IIT MADRAS ZANZIBAR YAIMARISHA UJUZI WA WATAALAMU KUPITIA MAFUNZO YA EPIDEMIOLOJIA NA DATA SCIENCE



Na Mwatima Issa

Taasisi ya Teknolojia ya India Madras Kampasi ya Zanzibar (IITMZ) imeendelea kuimarisha mpango wake wa utoaji wa mafunzo ya muda mfupi yenye mwelekeo wa vitendo kwa wanafunzi na watendaji kutoka sekta mbalimbali nchini, kwa lengo la kukuza ujuzi, vipaji na kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi.

Dhamira hiyo imejidhihirisha kupitia uzinduzi wa mafunzo ya muda mfupi ya Sayansi ya Data kwa Epidemiolojia na Uchambuzi wa Afya ya Jamii (Data Science for Epidemiology and Public Health Analytics) yaliyoandaliwa na IITMZ.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Utawala wa IITMZ, Dkt. Idrissa Said Amour, amesema kuwa taasisi hiyo inaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa watu wengi zaidi wanapata fursa ya kujengewa uwezo kupitia mafunzo ya kisasa ya kisayansi yenye mwelekeo wa vitendo, yatakayochangia kuboresha utendaji wao wa kazi.




Aidha, Dkt. Amour ameeleza kuwa uwepo wa IITMZ visiwani Zanzibar umefungua fursa kwa wananchi wa Zanzibar, Tanzania na Afrika kwa ujumla kupata elimu na mafunzo yenye viwango vya kimataifa bila kulazimika kusafiri nje ya nchi. Amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya dhamira ya taasisi ya kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kutumia teknolojia na uchambuzi wa data katika kutatua changamoto za afya ya jamii na maendeleo endelevu.

Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka IITMZ Dkt. Sweta Dey amesema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwajengea washiriki ujuzi wa kutumia Sayansi ya Data, Akili Unde (AI) na mbinu za kisasa za uchambuzi wa taarifa za afya ili kukabiliana na changamoto za afya ya jamii na magonjwa ya mlipuko. Amesema kuwa, yanawaunganisha wataalamu wa afya na teknolojia ili kuongeza uwezo wa kutatua changamoto za afya kwa kutumia taarifa na ushahidi.

Aidha, Dkt. Dey ameeleza kuwa katika dunia ya sasa, matumizi ya takwimu na uchambuzi wa kisasa yamekuwa nguzo muhimu katika kuboresha mifumo ya afya ya jamii. Amesema kuwa teknolojia za Sayansi ya Data zinasaidia kutabiri mwenendo wa magonjwa, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na kusaidia watunga sera kufanya maamuzi sahihi yanayotegemea ushahidi.

Akihitimisha, Dkt. Dey amewahimiza washiriki kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ili kupata ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kutumia teknolojia za kisasa katika kutatua changamoto za afya. Ameeleza matumaini yake kuwa maarifa yatakayopatikana yatachangia kuimarisha tafiti, kuboresha huduma za afya na kuleta suluhisho endelevu kwa manufaa ya jamii.

Naye msimamizi Mkuu wa mafunzo Prof. Manoj Kumar, amewataka washiriki hao kuwa huru kwa kutumia ujuzi wao ipasavyo ikiwa ni sehemu ya mafunzo hayo. Hata hivyo, amewataka washiriki kuwa karibu kubadilishana ujuzi katika katika kipindi chote cha mafunzo ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Wakitoa maoni yao washiriki wa mafunzo hayo wamesema kuwa wameridhishwa na upekee wa aina ya mafunzo yanayotolewa kwa watendaji na wanafunzi mbalimbali nchini kupitia wa IITMZ na kuahidi kuendelea kutumia fursa zinazoendelea kutolewa kujifunza.

Mafunzo hayo ya wiki mbili yanahusisha jumla ya washiriki 27 kati yao ni watendaji kutoka katika sekta za afya, takwimu, tafiti na wanafunzi wa elimu ya juu wanaomomea fani za sayansi.





No comments

Powered by Blogger.