Waandishi wa Habari Zanzibar Watakiwa Kuandika Habari za Takwimu Zinazoleta Suluhu kwa Jamii
Na Maryam Nassor
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuzingatia matumizi ya
takwimu katika uandishi wao ili kuzalisha habari zenye ushahidi, zinazoibua
changamoto na kupendekeza suluhu zenye manufaa kwa jamii.
Wito huo ,umetolewa na Afisa Habari na Mawasiliano wa Chama cha Waandishi
wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ), Khairat Ali, wakati wa
kufunga mafunzo ya siku mbili yaliyowakutanisha waandishi wa habari 20 kutoka vyombo mbali mbali vya habari kisiwani Unguja.
Khairat amesema ,mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika kuandika habari zinazozingatia takwimu, haki za wanawake katika uongozi, haki za kidemokrasia na uandishi wa habari za tija zinazochangia maendeleo ya jamii.
"Tumewafundisha masuala ya takwimu kwa sababu tunataka kuona
jitihada zetu katika kushughulikia masuala ya wanawake na uongozi zimefikia
wapi, zimeleta mafanikio kwa kiwango gani, na jamii imezipokea kwa namna
gani," amesema Khairat.
Kwa upande wake, mkufunzi wa mafunzo hayo, Dk. Imane Duwe, amesema mafunzo hayo yalijikita katika uandishi wa habari unaotoa suluhu (Solutions Journalism) pamoja na uandishi unaotumia takwimu kuonyesha picha halisi ya changamoto na mafanikio yaliyopo katika jamii.
Amesema, waandishi wa habari wanapaswa kutumia takwimu kama nyenzo ya
kuongeza uwajibikaji na kuangazia viongozi na watu wanaotoa huduma muhimu kwa
jamii, hususan wanawake waliopo katika ngazi za chini za uongozi ambao mara
nyingi hawapati kutambulika licha ya mchango wao mkubwa.
Aidha, amewasisitiza washiriki kuhakikisha makala watakazoandika
zinaunganisha takwimu sahihi na mapendekezo ya suluhu ili kusaidia jamii na
watunga sera kufanya maamuzi yenye tija.
Naye mjumbe wa TAMWA ZNZ, Bi. Shifaa Said, amewataka waandishi wa
habari kuendelea kuzingatia maadili ya taaluma na sheria za nchi wanapotekeleza
majukumu yao ili kulinda taaluma yao na kuepuka migogoro ya kisheria.
Amesema kuwa, ni muhimu vyombo vya habari kuwaibua wanawake
waliopo katika nafasi mbalimbali za uongozi wa ngazi za jamii ambao kazi zao
hazijulikani kwa wananchi, licha ya mchango wao mkubwa katika maendeleo.
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo, Hadija Juma na Zurima
Ramadhan, wameishukuru TAMWA ZNZ kwa kuwawezesha kushiriki mafunzo hayo,
wakisema yamewaongezea ujuzi wa kuandika habari zinazotumia takwimu na kutoa
suluhu kwa changamoto zinazoikabili jamii.
Mafunzo hayo ya siku mbili , yameandaliwa na TAMWA ZNZ kwa waandishi wa habari 30, ambapo 20 walitoka Unguja na 10 kutoka Pemba. Yalilenga kuimarisha uwezo wa waandishi katika uandishi wa habari za tija, matumizi ya takwimu na mbinu za uandishi unaotoa suluhu kwa maendeleo ya jamii.
Post a Comment