MIKOPO YA ASILIMIA 10 YAWANUFAISHA WACHACHE,
Na Maryam Nassor
Kwa zaidi ya miaka miwili, Semeni Bundala ameendelea kufika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini 'B' akiwa na matumaini ya kupata mkopo wa asilimia 10 uliotengwa kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi.
Kila
safari anarudi na majibu yale yale.
"Tumekuwa
tukifuatilia mikopo hii kwa muda mrefu bila mafanikio. Kila tunapofika
Halmashauri tunaelekezwa kujisajili kwenye mifumo mbalimbali. Hadi leo hatujui
tatizo ni nini," anasema.
Semeni si peke yake,
Malalamiko kama yake yanaendelea kusikika kutoka kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Kaskazini 'B', hali inayoibua maswali kuhusu uwazi, usawa na uwajibikaji katika utekelezaji wa mfumo wa mikopo ya asilimia 10 unaotekelezwa kwa utaratibu wa 4-4-2.
Sheria
ipo, lakini walengwa bado wanalalamika
Kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria Na. 9 ya Mwaka 2023, Serikali za Mitaa zina wajibu wa kuweka mazingira ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mipango mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, Kifungu cha 9 cha Sheria Na. 2 ya Mwaka 2022 kinaipa Mamlaka ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) jukumu la kusimamia na kuratibu programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayogawanywa kwa mfumo wa asilimia 4 kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.
Sheria hizo zilitungwa kuongeza fursa za kiuchumi, kukuza ajira na kuinua kipato cha wananchi.
Kwa mujibu wa miongozo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kila halmashauri inapaswa kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo hiyo.
Lakini uchunguzi huu unaonesha kuwa utekelezaji wake bado unaibua maswali.
Walengwa
wanasema hawafikii fursa
Semeni anasema kikundi chake kilitimiza masharti yote, ikiwemo kuwa na wanachama saba, kusajili kikundi na kuwa na vitambulisho vinavyotakiwa.
Hata hivyo, hadi sasa hakijapata mkopo.
Anasema katika Shehia ya Mahonda pekee kuna zaidi ya vikundi 24 vilivyosajiliwa, lakini bado havijapata mikopo.
Kwa
upande wake, Fatma Said, mkazi wa Mahonda mwenye ulemavu wa viungo, anasema
fedha zinazotengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu haziwafikii walengwa kama
ilivyokusudiwa.
Kwa mujibu wake, utekelezaji wa mgawanyo wa 4-4-2 hauonekani kufanyika kikamilifu, jambo linalowafanya watu wenye ulemavu kushindwa kupata asilimia mbili iliyotengwa kwa mujibu wa mfumo huo.
"Kutokupata mikopo hii kunaturudisha nyuma kiuchumi. Wengi wetu hatuna ajira na tulitegemea mikopo hii kuanzisha au kukuza shughuli za kujiongezea kipato," anasema.
Changamoto kama hiyo pia inamkumba Khatib Mohamed, Katibu wa Kikundi cha Vijana.
Anasema amekuwa akifuatilia mkopo huo kwa muda mrefu bila mafanikio, huku akielekezwa mara kwa mara kujisajili katika mifumo mbalimbali.
"Biashara yangu ya ufugaji wa kuku ilikufa kutokana na kukosa mtaji. Nilitegemea mkopo huu kuikuza biashara yangu, lakini kutokana na kuchelewa kuupata nimeendelea kuwa katika hali ngumu ya kiuchumi," anasema.
Kauli za wananchi hawa zinaibua maswali kuhusu uwazi wa mfumo wa usajili, ufanisi wa mchakato wa utoaji wa mikopo na kiwango cha uwajibikaji wa taasisi zinazosimamia mpango huo.
Halmashauri
yajibu tuhuma
Akijibu malalamiko hayo, Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Kaskazini 'B', Jina Mohamed Haji, anasema kuanzia mwaka 2022 hadi sasa vikundi 35 tayari vimepata mikopo.
Kati ya hivyo, vikundi 27 ni vya wanawake, sita vya vijana na viwili vya watu wenye ulemavu.
Anasema Halmashauri imewasilisha ZEEA zaidi ya shilingi milioni 952 kufikia Machi 31 mwaka huu.
Anaongeza kuwa tangu kuanza kwa mfumo wa kidijitali, vikundi sita tayari vimesajiliwa na vinasubiri kupatiwa mikopo baada ya maombi yao kuwasilishwa ZEEA kwa ajili ya uchambuzi.
Pia anakiri kuwa changamoto za mifumo ya benki zimechangia malalamiko ya baadhi ya wanufaika kuhusu marejesho ya mikopo na kuiomba ZEEA kuboresha mfumo wa usajili ili kuondoa changamoto zinazowakabili waombaji.
ZEEA
yaeleza mafanikio
Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA na Uhusiano wa ZEEA, Gharib Said Gharib, anasema mamlaka hiyo ilianzishwa kwa Sheria Na. 2 ya Mwaka 2022 kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mafunzo na mikopo.
Anasema hadi sasa taasisi hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 53.9 kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji.
Kwa mujibu wake, tangu mwaka 2024 kupitia mfumo wa 4-4-2, vikundi 20 vya vijana vimepatiwa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 220, vikundi 55 vya wanawake vimepata zaidi ya shilingi milioni 334.6, huku vikundi 12 vya watu wenye ulemavu vikipata zaidi ya shilingi milioni 49.2.
Anasema changamoto kubwa inayoiikabili ZEEA ni urejeshaji wa mikopo.
Hata hivyo, tathmini ya mwaka 2024 ilibaini kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wanufaika wa programu ya Inuka wamefanikiwa kuzalisha ajira.
Aidha, mamlaka hiyo imeondoa sharti lililowataka watu wenye ulemavu kukopa kupitia vikundi pekee na sasa wanaweza pia kukopa mmoja mmoja ili kuongeza fursa za kunufaika.
Tatizo
liko kwenye utekelezaji?
Mtaalamu wa masuala ya sheria Zanzibar, Almass Mohamed, anasema changamoto kubwa si ukosefu wa sheria bali ni utekelezaji wake.
Anaeleza kuwa Sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imeweka wajibu wa kuhakikisha fedha zinazotengwa zinawafikia walengwa kwa misingi ya usawa, uwazi na uwajibikaji.
"Endapo wananchi wanaendelea kulalamikia kutopata mikopo licha ya kutimiza masharti yaliyowekwa, ni dalili kwamba kuna mapungufu katika utekelezaji wa sheria, usimamizi wa mifumo au utoaji wa taarifa kwa umma."
Anasisitiza kuwa mfumo wa mikopo ya asilimia 10 unaotekelezwa kwa utaratibu wa 4-4-2 unapaswa kuzingatia haki, uwazi na usawa ili makundi yaliyokusudiwa yaweze kunufaika.
Pengo
kati ya takwimu na uhalisia
Uchunguzi huu unaonesha kuwa pamoja na kuwepo kwa sheria, sera na fedha za uwezeshaji wananchi kiuchumi, bado kuna wananchi wanaodai kutonufaika na mfumo huo licha ya kutimiza masharti yaliyowekwa.
Wakati Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini 'B' na ZEEA zikieleza mafanikio ya utoaji wa mikopo, ushahidi kutoka kwa baadhi ya walengwa unaonesha kuwepo kwa pengo kati ya takwimu zinazotolewa na taasisi hizo na hali wanayoikabili wananchi wanaosubiri kunufaika.
Bila
kuimarisha uwazi katika mchakato wa utoaji wa mikopo, kuboresha mifumo ya
usajili na kuongeza uwajibikaji wa taasisi husika, lengo la mfumo wa asilimia
10 wa kuwawezesha wananchi kiuchumi linaweza kuendelea kubaki kwenye maandishi
ya sheria kuliko kuonekana katika maisha ya wananchi.


Post a Comment