FATMA DAWA PILI: MWALIMU WA KIKE ALIYEFANIKIWA KUFAULISHA WANAFUNZI KWA ASILIMIA 100 MWAKA 2025

Na Maryam Nassor

Asubuhi inapowadia katika Skuli ya Sekondari Fukuchani, wanafunzi huanza kuingia mmoja baada ya mwingine wakiwa wamevalia sare zao kwa nidhamu. Walimu nao huelekea madarasani kwa wakati, huku mazingira ya shule yakionyesha utulivu na mpangilio unaovutia.

Katikati ya shughuli hizo yupo mwanamke mwenye tabasamu la utulivu lakini mwenye msimamo usioyumba kuhusu nidhamu, uwajibikaji na ubora wa elimu. Huyo ni Fatma Dawa Pili, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Fukuchani.

Kwa wengi, mafanikio ya shule hupimwa kwa matokeo ya mitihani  kwa Fatma, mafanikio huanzia katika kujenga mazingira yanayomwezesha mwanafunzi kuamini kuwa anaweza kufaulu, mwalimu kufanya kazi kwa moyo mmoja, na mzazi kushiriki kikamilifu katika safari ya elimu ya mtoto wake.

Katika kipindi kifupi tangu alipohamishiwa kuongoza Skuli ya Sekondari Fukuchani mwaka 2025, ameonyesha kwamba uongozi bora unaweza kubadili si tu matokeo ya kitaaluma, bali pia utamaduni mzima wa taasisi.

Safari ilipoanzia Potoa

Fatma Dawa Pili alizaliwa mwaka 1973 katika kijiji cha Potoa, Unguja. Tangu akiwa mtoto alijifunza thamani ya elimu, nidhamu na kufanya kazi kwa bidii. Alikulia katika mazingira yaliyomfundisha kwamba mafanikio hayatokani na bahati bali na kujituma na uvumilivu.

Baada ya kumaliza masomo yake, alichagua taaluma ya ualimu akiwa na dhamira ya kusaidia watoto kupata elimu bora na kuwaandaa kuwa raia wenye maarifa na maadili.

Mwaka 2000 alianza rasmi kazi ya ualimu katika Skuli ya Sekondari Mkwajuni. Huo ulikuwa mwanzo wa safari ambayo leo imefikia zaidi ya robo karne ya kulitumikia taifa kupitia sekta ya elimu.

Akiwa mwalimu mchanga, alijijengea sifa ya kufanya kazi kwa bidii, kuwajali wanafunzi na kushirikiana vizuri na walimu wenzake. Alitambua kuwa ili aweze kutoa mchango mkubwa zaidi, alihitaji kuendelea kujifunza.

Ndiyo maana mwaka 2003 alipata Stashahada ya Ualimu katika Chuo cha Ualimu Nkrumah, hatua iliyompa maarifa mapya ya kitaaluma na kumjengea uwezo wa kuchukua majukumu makubwa zaidi ya kiuongozi.

Baadaye alihamishiwa Skuli ya Sekondari Chaani, ambako aliteuliwa kuwa Mwalimu Mkuu Msaidizi. Nafasi hiyo ilimpa fursa ya kujifunza kwa vitendo namna ya kusimamia shule, kuongoza walimu na kuhakikisha ubora wa taaluma unaimarika.

Kutokana na uwezo wake, mwaka 2017 alipandishwa kuwa Mwalimu Mkuu. Huo ulikuwa uthibitisho kwamba uongozi wake uliaminiwa na kuthaminiwa.

Mwaka 2025 alipewa jukumu jipya la kuongoza Skuli ya Sekondari Fukuchani, akiwa na dhamana ya kuendeleza maendeleo ya shule hiyo.

Uongozi unaojenga matokeo

Fatma anaamini kuwa mafanikio ya shule hayatokani na juhudi za mtu mmoja, bali ushirikiano wa walimu, wanafunzi, wazazi na jamii.

Anasema kiongozi mzuri ni yule anayesikiliza, anashirikisha wengine katika maamuzi na anayetoa mfano kupitia matendo yake.

Chini ya uongozi wake, Skuli ya Sekondari Fukuchani yenye wanafunzi 419 na walimu 20 imeendelea kupiga hatua kubwa katika taaluma.

Matokeo ya Kidato cha Pili yaliongezeka kutoka asilimia 71 mwaka 2024 hadi asilimia 100 mwaka 2025. Vivyo hivyo, ufaulu wa Kidato cha Nne uliongezeka kutoka asilimia 93.33 hadi asilimia 100 katika kipindi hicho.

Kwa wengi, hizi ni takwimu tu. Lakini kwa Fatma, kila asilimia inawakilisha mwanafunzi aliyefanikiwa kutimiza ndoto yake na familia iliyopata matumaini mapya.

Anasema mafanikio hayo yametokana na kufuatilia kwa karibu maendeleo ya wanafunzi, kufanya tathmini za mara kwa mara, kuimarisha ushauri nasaha na kuhakikisha walimu wanapata mazingira mazuri ya kufundisha.

Kiongozi anayewaamini walimu

Walimu wanaofanya kazi chini ya Fatma wanamwelezea kama kiongozi anayejenga timu badala ya kuamuru.

Mwalimu Khamis Mohammed Nasoro anasema Fatma huwapa walimu nafasi ya kutoa mawazo yao na kuwashirikisha katika maamuzi muhimu ya shule.

"Kiongozi anapotusikiliza, tunahisi sisi ni sehemu ya mafanikio ya shule, Hilo limetuongezea ari ya kazi na kujituma zaidi," anasema.

Kwa upande wake, Mwalimu Jina Khamis Haji anasema Fatma ni kiongozi anayesisitiza nidhamu na uwajibikaji, lakini pia huwasaidia walimu kutatua changamoto wanazokutana nazo.

Anaongeza kuwa Fatma huamini kila mwalimu ana mchango muhimu katika kuinua kiwango cha elimu, jambo linalojenga mshikamano na mazingira mazuri ya kazi.

Mlezi wa wanafunzi

Mbali na kuwa msimamizi wa taaluma, Fatma pia ni mlezi wa wanafunzi.

Mwanafunzi Nairat Ame Ali anasema Mwalimu Mkuu huyo huwahimiza kuamini uwezo wao, kusoma kwa bidii na kutokata tamaa hata wanapokutana na changamoto.

"Anatusikiliza, anatupa ushauri na hutufanya tuamini kwamba tunaweza kufikia ndoto zetu," anasema.

Mtazamo huo umechangia kujenga ujasiri kwa wanafunzi na kuongeza ari ya kujifunza.

Kuimarisha ushiriki wa wazazi

Fatma anaamini elimu bora haiwezi kupatikana bila ushirikiano wa wazazi.

Chini ya uongozi wake, mawasiliano kati ya shule na wazazi yameimarishwa kupitia mikutano ya mara kwa mara na majadiliano kuhusu maendeleo ya wanafunzi.

Mzazi Musa Bakar Ali anasema tangu  mwalim Fatma afike shuleni hapo, wazazi wameanza kuwa na imani kubwa zaidi na shule.

"Tunaona mabadiliko katika nidhamu, ufaulu na namna shule inavyoendeshwa. Hilo limetufanya tushirikiane zaidi na walimu," anasema.

Siri ya mafanikio

Fatma anasema,  anaamini mafanikio hutokana na mambo matatu makubwa: nidhamu, uwajibikaji na ushirikiano.

Kwa mtazamo wake, mwanafunzi mwenye nidhamu ana nafasi kubwa ya kufaulu, mwalimu anayewajibika huongeza ubora wa elimu, na mzazi anayeshiriki huongeza uwezekano wa mtoto kufanikiwa.

Anasisitiza kuwa, viongozi wa elimu wanapaswa kuwa mfano wa maadili kwa walimu na wanafunzi badala ya kutegemea kutoa maagizo pekee.

Changamoto za uongozi

Pamoja na mafanikio hayo, safari ya uongozi haikosi changamoto.

Fatma anasema mahitaji ya elimu yanaendelea kuongezeka sambamba na ongezeko la wanafunzi. Miundombinu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na rasilimali nyingine bado vinahitaji kuimarishwa ili kuendana na mahitaji ya elimu ya kisasa.

Anaeleza kuwa, baadhi ya wanafunzi hukabiliwa na changamoto za kijamii na kiuchumi zinazoathiri maendeleo yao ya kitaaluma. Hivyo, ushirikiano kati ya shule, wazazi na jamii unaendelea kuwa muhimu katika kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayebaki nyuma.

Anasisitiza kuwa, changamoto hizo hazipaswi kuwa sababu ya kukata tamaa, bali ziwe chachu ya kutafuta suluhisho kupitia ushirikiano na ubunifu.

Maono yake

Fatma anatamani kuona Skuli ya Sekondari Fukuchani ikiendelea kuwa miongoni mwa shule bora zinazozalisha wanafunzi wenye ufaulu wa hali ya juu, maadili mema na uwezo wa kushindana katika dunia ya sasa.

Anasema kuwa,  anatamani kuona walimu wakipewa fursa zaidi za mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza ubunifu katika ufundishaji na matumizi ya teknolojia katika elimu.

Aidha kwa wasichana, ana ujumbe mahsusi kwamba wasikubali changamoto za maisha ziwe kikwazo cha kufikia ndoto zao. Anaamini elimu ndiyo silaha kubwa ya kujenga maisha bora na kuleta mabadiliko katika jamii.

Uongozi unaoacha urithi

Safari ya Fatma Dawa Pili inaonyesha kwamba uongozi si cheo, bali ni uwezo wa kuhamasisha wengine kufikia mafanikio ya pamoja.

Kutoka kijiji cha Potoa hadi kuwa Mwalimu Mkuu anayesimamia shule yenye matokeo ya asilimia 100 katika mitihani ya taifa, amethibitisha kuwa dhamira, uadilifu na kufanya kazi kwa ushirikiano vinaweza kubadilisha taasisi na kugusa maisha ya watu wengi.

 

No comments

Powered by Blogger.