Ashura Haji Ali : kiongozi anaye beba matumaini ya wananchi wa Mahonda


Na Maryam Nassor

Ni saa moja usiku katika Shehia ya Mahonda, Wilaya ya Kaskazini "B", Unguja. Wakati wakazi wengi wakiwa wamehitimisha shughuli za siku na kujiandaa kupumzika, simu ya Bi Ashura Haji Ali inaita.

Upande wa pili wa simu kuna sauti ya mwanamke mwenye wasiwasi.

"Mama Ashura, ng'ombe wameingia shambani kwangu. Mazao yote yanaonekana kuharibika. Nifanye nini?"

Bila kusita, Bi Ashura anamtuliza na kumshauri asichukue sheria mkononi. Kisha anamwahidi kufika alfajiri ili kujionea hali halisi.

Hivyo ndivyo yalivyo maisha yake ya kila siku.

Kwa bi Ashura Haji Ali, uongozi wake hauanzii ofisini wala hauishii kwenye mikutano anasema ni zaidi ya miaka 10 anatumikia nafasi hiyo ya Naibu sheha shehia ya Mahonda. Na uongozi wake Huanzia pale mwananchi anapohitaji msaada.

Ndiyo maana wakazi wengi wa Mahonda humfahamu kama "Mama wa Wananchi." Si cheo rasmi, bali heshima aliyojijengea kupitia huduma kwa jamii.

Safari ilivyoanza Mtende wilaya ya Kusini Unguja.

Ashura Haji Ali alizaliwa Mtende , wilaya ya Kusini Unguja, mwaka 1961, katika familia iliyomlea kwa misingi ya heshima, bidii na kuwajali wengine.

Akiwa mtoto alifundishwa kuwa mafanikio ya mtu hayapimwi kwa mali alizonazo, bali kwa mchango anaoutoa katika kubadili maisha ya wengine. Mafunzo hayo yalimjengea moyo wa huruma na hamasa ya kushiriki shughuli za kijamii.

Baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari , aliamua kuwa mwalimu, akiamini elimu ndiyo njia bora ya kuijenga jamii kupitia watoto. Kwa miaka mingi alifanya kazi kama Mwalimu Msaidizi na mshauri katika Skuli ya Msingi Mahonda, ambako hakufundisha tu kusoma na kuandika, bali pia maadili, nidhamu na moyo wa kuwajali wengine.

Wazazi wengi waliomfahamu katika kipindi hicho bado wanamkumbuka kama mwalimu aliyekuwa tayari kubaki baada ya vipindi ili kuwasaidia wanafunzi waliohitaji msaada zaidi. Hata nje ya shule, alikuwa karibu na jamii, akisikiliza migogoro ya kifamilia, kutembelea wagonjwa na kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo.

Baada ya kulitumikia taifa kwa miaka mingi katika sekta ya elimu, Ashura alistaafu mwaka 2022. Kwa wengi huo ungekuwa mwisho wa utumishi wake, lakini kwake ulikuwa mwanzo wa hatua nyingine ya kuwahudumia wananchi.

Kutokana na uadilifu, busara na uwezo wake wa kusuluhisha migogoro, wakazi wa Mahonda walimtaka aendelee kuwahudumia. Hatimaye akachaguliwa kuwa Naibu Sheha wa Shehia ya Mahonda, nafasi ambayo hadi sasa anamshikilia katika uongozi huo.

"Nilipostaafu sikuona sababu ya kukaa nyumbani wakati bado nina uwezo wa kuwasaidia watu. Niliona huu ni mwendelezo wa kazi niliyoianza miaka mingi iliyopita," anasema.

Kiongozi asiyesema 'Nimechoka'

Ukimpigia simu BiAshura, mara nyingi utasikia majibu yanayofanana.

"Sawa, nakuja."

Au:

"Nipe dakika chache nifike."

Kwa wakazi wa Mahonda, hayo si maneno ya kawaida. Ni sehemu ya maisha ya kiongozi ambaye yuko tayari kuitikia wito wakati wowote.

Simu yake hupigwa kuhusu migogoro ya mipaka, migogoro ya kifamilia, wagonjwa wanaohitaji msaada wa kufikishwa hospitalini au wakulima waliopata hasara mashambani. Kwa kila anayemtafuta,bi Ashura huamini kuwa kiongozi anapaswa kuwa karibu na wananchi kuliko wanavyokuwa karibu naye.

Anasema kusikiliza ndiyo hatua ya kwanza ya kutatua tatizo.

"Mwananchi anapopata nafasi ya kusikilizwa, tayari nusu ya tatizo lake huwa limeanza kutatuliwa."

Sheha anayemuamini

Sheha wa Mahonda, Ali Issa Kinole, anasema Bi Ashura ni miongoni mwa viongozi anaowaamini zaidi katika utendaji wa kila siku.

"Ninaweza kumkabidhi jukumu lolote nikijua halitakwama. Anafanya kazi kwa moyo, uaminifu na kujituma," anasema.

Kwa mujibu wa Sheha huyo, wakati mwingine taarifa za matatizo huwafikia wananchi kabla hata hazijamfikia yeye. Anapopiga simu kufuatilia, mara nyingi hukuta Ashura tayari amefika eneo la tukio na ameanza kushughulikia tatizo.

"Ana uwezo mkubwa wa kuwasikiliza watu. Hali hiyo imejenga imani kubwa ya wananchi kwa viongozi wa shehia," anasema.

Kusimamia haki kwa vitendo

Asya Yussuf ni miongoni mwa wakazi wa Mahonda wanaokumbuka msaada alioupata kutoka kwa Bi Ashura.

Anasema , Siku moja alikuta ndizi, mihogo na mahindi yake vimeharibiwa na ng'ombe. Aliona jasho lake la miezi kadhaa limepotea ndani ya muda mfupi.

Baada ya kupata taarifa hizo, bi Ashura alifika shambani, akakagua kiwango cha uharibifu, akawaita wahusika na kuhakikisha taratibu zote zinazohusika katika kutafuta suluhu zinafuatwa. Hatimaye Asya alipata fidia.

"Niliona kweli kuna viongozi wanaoweza kusimamia haki bila kumuogopa mtu," anasema.

Simulizi kama hiyo inaelezwa pia na Hamad Suleiman, ambaye mazao yake yaliharibiwa na mifugo. Mwanzoni alihisi asingepata haki, lakini Bi Ashura alimsaidia kufuatilia suala hilo hadi lilipopatiwa ufumbuzi na fidia kulipwa.

"Alinipa moyo wa kuamini kwamba haki inaweza kupatikana ukiwa na viongozi wanaowajali wananchi," anasema.

Uongozi wa karibu na wananchi

Ukitembea na Bi Ashura katika mitaa ya Mahonda, si vigumu kuona uhusiano wake na wananchi. Karibu kila kona kuna anayemsalimia kwa jina, anayemuita ili amweleze changamoto au mtoto anayemkimbilia kwa furaha.

Uhusiano huo haukujengwa ndani ya mikutano, bali kwa miaka mingi ya kusikiliza, kutembelea wananchi na kushiriki maisha yao ya kila siku.

BiAshura anaamini kiongozi hapaswi kusubiri wananchi wamfuate ofisini.

"Nikitaka kujua maisha ya wananchi, lazima niwaendee. Hapo ndipo ninaelewa wanachopitia na namna bora ya kuwasaidia," anasema.

Urithi wa huduma

Kwa Bi Ashura Haji Ali , anasema mafanikio hayapimwi kwa idadi ya vyeti au nafasi za uongozi alizowahi kushika.

Anasema kwake, mafanikio ni mkulima aliyepata haki, familia iliyopatanishwa, mwananchi aliyesikilizwa, kijana aliyepata ushauri na mama aliyepata mtu wa kumfariji wakati wa shida.

Kutoka Mtende alikozaliwa, kupitia taaluma yake ya ualimu katika Skuli ya Msingi M ahonda hadi kuwa Naibu Sheha wa Mahonda, safari yake imejengwa juu ya msingi mmoja usiobadilika wa huduma kwa jamii.

Katika kipindi ambacho wananchi wengi hulalamikia viongozi kutokuwa karibu nao, Bi Ashura ameamua kuwa tofauti. Amejenga uongozi unaotanguliza kusikiliza, kufika mahali penye tatizo na kufuatilia hadi suluhu ipatikane.

Kwa wakazi wa Mahonda, yeye si Naibu Sheha pekee. Ni kiongozi ambaye wamejifunza kumwamini, kumtegemea na kumwona kama sehemu ya suluhisho la changamoto zinazowakabili. Huo ndio urithi anaoujenga kupitia utumishi wake kwa jamii.

No comments

Powered by Blogger.