Kutoka kupiga debe hadi kiongozi: Safari ya Azmina na mapambano ya viongozi wanawake vijana Zanzibar


Na Maryam Nassor

"Nilichoka kuona wanawake na vijana wakitumika kupiga kampeni wakati wa uchaguzi, lakini wakibaki pembeni wakati wa kufanya maamuzi."

Kauli hiyo ya Azmina Said Jabiri, mwanamke mwenye umri wa miaka 26 kutoka Zanzibar, inaeleza kwa ufupi hali ambayo imeendelea kuwakabili wanawake wengi vijana katika siasa. Kwa miaka mingi wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wapiga kura, kushiriki mikutano ya kampeni na kuwapigia debe wagombea, lakini nafasi za kufanya maamuzi zimeendelea kubaki mikononi mwa wachache.

Hicho ndicho kilichomsukuma Azmina kuingia katika siasa. Hakutafuta umaarufu wala madaraka, bali alitaka kuthibitisha kwamba mwanamke kijana anaweza kushiriki kikamilifu katika uongozi na kutoa mchango unaoonekana katika maendeleo ya jamii.

"Niliingia katika siasa kwa sababu niliona masuala mengi yanayowahusu vijana hayapewi nafasi ya kutosha katika sera, mipango na bajeti. Mara nyingi maamuzi yalifanywa bila sauti za vijana, hususan wanawake vijana, kusikika," anasema.

Leo hii Azmina ni Mwenyekiti wa UVCCM Jimbo la Kwahani. Hata hivyo, nafasi hiyo haikuja kwa urahisi. Ni matokeo ya miaka ya kujifunza, kuvumilia na kukabiliana na changamoto ambazo wanawake wengi vijana hukutana nazo wanapoamua kuingia katika siasa.

Safari iliyoanzia nyuma ya pazia

Azmina anasema alianza kuvutiwa na siasa mwaka 2010 akiwa bado mdogo. Kila uchaguzi ulipofika aliona wanawake wengi wakihamasisha wananchi, kuandaa mikutano na kushiriki shughuli mbalimbali za kampeni. Lakini baada ya uchaguzi kumalizika, waliokuwa mstari wa mbele walitoweka katika meza za maamuzi.

Kadiri alivyokua, ndivyo alivyozidi kujiuliza kwa nini wanawake wengi waliishia kuwa wapiga debe badala ya kuwa viongozi.

Swali hilo ndilo lililomjengea hamasa ya kuingia katika siasa akiwa na lengo la kubadilisha mtazamo huo.


"Niliamini kuwa kama hakuna wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi, hali itaendelea kuwa ileile kwa miaka mingi ijayo," anasema.

Kushindwa kulimfundisha uongozi

Mwaka 2025, Azmina aliamua kuwania nafasi ya udiwani. Alikuwa na matumaini makubwa ya kushinda, lakini aliondolewa katika kura za mchujo.

Badala ya kukata tamaa, aliamua kujifunza.

"Nilidhani udiwani ni nafasi ambayo ningeipata kwa urahisi. Lakini niligundua kuwa siasa zinahitaji maandalizi ya muda mrefu, kujenga mtandao wa watu na kuelewa mazingira ya ushindani. Kushindwa kwangu kulinifunza kuwa uongozi si jambo la kukurupuka."

Anasema uzoefu huo ulimfundisha umuhimu wa kupanga mikakati, kujenga mahusiano na kutambua kwamba katika siasa ushindi haupatikani kwa nia njema pekee, bali pia kwa maandalizi na uvumilivu. 

Mbali na kushindwa, anakumbuka pia kipindi kigumu alichopitia wakati wa harakati hizo.

"Nilikumbana na vitisho na shinikizo kubwa kiasi kwamba afya yangu iliathirika na nikapungua uzito. Lakini sikuruhusu changamoto hizo zizime ndoto yangu ya kuwatumikia wananchi."


Licha ya maumivu hayo, Azmina hakurudi nyuma. Aliendelea kushiriki shughuli za kisiasa huku akijifunza kutoka kwa kila changamoto aliyokutana nayo.

Ndoto iliyotimia

Baadaye, Azmina aligombea nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Jimbo la Kwahani. Katika mchakato huo alikabiliana na ushindani mkali kutoka kwa wagombea wengine. Baada ya hatua mbalimbali za uchaguzi, aliibuka mshindi.

Kwa Azmina, ushindi huo haukuwa mwisho wa safari, bali mwanzo wa wajibu mkubwa zaidi.

Anasema nafasi hiyo inampa fursa ya kuwaunganisha vijana, kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za maendeleo, kujenga uongozi unaowajumuisha wanawake na kuhimiza vijana kujiajiri kupitia ujasiriamali.

Hata hivyo, anaamini mafanikio yake hayawezi kufuta ukweli kwamba wanawake wengi vijana bado wanakabiliwa na vikwazo vinavyowazuia kufikia nafasi za maamuzi.

"Ningependa kuona wanawake wengi zaidi wakijitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. Tukibaki wachache, tutakuwa tunabadilisha simulizi la mtu mmoja badala ya kubadilisha mfumo mzima."

Simulizi ya Azmina si hadithi ya ushindi wa mtu mmoja pekee. Ni kielelezo cha changamoto zinazoendelea kuwakabili wanawake wengi vijana Zanzibar wanapotafuta nafasi katika uongozi wa kisiasa na kijamii.

Changamoto zinazowazuia wanawake vijana kufika kwenye meza za maamuzi

Safari ya Azmina inaonyesha kwamba mafanikio katika siasa yanawezekana. Hata hivyo, simulizi yake pia inaakisi hali inayowakumba wanawake wengi vijana Zanzibar, ambao licha ya kuwa na uwezo na elimu, bado hukutana na vizingiti vinavyowafanya wasifikie nafasi za maamuzi kwa urahisi.

Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, wanawake ni takribani asilimia 51.6 ya wakazi wa Zanzibar. Hata hivyo, idadi hiyo kubwa haijaakisiwa ipasavyo katika nafasi za uongozi wa kisiasa na taasisi nyingine za maamuzi. Uwakilishi wa wanawake bado uko chini ya kiwango kinachotarajiwa ukilinganisha na mchango wao katika maendeleo ya jamii.

Wataalamu wa masuala ya jinsia wanaeleza kuwa tatizo hilo halitokani na ukosefu wa uwezo wa wanawake, bali ni matokeo ya mchanganyiko wa changamoto za kijamii, kiuchumi na kimfumo ambazo zimeendelea kujirudia kwa miaka mingi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni mitazamo ya kijamii inayohusisha uongozi na wanaume, gharama kubwa za kushiriki katika siasa, ukosefu wa mitandao ya kisiasa kwa wanawake vijana, pamoja na vitisho na unyanyasaji wa kisiasa unaowafanya baadhi yao kuogopa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali.

Azmina anasema changamoto hizo si za kinadharia, bali ni hali aliyoishi mwenyewe.

"Wakati wa kugombea nilikutana na shinikizo kubwa. Wakati mwingine unajiuliza kama kweli unastahili kuendelea. Lakini nilijikumbusha kuwa nikikata tamaa, nitakuwa nimewaongezea nguvu wanaoamini wanawake hawawezi kuwa viongozi."

Kauli yake inaonyesha kuwa mapambano ya wanawake wengi vijana hayaishii kwenye ushindani wa kura pekee, bali pia yanahusisha vita ya kupambana na hofu, dhana potofu na mazingira ambayo wakati mwingine hayatoi fursa sawa kwa wagombea wote.

Sheria na Sera zinasemaje?

Tanzania imeweka msingi wa kisheria unaotambua usawa wa wanawake na wanaume katika kushiriki maisha ya kisiasa na kijamii. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua haki ya kila mwananchi kushiriki katika shughuli za umma bila ubaguzi, huku Katiba ya Zanzibar nayo ikisisitiza misingi ya usawa na haki kwa wananchi wote.

Aidha, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jinsia, pamoja na ahadi mbalimbali ambazo Tanzania imeridhia katika ngazi za kikanda na kimataifa, zinataka wanawake washiriki kikamilifu katika nafasi za maamuzi.

Miongoni mwa ahadi hizo ni Itifaki ya Maputo, ambayo inazitaka nchi wanachama kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa katika uongozi na siasa, pamoja na Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, inayosisitiza kujengwa kwa jamii jumuishi yenye ushiriki sawa wa wanawake na wanaume.

Vilevile, Lengo la Tano la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 5) linazitaka nchi kuhakikisha wanawake wanapata ushiriki kamili na wenye usawa katika ngazi zote za kufanya maamuzi katika maisha ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa sheria, sera na ahadi hizo, bado pengo kati ya maandishi na utekelezaji linaendelea kujitokeza. Wanawake wengi vijana wanaendelea kukumbana na mazingira yanayowafanya kushiriki katika kampeni za kisiasa bila kupata nafasi zinazolingana katika kufanya maamuzi.

Wajibu wa Taasisi

Wachambuzi wa masuala ya utawala bora wanaeleza kuwa kuongeza idadi ya wanawake vijana katika nafasi za uongozi si jukumu la wanawake pekee.

Vyama vya siasa vinapaswa kuweka mazingira yanayowawezesha wanawake vijana kugombea nafasi mbalimbali kwa usawa, huku taasisi za umma zikiendelea kuimarisha utekelezaji wa sera zinazokuza ushiriki wa wanawake katika maamuzi.

Aidha, viongozi wa dini, wazee wa mila, familia na jamii kwa ujumla wanayo nafasi muhimu katika kubadili mitazamo inayowafanya wanawake waonekane kuwa wasaidizi wa viongozi badala ya viongozi wenyewe.

Bila mabadiliko ya kimfumo na ya kimtazamo, wanawake wengi vijana wataendelea kubaki mstari wa mbele wakati wa kampeni, lakini nyuma ya pazia wakati wa maamuzi.

W-LEAD: Jaribio la kubadili simulizi

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA Zanzibar) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kimeanzisha programu ya Women Leadership, Empowerment, Access and Development (W-LEAD) inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake vijana na watu wenye ulemavu katika nafasi za uongozi na maamuzi.

Programu hiyo inalenga kuwajengea wanawake vijana maarifa, ujasiri na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika michakato ya kidemokrasia, kujiamini wanapowania nafasi za uongozi na kujenga mitandao ya kitaaluma itakayowawezesha kusonga mbele katika safari zao za uongozi.

Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa TAMWA Zanzibar, Mohamed Khatib Mohamed, anasema programu hiyo imepangwa kuwafikia wanawake vijana 100 kupitia mafunzo ya uongozi na maendeleo ya stadi mbalimbali, huku wanawake vijana 60 wakipata fursa ya kujifunza kwa vitendo ndani ya taasisi za umma, sekta binafsi na asasi za kiraia.

Anasema mafunzo hayo, yatawasaidia washiriki kuelewa mifumo ya utawala, kujenga uwezo wa kufanya maamuzi, kuimarisha mawasiliano ya kiuongozi na kuongeza kujiamini wanaposhiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Mbali na kuwajengea uwezo wanawake vijana, programu hiyo pia inalenga kuwafikia zaidi ya wananchi 100,000 kupitia kampeni za kuhamasisha usawa wa kijinsia. Lengo ni kubadili mtazamo wa jamii kuhusu nafasi ya wanawake katika uongozi na kujenga mazingira yanayowapa wanawake na watu wenye ulemavu fursa sawa za kushiriki katika kufanya maamuzi.



Kwa upande wake, Mratibu wa mradi kutoka Jumuiya ya Watu Wasioona Zanzibar (ZANAB), Rukia Saleh Ali, anasema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa wanawake vijana, wakiwemo wenye ulemavu, hawabaki nyuma katika juhudi za kujenga kizazi kipya cha viongozi.

Anasema ujumuishaji wa wanawake wenye ulemavu katika programu hiyo ni hatua muhimu ya kuhakikisha kuwa fursa za uongozi zinawafikia wanawake wote bila ubaguzi.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo, Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Nairat Abdullah Ali, anasema licha ya wanawake kuwa zaidi ya nusu ya wakazi wa Zanzibar, uwakilishi wao katika nafasi za maamuzi bado uko chini ya kiwango kinachotarajiwa.

Anasema, hali hiyo imechangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo mila na desturi zinazowapa wanaume nafasi kubwa zaidi katika uongozi, pamoja na mazingira ya kijamii ambayo kwa muda mrefu yamewafanya wanawake wengi kukosa kujiamini kugombea nafasi za maamuzi.

 

"Kupitia programu hii tunalenga kuwawezesha wanawake, hususan wanawake vijana na watu wenye ulemavu, kujenga uwezo wa uongozi, kujiamini na kushiriki kikamilifu katika mifumo ya kidemokrasia na nafasi za maamuzi," anasema.

 

Kwa mujibu wa TAMWA Zanzibar, programu hiyo pia inaunga mkono utekelezaji wa ahadi mbalimbali ambazo Tanzania imeziridhia katika ngazi za kikanda na kimataifa, zikiwemo Itifaki ya Maputo na Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika zinazosisitiza ushiriki sawa wa wanawake na wanaume katika vyombo vya maamuzi.

Mradi wa W-LEAD unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya TAMWA Zanzibar, Jumuiya ya Watu Wasioona Zanzibar (ZANAB), Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Zanzibar University. Mradi huo unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia mpango wa Women and Youth Democratic Engagement (WYDE) na unatarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2027.

 

Zaidi ya simulizi ya Azmina

Kwa Azmina, mafanikio ya kweli hayaishii kushinda uchaguzi wa ndani wa chama. Anaamini ushindi mkubwa zaidi utapatikana pale ambapo wanawake wengi vijana wataacha kuonekana kama nguvu ya kampeni pekee na kuanza kuwa sehemu ya kawaida ya meza za maamuzi.

 

"Nitafurahi zaidi nikiona wanawake wengi wakigombea nafasi za uongozi bila hofu. Uongozi haupaswi kuamuliwa na jinsia, bali na uwezo, maono na utayari wa kuwatumikia wananchi."

Kauli hiyo inabeba ujumbe mpana kuliko maisha yake binafsi. Inaonyesha kuwa safari ya mwanamke mmoja inaweza kuwa kichocheo cha mabadiliko ya mfumo mzima ikiwa taasisi za umma, vyama vya siasa, mashirika ya kiraia na jamii kwa ujumla zitachukua hatua za kuondoa vikwazo vinavyowazuia wanawake vijana kushiriki kikamilifu katika uongozi.

Safari ya Azmina inaonesha kuwa uwezo wa wanawake vijana si tatizo. Changamoto kubwa ni mazingira yanayowazunguka. Endapo sheria, sera na mipango ya kuwawezesha wanawake itatekelezwa kwa vitendo na si kwa maandishi pekee, Zanzibar inaweza kujenga kizazi kipya cha viongozi wanawake kitakachochangia maendeleo jumuishi na utawala unaowakilisha wananchi wote.

Kwa maana hiyo, simulizi ya Azmina si hadithi ya ushindi wa mwanamke mmoja. Ni kioo kinachoonyesha safari ambayo wanawake wengi vijana bado wanaendelea kuitembea; safari ya kutoka kuwa wapiga debe hadi kuwa viongozi wanaoshiriki kikamilifu katika kuamua mustakabali wa jamii yao.

No comments

Powered by Blogger.