TAMWA ZNZ, ZANAB NA SUZA WAANDA RASIMU YA AWALI YA KOZI YA UONGOZI KWA WANAWAKE ILI KUONGEZA USHIRIKI WAO KATIKA NAFASI ZA MAAMUZI



Na Maryam Nassor

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ), kwa kushirikiana na Jumuiya ya Watu Wasioona Zanzibar (ZANAB) na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), wamefanya kikao cha awali cha rasimu wa mtaala wa mafunzo ya uongozi kwa wanawake na wasichana utakaotumika kuendesha kozi fupi chuoni hapo, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha unakidhi viwango vya kitaaluma na mahitaji ya kuwajengea uwezo wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi.

Akifungua kikao hicho kilichofanyika katika kampasi ya SUZA Tunguu Unguja , kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Said Juma alisema bado kuna pengo kubwa la uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi katika taasisi mbalimbali, hivyo mtaala huo utasaidia kuwajengea wanawake uwezo, ujasiri na maarifa ya uongozi.

Alisema hatua hiyo, inaunga mkono jitihada za kufikia usawa wa asilimia 50 kwa 50 katika nafasi za uongozi, akibainisha kuwa kwa awamu ya kwanza kozi hiyo itatolewa bila malipo kwa walimu na wanafunzi wa SUZA.

"Naamini kozi hii ni muhimu na itasaidia kupunguza pengo kubwa lililopo katika nafasi za uongozi kwa wanawake nchini," alisema Dk. Said.

Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Nairat Abdullah Ali, alisema mtaala huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa W-LEAD unaotekelezwa kwa ushirikiano na ZANAB, ukiwa na lengo la kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi na maamuzi.


Alisema uzoefu wa utekelezaji wa mradi ,umeonesha umuhimu wa kushirikiana na vyuo vikuu, kwa kuwa ndiyo vinavyoandaa viongozi wa baadaye.

"Katika uchaguzi uliopita tumeona uwakilishi wa wanawake katika nafasi za udiwani ukiongezeka kwa asilimia 25, jambo ambalo halikuwahi kushuhudiwa katika miaka ya nyuma," alisema Nairat.

Aliongeza kuwa, mafunzo yaliyotolewa kupitia mradi huo yamechangia wanawake wengi kupata ujasiri wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, zikiwemo za ngazi za juu.

Kwa upande wake,Meneja wa Kitengo cha Mawasiliano wa TAMWA ZNZ, Sophie Ngalapy, alipendekeza kozi hiyo kutolewa kama mafunzo ya muda mfupi, yanayolenga kuwajengea washiriki uwezo wa kujiamini, kuongoza na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.



Naye Mtaalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa TAMWA ZNZ, Mohamed Hatib Mohamed, alisema mradi wa W-LEAD umefikia asilimia 90 ya utekelezaji na tayari umefanikiwa kuwajengea uwezo wanawake viongozi na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Alisema kupitia utekelezaji wa mtaala huo katika SUZA na Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), wanatarajia kuona ongezeko la wanawake wenye uwezo, sifa na kujiamini kushika nafasi za uongozi.




"Changamoto kubwa iliyokuwepo ni wanawake wengi kutokujiamini kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. Kupitia mradi huu tunawajengea uwezo ili wajitokeze kwa wingi kushiriki katika maamuzi," alisema Mohamed.

Aidha aliishauri SUZA, kuweka mfumo wa takwimu utakaofuatilia idadi ya wanawake watakaopata mafunzo hayo ili kupima matokeo ya mtaala katika kuongeza ushiriki wao kwenye nafasi za uongozi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ZANAB, Rukia Saleh Ali, alisema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha wanawake vijana, wakiwemo wenye ulemavu, wanapata fursa sawa za kushiriki katika mafunzo hayo.


Alisisitiza, umuhimu wa kuweka mazingira jumuishi na rafiki kwa watu wenye ulemavu ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika utekelezaji wa mtaala huo.

Akiwasilisha rasimu ya mtaala huo, Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Msingi na Mafunzo ya Uongozi wa SUZA, Abdul Rahman Khamis, alisema kozi hiyo itafundishwa kwa muda wa wiki mbili na wahitimu watatunukiwa vyeti vinavyotambuliwa rasmi.

Alieleza kuwa, awamu ya kwanza kozi hiyo itatolewa kwa walimu na wanafunzi wa SUZA bila malipo, kabla ya kupanuliwa kwa wananchi wengine wenye uhitaji wa mafunzo hayo.

Kikao hicho cha awali cha rasimu ya mtaala wa kozi ya wanawake na uongozi kimeandaliwa na TAMWA ZNZ, kwa kushirikiana na ZANAB na SUZA na kiliwakutanisha wadau mbalimbali wa maswali ya wanawake kwa lengo la kuhakikisha mtaala huo unakidhi viwango vinavyohitajika na unachangia kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi nchini.

























No comments

Powered by Blogger.