MIAKA 30 YA MCT: VIONGOZI WA VYOMBO VYA HABARI WATAFAKARI MUSTAKABALI WA TASNIA KATIKA ENZI YA KIDIJITALI

Na Maryam Nassor

MOROGORO: Baada ya miaka 30 ya mfumo wa kujisimamia kwa sekta ya habari nchini Tanzania, viongozi wa vyombo vya habari wamekutana mkoani Morogoro kufanya tathmini ya mafanikio yaliyopatikana, changamoto zinazoikabili tasnia hiyo na mikakati ya kujenga mustakabali imara wa uandishi wa habari unaoendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya jamii.

Akifungua mkutano wa siku mbili wa mashauriano kati ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) na viongozi wa vyombo vya habari unaofanyika Julai 16–17, 2026 huko hotel ya Antique Legacy Morogoro, Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura, alisema mfumo wa kujisimamia umeiwezesha sekta ya habari kuimarisha maadili, kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kujenga utamaduni wa uwajibikaji bila kutegemea mifumo ya adhabu ya mahakama.
Alisema katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, MCT imekuwa mstari wa mbele katika kutatua migogoro kati ya vyombo vya habari na wananchi kupitia usuluhishi, imeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari, kushiriki katika uchechemuzi wa sera na sheria mbalimbali zinazohusu tasnia pamoja na kuandaa Kanuni za Maadili ya Uandishi wa Habari zinazotumika nchini.

"Mfumo wa kujisimamia umeifanya Tanzania kutambulika kimataifa kama moja ya nchi zinazotekeleza usimamizi wa kitaaluma wa vyombo vya Habari, Haya ni mafanikio makubwa ambayo yanapaswa kulindwa na kuendelezwa," alisema Sungura.

Hata hivyo, alisema tasnia hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji hatua za pamoja kutoka kwa wadau wote.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni kudhoofika kwa mshikamano wa sekta hiyo, kuyumba kwa uchumi wa vyombo vya habari, changamoto zinazoendelea kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, kupungua kwa imani ya wananchi kwa vyombo vya habari pamoja na kuongezeka kwa hofu kuhusu usalama wa wanahabari wanapotekeleza majukumu yao.

Kwa mujibu wa Sungura, mabadiliko ya teknolojia, hususan matumizi ya akili unde (Artificial Intelligence - AI), yameleta fursa mpya lakini pia yameongeza ushindani mkubwa katika uzalishaji na usambazaji wa habari.

Alisema ili sekta iweze kuendelea kuwa imara, kuna haja ya kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa kusaidia maendeleo ya vyombo vya habari pamoja na kufanya marekebisho ya sera na sheria ili maamuzi yanayotolewa na MCT yatambuliwe zaidi kisheria.
Aidha, aliwataka wamiliki wa vyombo vya habari kubadili mifumo yao ya biashara kwa kuwekeza katika huduma za kidijitali, uzalishaji wa maudhui maalumu, huduma za data na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea matangazo pekee.

Tasnia ibadili mbinu za kufikia hadhira

Mhariri na mwanzilishi wa Malunde Media, Kadama Malunde, alisema mkutano huo umetoa nafasi muhimu kwa viongozi wa vyombo vya habari kutafakari mwelekeo mpya wa tasnia katika kipindi ambacho teknolojia imebadili namna wananchi wanavyopokea habari.

Alisema changamoto kubwa kwa sasa siyo tu ushindani wa kidijitali, bali ni namna vyombo vya habari vitakavyoweza kujenga uaminifu kwa wasomaji na watazamaji.

"Leo kila mtu anaweza kuchapisha taarifa kupitia simu yake, kinachotutofautisha sisi wanahabari ni weledi, uhakiki wa taarifa na maadili. tukiyaacha hayo, tutapoteza nafasi yetu katika jamii," alisema Malunde.

Aliongeza kuwa, vyombo vya habari vinapaswa kuwekeza zaidi katika ubunifu wa maudhui ya kidijitali, matumizi sahihi ya akili unde na mifumo ya mapato inayoweza kuviwezesha kuendelea kufanya kazi kwa kujitegemea.

Maadili ndiyo msingi wa kurejesha imani ya umma

Naye mshiriki wa mkutano huo, Saada Amir kutoka Mwananchi Communication, alisema moja ya maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele ni kujenga upya imani ya wananchi kwa vyombo vya habari kupitia uandishi unaozingatia ukweli, uwazi na uwajibikaji.
Alisema, katika kipindi ambacho taarifa nyingi zisizo sahihi zinasambaa kupitia mitandao ya kijamii, wananchi wanahitaji vyombo vya habari vinavyotoa taarifa zilizofanyiwa uhakiki na zinazozingatia maadili ya taaluma.

"Tunapaswa kuhakikisha kila habari tunayochapisha inaleta thamani kwa jamii, Uaminifu ndio mtaji mkubwa wa chombo cha habari katika dunia ya sasa ya kidijitali," alisema Saada Amir.

Aliongeza kuwa, mafunzo endelevu kwa wahariri na waandishi wa habari yataendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuhakikisha tasnia inaendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia bila kupoteza misingi ya taaluma.

Mustakabali wa tasnia

Kwa upande wake , Mratibu wa MCT Zanzibar Ziada Kilobo amesema kuwa mafanikio ya miaka 30 ya mfumo wa kujisimamia yanapaswa kuwa msingi wa kujenga tasnia yenye uchumi imara, uhuru wa kitaaluma na uwezo wa kukabiliana na changamoto mpya zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.
Amesisitiza kuwa, ushirikiano kati ya MCT, vyombo vya habari, serikali, washirika wa maendeleo na wananchi utakuwa muhimu katika kuhakikisha tasnia ya habari inaendelea kuwa nguzo ya uwajibikaji, demokrasia na maendeleo ya Taifa.

Mkutano huo umeandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na taasisi ya VIKES – Finnish Foundation for Media and Development, ukiwakutanisha viongozi 21 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kujadili changamoto na fursa zinazoikabili tasnia katika kipindi hiki cha mageuzi ya kidijitali.

No comments

Powered by Blogger.