JUMAZA YAUNGA MKONO MARIDHIANO YA CCM NA ACT WAZALENDO

Na Mwandishi Wetu

 Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) imesema inaunga mkono maridhiano yaliyofikiwa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo, ikieleza kuwa ni hatua muhimu ya kuimarisha amani, umoja na maendeleo ya Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Jamatkhana, Vuga, Katibu Mtendaji wa JUMAZA, Sheikh Ali Abdalla Amour, alisema jumuiya hiyo imepokea kwa furaha maridhiano yaliyotangazwa hadharani Julai 9 katika viwanja vya Ikulu Zanzibar mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Alisema, maridhiano hayo yanaonesha utayari wa viongozi wa kisiasa kuweka mbele maslahi ya Zanzibar na wananchi wake badala ya tofauti za kisiasa.

Sheikh Amour aliwataka viongozi ,waliohusika kuyasimamia makubaliano hayo kwa uaminifu na kuepuka kuyasaliti ili kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano nchini.

“Ufanisi wa maridhiano haya utategemea uaminifu, dhamira ya kweli na utekelezaji wa makubaliano kwa ikhlasi. Viongozi wote wana wajibu wa kutekeleza ahadi walizoweka mbele ya wananchi na mbele ya Mwenyezi Mungu,” alisema.

Aidha, aliwapongeza viongozi wastaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Dk. Amani Abeid Karume na Juma Duni Haji kwa mchango wao katika kusimamia mchakato wa maridhiano katika vipindi vyao vya uongozi.

“Viongozi wetu wameonesha ukomavu wa kisiasa uliowezesha kufikiwa kwa makubaliano tunayoyaona leo,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Amiri wa JUMAZA Taifa, Sheikh Mohammed Haji Omar, alisema uwepo wa nia ya dhati miongoni mwa viongozi ndio msingi wa mafanikio ya maridhiano hayo.

Alisema ,ana matumaini makubwa kuwa makubaliano hayo yataendelea kuimarika na kuleta manufaa kwa wananchi wa Zanzibar.

Alibainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo kilichobaki ni kuimarisha mshikamano wa wananchi katika nyanja za maadili, siasa na maendeleo.

“Tunayo imani kubwa kuwa mambo yatakuwa mazuri zaidi kutokana na juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali katika kuleta maendeleo,” alisema.

Naye Katibu wa Bodi ya Wadhamini wa JUMAZA, Masoud Hemed Nassor, alisema jumuiya hiyo iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali wakati wowote itakapohitajika ili kuhakikisha maridhiano hayo yanadumu na kuzaa matunda yenye manufaa kwa Zanzibar na wananchi wake.

Baadhi ya wananchi waliozungumza kwa nyakati tofauti waliunga mkono mchakato huo wa maridhiano, wakisema suluhu na maelewano ni sehemu ya mafundisho ya dini ya Kiislamu na ndiyo msingi wa kulinda amani, mshikamano na maendeleo ya taifa.

No comments

Powered by Blogger.