemea mkopo huu kuikuza biashara yangu, lakini kutokana na kuchelewa kuupata nimeendelea kuwa katika hali ngumu ya kiuchumi," anasema.

Kauli za wananchi hawa zinaibua maswali kuhusu uwazi wa mfumo wa usajili, ufanisi wa mchakato wa utoaji wa mikopo na kiwango cha uwajibikaji wa taasisi zinazosimamia mpango huo.

Halmashauri yajibu tuhuma

Akijibu malalamiko hayo, Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Kaskazini 'B', Jina Mohamed Haji, anasema kuanzia mwaka 2022 hadi sasa vikundi 35 tayari vimepata mikopo.

Kati ya hivyo, vikundi 27 ni vya wanawake, sita vya vijana na viwili vya watu wenye ulemavu.

Anasema Halmashauri imewasilisha ZEEA zaidi ya shilingi milioni 952 kufikia Machi 31 mwaka huu.

Anaongeza kuwa  , kwa mwaka huu 2026 tangu kuanza kwa mfumo wa kidijitali, vikundi sita pekee ndiyo vimejitokeza  na  tayari vimesajiliwa  vinasubiri kupatiwa mikopo baada ya maombi yao kuwasilishwa ZEEA kwa ajili ya uchambuzi.

Pia anakiri kuwa changamoto za mifumo ya benki  ikiwemo mifumo kutokuwa hewani,  zimechangia malalamiko ya baadhi ya wanufaika kuhusu marejesho ya mikopo na kuiomba ZEEA kuboresha mfumo wa usajili ili kuondoa changamoto zinazowakabili waombaji.

ZEEA yaeleza mafanikio

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mitaji kutoka ZEEA ,  Kassim Haji Mrisho, anasema mamlaka hiyo ilianzishwa kwa Sheria Na. 2 ya Mwaka 2022 kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mafunzo na mikopo.

Anasema hadi sasa taasisi hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni   tatu kati  ya bilioni nne  zilizowasilishwa ZEEA tokea mwaka 2022 hadi sasa kupitia programu ya Makundi maalum ya wajasiriamali  yaani 4-4-2.

Kwa mujibu wake, tangu mwezi  May, mwaka 2022 kupitia mfumo wa 4-4-2,vikundi 20 vya vijana vimepatiwa mikopo yenye thamani ya shilingi  milioni 976, vikundi 55 vya wanawake vimepata zaidi ya shilingi bilioni 1.9 , huku vikundi 12 vya watu wenye ulemavu vikipata zaidi ya shilingi milioni  1.8.

Aidha anasema , zaidi ya vikundi 100 bado havijapatiwa mikopo hiyo kwa sababu mbali mbali ikiwemo,   wengi bado hawajaakizi vigezo vyao.

Anasema changamoto kubwa inayoiikabili ZEEA ni urejeshaji wa mikopo. Huku akiitaja halmashauri inayofanya vibaya katika halmashauri zote za Zanzibar ni Mjini Unguja kutokana na ucheleweshaji wa michango ya asilimia 10 ya mapato yake.

Hata hivyo, tathimini ya mwaka 2024 ilibaini zaidi ya wananchi  elfu 3796 wanufaika na program hiyo  na wamefanikiwa kuzalisha ajira. Wanawake  wakiwa 3262  , vijana wakiwa 534  huku watu wenye ulemavu wakiwa 263.

Aidha, mamlaka hiyo imeondoa sharti lililowataka watu wenye ulemavu kukopa kupitia vikundi pekee na sasa wanaweza pia kukopa mmoja mmoja ili kuongeza fursa za kunufaika.

 Aidha amesema kuwa,  walengwa wakishindwa kurejesha mikopo wanachokifanya ni kufungia leseni na sehemu zao za biashara. Akibainisha kuwa kwa vile wanashirikiana na halmashauri ikitokea kikundi kimeshindwa kurejesha mikopo hiyo, wao ndiyo wanaowachukulia hatua.

Tatizo liko kwenye utekelezaji?

Mtaalamu wa masuala ya sheria Zanzibar, Almass Mohamed, anasema changamoto kubwa si ukosefu wa sheria bali ni utekelezaji wake.

Anaeleza kuwa Sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imeweka wajibu wa kuhakikisha fedha zinazotengwa zinawafikia walengwa kwa misingi ya usawa, uwazi na uwajibikaji.

"Endapo wananchi wanaendelea kulalamikia kutopata mikopo licha ya kutimiza masharti yaliyowekwa, ni dalili kwamba kuna mapungufu katika utekelezaji wa sheria, usimamizi wa mifumo au utoaji wa taarifa kwa umma."

Anasisitiza kuwa mfumo wa mikopo ya asilimia 10 unaotekelezwa kwa utaratibu wa 4-4-2 unapaswa kuzingatia haki, uwazi na usawa ili makundi yaliyokusudiwa yaweze kunufaika.

Pengo kati ya takwimu na uhalisia

Uchunguzi huu unaonesha kuwa pamoja na kuwepo kwa sheria, sera na fedha za uwezeshaji wananchi kiuchumi, bado kuna wananchi wanaodai kutonufaika na mfumo huo licha ya kutimiza masharti yaliyowekwa.

Wakati Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini 'B' na ZEEA zikieleza mafanikio ya utoaji wa mikopo, ushahidi kutoka kwa baadhi ya walengwa unaonesha kuwepo kwa pengo kati ya takwimu zinazotolewa na taasisi hizo na hali wanayoikabili wananchi wanaosubiri kunufaika.

Bila kuimarisha uwazi katika mchakato wa utoaji wa mikopo, kuboresha mifumo ya usajili na kuongeza uwajibikaji wa taasisi husika, lengo la mfumo wa asilimia 10 wa kuwawezesha wananchi kiuchumi linaweza kuendelea kubaki kwenye maandishi ya sheria kuliko kuonekana katika maisha ya wananchi.

 

 

No comments

Powered by Blogger.