Mifumo ya kidijitali kuimarisha uwazi wa mikopo Zanzibar

Na Maryam Nassor

Teknolojia imeendelea kubadili jinsi taasisi za umma zinavyotoa huduma kwa wananchi. Kwa kutumia mifumo ya kidijitali, huduma nyingi zimekuwa rahisi kupatikana; zimeongeza uwazi na kupunguza urasimu.

Zanzibar nayo ina nafasi ya kutumia teknolojia kuimarisha usimamizi wa mikopo ya maendeleo inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mfumo wa 4-4-2, ili kuhakikisha fursa hizo zinawafikia walengwa kwa haki, uwazi na ufanisi.

Katika miaka ya hivi karibuni, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kutekeleza mpango huo kwa lengo la kuongeza ushiriki wa makundi maalumu katika shughuli za kiuchumi, kupunguza umaskini na kuchochea maendeleo ya jamii.

Hata hivyo, pamoja na dhamira hiyo, changamoto za ukosefu wa uwazi, ucheleweshaji wa majibu ya maombi, upatikanaji mdogo wa taarifa na kutokuwepo kwa mfumo wa kidijitali wa kufuatilia maombi zimeendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali.

Wadau wa maendeleo na wataalamu wa sera wanaamini kuwa matumizi ya teknolojia yanaweza kubadili hali hiyo kwa kuongeza uwajibikaji wa taasisi zinazotekeleza mpango huo na kujenga imani ya wananchi.

Mfumo wa kidijitali unaweza kuondoa malalamiko

Mchambuzi wa sera za Uchumi Zanzibar, Almass Mohamed, anasema mfumo wa kidijitali unaweza kupunguza changamoto nyingi zinazohusiana na utoaji wa mikopo.

"Mwombaji anatakiwa aweze kufuatilia maombi yake kwa kutumia simu au tovuti. Aone lini maombi yamepokelewa, yako hatua gani, yameidhinishwa au yamekataliwa pamoja na sababu zake. Huo ndio msingi wa uwazi."

Anaongeza kuwa, mfumo huo unapaswa kuwa na taarifa zinazoonyesha idadi ya waombaji, walionufaika, fedha zilizotolewa kwa kila wilaya na shehia pamoja na  kiwango cha marejesho ya mikopo.

Kwa mujibu wake, upatikanaji wa taarifa hizo utapunguza malalamiko ya upendeleo na kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi zinazotekeleza mpango huo.

Wadau wa maendeleo wataka uwazi zaidi

Mkurugenzi wa Jumuiya  ya Wanawake wenye  Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) inayojihusisha na uwezeshaji wa wanawake, Salma Saadat, anasema wananchi wengi bado hawajui kiasi cha fedha kinachotengwa kila mwaka wala namna kinavyogawiwa.

"Wananchi wakipata taarifa za wazi wataweza kuuliza maswali sahihi na kufuatilia matumizi ya fedha za umma. Hiyo ndiyo tafsiri halisi ya uwajibikaji."

Anashauri pia kuwa, kila halmashauri ichapishe taarifa za kila robo mwaka zikionyesha kiasi cha fedha kilichotolewa, idadi ya wanufaika, aina za biashara zilizofadhiliwa na kiwango cha marejesho ya mikopo.

UN Women: Uwezeshaji wa wanawake ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi

Hoja za wataalamu hao zinaungwa mkono na UN Women. Katika makala yake ya mwaka 2023 yenye kichwa Five Things to Accelerate Women's Economic Empowerment, shirika hilo linaeleza kuwa wanawake duniani bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa mitaji na huduma za kifedha, hali inayozuia ukuaji wa biashara zao.

UN Women inakadiria kuwa, biashara ndogo na za kati zinazomilikiwa na wanawake zinakabiliwa na pengo la upatikanaji wa mitaji linalofikia takribani dola za Marekani trilioni 1.7 duniani.

Shirika hilo linaeleza kuwa kuziba pengo hilo kupitia sera bora, huduma za kifedha jumuishi na matumizi ya teknolojia kunaweza kuongeza mapato ya biashara zinazomilikiwa na wanawake kwa wastani wa asilimia 12 ifikapo mwaka 2030.

Aidha, UN Women inasisitiza kuwa uwekezaji katika teknolojia, elimu ya fedha, taarifa sahihi na huduma za kifedha zinazowafikia wanawake ni miongoni mwa njia muhimu za kuongeza ushiriki wao katika uchumi na kukuza maendeleo endelevu.

Katika muktadha wa Zanzibar, wataalamu wanaamini kuwa mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa mikopo unaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuwafikia wanawake wengi zaidi, kupunguza gharama za kufuatilia huduma na kuongeza uwazi katika utoaji wa mikopo ya 4-4-2.

Baraza la Wawakilishi lina wajibu wa kusimamia uwajibikaji

Mwakilishi wa Jimbo la Paje, Jaku Hashimu Ayoub, anasema Baraza la Wawakilishi lina wajibu wa kuhakikisha fedha za umma zinazotengwa kwa ajili ya uwezeshaji wa wananchi zinatumika kwa uwazi na ufanisi.

"Tunapaswa kuhoji bajeti zilizotengwa, fedha zilizotolewa na matokeo yaliyopatikana. Wananchi wanahitaji kuona fedha zao zinaleta maendeleo halisi."

Anasema matumizi ya mifumo ya kidijitali yatawawezesha wajumbe wa Baraza kufanya ufuatiliaji kwa kutumia takwimu sahihi badala ya taarifa za jumla.

Wananchi wanataka mfumo unaoeleweka

Katika mahojiano na baadhi ya viongozi wa vikundi vya wanawake na vijana, wengi walieleza kuwa changamoto kubwa ni kutokupata mrejesho kuhusu maombi yao baada ya kuyawasilisha.

Mwenyekiti wa kikundi cha wanawake kutoka Kaskazini Unguja, Bi. Halima Ali, anasema:

"Tunaomba mikopo lakini mara nyingi hatupati mrejesho. Mfumo wa simu au mtandao ungeondoa usumbufu wa kufuatilia ofisi hadi ofisi."

Kwa upande wake, kijana mjasiriamali Ahmed Juma anasema mfumo wa kidijitali ungepunguza gharama za usafiri na muda wa kufuatilia maombi.

"Tungepata pia elimu ya kutumia mifumo ya kujaza maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao. Hilo lingeongeza uelewa wetu na kurahisisha upatikanaji wa mikopo."

Wataalamu wanapendekeza nini?

Mtaalamu wa sera na utawala bora Zanzibar, Hafidh Ibrahim, anasema suluhisho la muda mrefu ni kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya kidijitali.

Anapendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kufuatilia maombi ya mikopo kwa kutumia simu na tovuti, kuchapishwa kwa takwimu za wanufaika kila robo mwaka na kutoa sababu za kukubaliwa au kukataliwa kwa maombi ili kuongeza uwazi.

Aidha, anashauri kuanzishwa kwa mfumo wa kupokea malalamiko kwa njia ya mtandao, kutoa mafunzo ya matumizi ya mifumo ya kidijitali kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya ZEEA, halmashauri na Baraza la Wawakilishi.

"Teknolojia inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata mikopo kwa haki, uwazi na kwa wakati."

Hitimisho

Mifumo ya kidijitali si suala la teknolojia pekee, bali ni nyenzo ya kujenga uwajibikaji, uwazi na usawa katika utoaji wa huduma za umma.

Kwa Zanzibar, uwekezaji katika mfumo wa kisasa wa usimamizi wa mikopo unaweza kuongeza imani ya wananchi, kupunguza malalamiko na kuhakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanapata fursa zinazostahili.

Kadiri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyoendelea kutekeleza sera za uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, matumizi ya teknolojia yanapaswa kwenda sambamba na uchapishaji wa takwimu za utekelezaji, usimamizi madhubuti wa fedha na ushiriki wa wananchi katika kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma.

Kwa kufanya hivyo, mpango wa 4-4-2 unaweza kuwa mfano wa mafanikio katika kujenga uchumi shirikishi unaowanufaisha wananchi wote na kuchochea maendeleo endelevu ya Zanzibar.

 

No comments

Powered by Blogger.