Viongozi Wanawake kutoka Vyombo vya Habari Wapatiwa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi

Na Maryam Nassor
WANAWAKE viongozi kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini Tanzania wameshiriki mafunzo ya siku tatu kuhusu uongozi na usimamizi, yanayolenga kuimarisha usimamizi wa vyumba vya habari (newsrooms), kuongeza uendelevu wa taasisi za habari na kukuza ubunifu katika sekta hiyo.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa
kushirikiana na Taasisi ya Finland ya Vyombo vya Habari na Maendeleo (VIKES)
kupitia mradi wa Media and Rights Empowerment Initiative (MREI).
Akifungua mafunzo hayo, huko Morogoro katika hotel ya Antique Legacy Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Katibu Mkuu wa Mabaraza ya Habari Kimataifa, Ernest Sungura, amesema mpango huo unalenga kuwapa wanawake viongozi ujuzi wa vitendo katika uongozi na usimamizi ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya habari, hususan katika enzi ya mabadiliko ya kidijitali.

Amesema washiriki 12 kutoka vyombo vya habari vya magazeti, redio,
televisheni na mitandao ya kidijitali wanashiriki katika mafunzo hayo yenye
lengo la kuwajengea uwezo wa kuongoza taasisi za habari katika mazingira
yanayobadilika kwa kasi.
Kwa mujibu wa Sungura, wanawake wana nafasi muhimu katika kuunda taswira ya sekta ya habari nchini, na kuimarisha uwezo wao wa kiuongozi kutachangia kujenga taasisi imara za habari, kuendeleza uandishi wa habari wenye weledi na kuhudumia maslahi ya umma.

Ameeleza kuwa kupitia mradi wa MREI, MCT inawekeza katika kuwawezesha
wanawake viongozi wa vyombo vya habari ili taasisi wanazoongoza ziweze
kujitegemea, kuwa na uhimilivu wa kifedha na kuendelea kutoa huduma bora za
habari.
Aidha, amewahimiza washiriki kutumia maarifa na ujuzi watakaoupata katika mafunzo hayo kuleta maboresho yanayoweza kupimika ndani ya siku 90 baada ya kukamilika kwa programu hiyo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa MREI, Ziada Kilobo, amesema mafunzo
hayo yanajumuisha mada mbalimbali, ikiwemo uongozi wa kimkakati, usimamizi wa
fedha, usimamizi wa rasilimali watu, ushirikishwaji wa hadhira, mageuzi ya
kidijitali pamoja na utawala wa uhariri.
Kilobo amesema lengo la programu hiyo ni kuimarisha utendaji wa uhariri
na kuongeza uendelevu wa taasisi za habari huku zikiendelea kuzingatia viwango
vya taaluma na maadili ya uandishi wa habari.
Aidha, amewataka viongozi hao kuyatumia mafunzo hayo kutafuta suluhisho
la changamoto za kifedha zinazoathiri vyombo vya habari wanavyoviongoza.
"Ni vyema baada ya mafunzo haya tukashuhudia mabadiliko chanya katika utendaji kazi wenu, lakini pia katika kubuni na kutafuta vyanzo vya mapato vitakavyoviwezesha vyombo vyenu vya habari kujiendesha kwa ufanisi," amesema Kilobo.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki, Zainab Abdallah kutoka
Azam Media amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha utendaji katika taasisi
zao na kuwapa uwezo wa kubuni na kuandaa miradi mbalimbali itakayochangia
kuongeza mapato na kuimarisha uendelevu wa vyombo vya habari wanavyoviongoza.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wanawake viongozi 12 kutoka vyombo vya habari vya magazeti, redio, televisheni na mitandao ya kidijitali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za MCT kupitia mradi wa MREI za kuimarisha uongozi, usimamizi na uhimilivu wa sekta ya habari nchini Tanzania.

Post a Comment