Mikopo ya Asilimia 10: Ahadi bado haijatimizwa kwa wote
Mikopo ya Asilimia 10: Ahadi bado haijatimizwa kwa wote,
-
Walitimiza
masharti, lakini bado wanasubiri,
Na Maryam
Nassor
Zaidi ya
mwaka mmoja umepita tangu Khadija Abdalla na wenzake wa kikundi cha wanawake
kutoka Shehia ya Mahonda, Wilaya ya Kaskazini 'B', Unguja, waanze kufuatilia
mkopo wa asilimia 10 unaotolewa kupitia mfumo wa 4-4-2. Walisajili kikundi,
wakafungua akaunti ya benki na kukamilisha masharti yote yaliyowekwa wakiamini
wangepata mtaji wa kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali.
Badala
yake, wameendelea kusubiri bila kujua lini watafaidika na mpango huo.
Kila
wanapofuatilia maombi yao, hupewa jibu lilelile:
"Jisajilini
tena kwenye mfumo mpya wa kidijitali."
Kwa
Khadija, majibu hayo yamekuwa yakijirudia kwa miezi mingi bila kupewa taarifa
zinazoonyesha hatua iliyofikiwa au sababu ya kuchelewa kwa mkopo.
"Tuna
hamu ya kupata mkopo huu ili kuendeleza shughuli zetu za ujasiriamali. Lakini
mpaka leo bado hatujafanikiwa. Kila tunapoulizia tunaambiwa tujisajili tena
kwenye mfumo wa kidijitali badala ya ule wa awali wa karatasi," anasema.
Simulizi yake si ya kipekee. Inaakisi hali inayowakabili wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar ambao, licha ya kutimiza masharti, bado hawajapatiwa mikopo au taarifa za kueleweka kuhusu maombi yao.
Maswali yanayohitaji
majibu
Malalamiko
ya wananchi yanaibua maswali muhimu. Mikopo hiyo inatolewa kwa utaratibu gani?
Ni nani anayestahili kunufaika? Kwa nini baadhi ya vikundi hupata mikopo mapema
huku vingine vikisubiri kwa muda mrefu bila maelezo ya wazi?
Maswali
haya yanaonyesha umuhimu wa kuangalia kwa karibu utekelezaji wa mpango huu na
kama kweli unatimiza lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Mikopo ya
asilimia 10 ni mpango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar unaolenga kuwawezesha
wananchi kupitia sehemu ya mapato ya ndani ya halmashauri. Kupitia mfumo wa
4-4-2, asilimia nne ya fedha hutengwa kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana na
asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.
Lengo lake
ni kuongeza mitaji kwa makundi hayo, kukuza ajira, kupunguza umaskini na
kuimarisha shughuli za uzalishaji mali.
Mpango huu
umejengwa juu ya Sheria ya Serikali za Mitaa Na. 9 ya mwaka 2023 na Sheria ya
Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) Na. 2 ya mwaka 2022,
ambazo zinaelekeza halmashauri na ZEEA kusimamia utekelezaji wa programu za
uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Pamoja na msingi huo wa kisheria, simulizi za walengwa zinaonyesha bado kuna pengo kati ya matarajio ya wananchi na utekelezaji wa mpango.
Masharti yanayowakwamisha
baadhi ya walengwa
Kwa watu
wenye ulemavu, kuruhusiwa kuomba mikopo hata mmoja mmoja kulionekana kuongeza
fursa za kunufaika. Hata hivyo, baadhi yao wanaona bado kuna masharti
yanayowazuia.
Kassimu Mohamed, mkazi wa Mahonda mwenye ulemavu wa viungo, anasema anatamani kupata mtaji wa kuanzisha biashara lakini anakwama kutokana na sharti la kuwa tayari ana biashara kabla ya kupata mkopo.
"Nitaanzaje
biashara wakati sina mtaji wala ajira? Kama kweli lengo ni kutuwezesha
kiuchumi, basi tupewe mtaji pamoja na mafunzo ili nasi tuweze kujenga maisha
yetu na familia zetu," anasema.
Kauli yake inaibua mjadala kuhusu iwapo masharti yaliyopo yanawafikia walengwa waliokusudiwa. Kwa baadhi yao, uwezeshaji wa kweli unapaswa kuanza kwa kuwasaidia wale wasio na mtaji wa kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Vijana nao wanasubiri
Changamoto
zinazowakabili wanawake na watu wenye ulemavu zinaonekana pia kwa vijana.
Omar Nassor
anasema kikundi chao kilikamilisha taratibu zote za maombi, lakini hadi sasa
hakijapatiwa mkopo wala maelezo yanayowapa uhakika wa lini watanufaika.
Anasema
katika mazingira ambayo Serikali haiwezi kuwaajiri wananchi wote, mikopo ya
asilimia 10 inapaswa kuwa fursa ya kuwasaidia vijana kujiajiri badala ya
kuendelea kusubiri ajira rasmi.
"Tuko
tayari kufanya biashara na kujikwamua kiuchumi, lakini kila tunapofuatilia
tunaambiwa tuendelee kusubiri kwa sababu mifumo haijakaa sawa. Hali hii
inatukatisha tamaa kwa sababu hatuna uhakika wa lini tutapata mkopo,"
anasema.
Kauli yake inaonyesha kuwa changamoto kubwa si ukosefu wa nia ya kufanya kazi, bali kutokuwa na uhakika wa lini ahadi ya uwezeshaji itageuka kuwa fursa halisi.
Majibu ya
Mamlaka: Utekelezaji unaendelea
Malalamiko ya wananchi yanapowasilishwa kwa mamlaka, picha inayojitokeza ni kwamba mpango wa mikopo unaendelea kutekelezwa na tayari umewanufaisha baadhi ya walengwa.
Afisa
Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Kaskazini 'B', Jina Mohamed Haji, anasema tangu
mwaka 2022 hadi sasa vikundi 35 vimepatiwa mikopo. Kati ya hivyo, 27 ni vya
wanawake, sita vya vijana na viwili vya watu wenye ulemavu.
Anasema pia
Halmashauri imewasilisha zaidi ya shilingi milioni 952 kwa Wakala wa Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) kufikia Machi 31 mwaka huu kwa ajili ya
kutekeleza mpango huo.
Hata hivyo,
anakiri kuwa baadhi ya changamoto zimejitokeza, hususan katika mifumo ya benki
inayotumika kusimamia marejesho ya mikopo. Kwa mujibu wake, hali hiyo
imechangia baadhi ya malalamiko kutoka kwa wanufaika na waombaji.
Kutokana na changamoto hizo, anashauri kuendelea kuboresha mfumo wa usajili na utoaji wa huduma ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo na kuongeza ufanisi wa programu.
ZEEA yatoa taswira ya mafanikio
Kwa upande
wake, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA na Uhusiano wa ZEEA, Gharib Said Gharib,
anasema mamlaka hiyo ilianzishwa kuratibu programu za uwezeshaji wananchi
kiuchumi kupitia mafunzo na mikopo.
Anasema
hadi sasa ZEEA imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 53.9
kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji.
Kwa mujibu
wake, tangu mwaka 2024 kupitia mfumo wa 4-4-2, vikundi 20 vya vijana vimepatiwa
mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 220, vikundi 55 vya wanawake zaidi ya
shilingi milioni 334.6 na vikundi 12 vya watu wenye ulemavu zaidi ya shilingi
milioni 49.2.
Anasema
takwimu hizo zinaonyesha kuwa mpango huo unaendelea kuwafikia walengwa na una
uwezo mkubwa wa kubadili maisha ya wananchi endapo utasimamiwa kwa ufanisi na
kuwafikia wahitaji kwa wakati.
Pamoja na mafanikio hayo, anakiri kuwa changamoto kubwa inayoikabili programu ni urejeshaji wa mikopo. Hata hivyo, anasema tathmini ya mwaka 2024 ilibaini kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wanufaika wa programu ya Inuka wamefanikiwa kuzalisha ajira.
Tatizo haliko
kwenye sheria
Kwa mujibu
wa mtaalamu wa sheria kutoka Zanzibar, Almass Mohamed, changamoto kubwa haipo
katika uwepo wa sheria, bali katika utekelezaji wake.
Anasema
sheria zilizopo zimeweka msingi mzuri wa kuwawezesha wanawake, vijana na watu
wenye ulemavu, lakini mafanikio ya programu yatategemea uwazi, usawa na
uwajibikaji wa taasisi zinazozisimamia.
Kwa mtazamo
wake, wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi kuhusu masharti, vigezo vya
kupata mikopo na hatua za maombi yao ili kuondoa sintofahamu inayojitokeza.
"Serikali,
halmashauri, ZEEA na wadau wote wana wajibu wa kuhakikisha mikopo ya asilimia
10 inawafikia walengwa na kutimiza lengo la kuwawezesha wanawake, vijana na
watu wenye ulemavu kujenga uchumi imara na kuchangia maendeleo ya
Zanzibar," anasema.
Kauli hiyo inaonyesha kuwa mafanikio ya mpango huu hayatategemea tu kiasi cha fedha kinachotengwa, bali pia namna taasisi zinavyowajibika katika kusimamia utoaji wake na kuwafikia walengwa kwa wakati.
Uwazi utaongeza
imani ya wananchi
Simulizi za
Khadija Abdalla, Kassimu Mohamed na Omar Nassor zinaonyesha matarajio makubwa
ambayo wananchi wameyaweka kwenye mikopo ya asilimia 10. Kwao, mpango huu ni
fursa ya kujenga maisha bora kupitia ujasiriamali na shughuli nyingine za
uzalishaji mali.
Kwa upande
mwingine, takwimu zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini 'B' pamoja
na ZEEA zinaonyesha kuwa tayari makundi kadhaa yamenufaika na mpango huo. Hata
hivyo, malalamiko ya baadhi ya waombaji yanaonyesha kuwa bado kuna haja ya
kuimarisha utoaji wa taarifa, kurahisisha mifumo ya maombi na kuhakikisha
waombaji wanapata mrejesho wa wakati kuhusu hatua za maombi yao.
Kuboresha
maeneo hayo kutasaidia kujenga imani ya wananchi kwa programu na kupunguza
sintofahamu kuhusu namna mikopo inavyotolewa.
Uwajibikaji
ndiyo kipimo cha mafanikio
Mikopo ya
asilimia 10 ni fursa muhimu ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye
ulemavu kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa Zanzibar. Uwepo wa
sheria, taasisi na fedha ni msingi muhimu, lakini mafanikio yake yatapimwa kwa
uwezo wa mfumo kuwafikia walengwa kwa haki, uwazi na kwa wakati.
Wananchi
wanahitaji kuona kuwa taratibu zilizowekwa zinafanya kazi kwa ufanisi, maombi
yao yanapatiwa majibu kwa wakati na changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa
uwazi. Hivyo ndivyo imani kwa programu itaongezeka na lengo la kupunguza
umaskini kupitia uwezeshaji wa kiuchumi litafikiwa.
Kwa
kuendelea kuboresha mawasiliano, kurahisisha mifumo ya maombi na kuimarisha
uwajibikaji wa taasisi zinazosimamia mpango huu, mikopo ya asilimia 10 inaweza
kuendelea kuwa chachu ya maendeleo jumuishi na kuwasaidia wananchi wengi zaidi
kujenga uchumi imara na maisha yenye tija Zanzibar.


Post a Comment