ZAFELA yawafikia wananchi 1,700 kwa msaada wa Kisheria



NA NUSRA SHAABAN

ZAIDI ya wananchi 1,700 kutoka shehia 14 za Unguja wamefikiwa na huduma za msaada wa kisheria kupitia mikutano ya uhamasishaji iliyoendeshwa na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa haki za kisheria na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa jamii.

Akizungumza na mwandishi wa Habari hizi , wakati wa kufungwa kwa mikutano hiyo,huko kwa Ali Nato, Mjini Unguja, Mwanasheria wa ZAFELA, Mwanaisha Mustafa Makame, alisema lengo la programu hiyo ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za msingi na kuwasaidia kupata suluhisho la changamoto mbalimbali za kisheria.

Alisema hatua hiyo ni jitihada za ZAFELA za kuendelea kusogeza huduma za elimu na msaada wa kisheria karibu na wananchi chini ya ufadhili wa UNDP ili kujenga jamii yenye uelewa wa sheria. Alifafanua kuwa kupitia mikutano hiyo wananchi walipata elimu kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, pamoja na taratibu za kufuata wanapohitaji msaada wa kisheria.



"Tunataka wananchi wafahamu haki zao na wajue wapi pa kufika wanapokumbana na changamoto za kisheria. Elimu hii ni muhimu katika kujenga jamii inayotambua sheria na kuzitumia kulinda haki zake," alisema Mwanaisha.

Alisema ili kufanikisha mikutano hiyo, ZAFELA ilishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Wasaidizi wa Sheria, Mahakama ya Kadhi, Dawati la Jinsia pamoja na Skuli ya Sheria Zanzibar, waliotoa elimu ya kisheria na kujibu maswali ya wananchi kuhusu changamoto zinazowakabili.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Sheria, Salma Abdala, aliwataka wananchi kutumia elimu waliyoipata kwa vitendo na kuendelea kutoa taarifa za matukio ya ukiukwaji wa sheria bila woga. "Ni muhimu kuripoti changamoto mapema ili zipatiwe ufumbuzi kwa mujibu wa sheria. Elimu mliyoipata leo iwe mwanzo wa kutafuta haki kwa njia sahihi," alisema.




Naye Sheha wa Kwa Ali Nato, Salum Shaaban, aliipongeza ZAFELA kwa kuifikia jamii moja kwa moja na kuwahimiza wananchi kutumia fursa za kukutana na wanasheria kueleza changamoto zao ili zipatiwe ufumbuzi wa kisheria.

. Kwa upande wake, mkazi wa Kwa Ali Nato, Fatma Khamis, alisema wananchi wamefurahishwa na ujio wa ZAFELA katika shehia yao, akieleza kuwa elimu waliyoipata imewaongezea uelewa kuhusu haki zao na kuwapa matumaini kuwa changamoto walizowasilisha zitapatiwa ufumbuzi. Aidha, mikutano hiyo ilizinduliwa Julai 13, 2026 katika Shehia ya Kandwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, na kuhitimishwa katika Shehia ya Kwa Ali Nato, Mkoa wa Mjini.




No comments

Powered by Blogger.