WATU WENYE ULEMAVU WAACHANA NA UTEGEMEZI WA MISAADA

 

Waamini Uwezeshaji  kiuchumi: Ndiyo njia bora ya kuondokana  na utegemezi wa kipato.

Na Maryam Nassor

Kwa miaka mingi, watu wenye ulemavu wamekuwa wakipokea misaada mbalimbali, ikiwemo vyakula, nguo, vifaa vya matumizi ya kila siku na fedha kutoka kwa taasisi za kijamii, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na watu binafsi.

 Ingawa misaada hiyo imekuwa muhimu katika kukidhi mahitaji ya msingi ya kila siku, wataalamu wa maendeleo ya jamii wanaeleza kuwa utegemezi wa misaada pekee hauwezi kuwa suluhisho la kudumu la kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu.

Wanaamini kuwa uwezeshaji wa kiuchumi, elimu na upatikanaji wa ujuzi wa kujitegemea ndiyo njia bora zaidi ya kuwainua na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

Zanzibar, yenye wakazi zaidi ya milioni 1.8 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, inakadiriwa kuwa na watu wenye ulemavu wanaofikia asilimia 11.4 ya idadi ya watu wake. Hata hivyo, pamoja na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, baadhi yao wamefanikiwa kuvuka vikwazo na kujenga maisha ya kujitegemea. 

Akizungumza na mwandishi wa makala hii, Awena Hassan, mkazi wa Kitope mkoani wa Kaskazini Unguja ambaye ni mtu mwenye ulemavu wa kuona, anasema alizaliwa akiwa haoni, lakini hakukata tamaa katika safari yake ya kutafuta  elimu.

Anasema alisoma kwa bidii hadi kufanikiwa kupata diploma ya elimu, na sasa ni mwalimu wa watoto wasioona katika Skuli ya Kisiwandui, Unguja.

“Niliamini kuwa watu wenye ulemavu wana uwezo sawa na wengine. Changamoto tulizonazo hazipaswi kutuzuia kufikia malengo yetu,” anasema Awena.

Anaongeza kuwa ni wakati wa watu wenye ulemavu kujiamini, kutumia vipaji na uwezo wao, na kutimiza ndoto zao badala ya kusubiri misaada ya chakula au fedha kama suluhisho la changamoto za maisha.

“Kuna watu wengi wenye ulemavu ambao leo ni wafanyabiashara wakubwa, viongozi na wataalamu katika sekta mbalimbali. Hii inaonesha kuwa ulemavu si kikwazo cha mafanikio endapo mtu atapata fursa na kuwa tayari kuitumia,” anasisitiza.

Kwa upande wake, Mohamed Hassan Suleiman, mwenye ulemavu wa viungo, anasema baadhi ya watu wenye ulemavu bado wanaamini kuwa wao ni wa kupokea misaada pekee kutokana na mtazamo uliopo katika jamii.

“Watu wengi wamezoea kuwaona watu wenye ulemavu kama watu wa kusaidiwa tu. Hata sisi wenyewe wakati mwingine tunakubali hali hiyo. Tunapaswa kubadili fikra na kuamini kuwa tunaweza kufanya kazi na kuzalisha kama wengine,” anasema. 

Mohamed anasema kuwa baada ya kupata elimu ya ujasiriamali, mtazamo wake ulibadilika na kugundua kuwa watu wenye ulemavu wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kujipatia kipato.

“Nilikuwa nikisubiri watu waniletee chakula au fedha za matumizi ya nyumbani. Lakini niligundua kuwa misaada huisha haraka na maisha hubaki yaleyale. Nilipopewa mafunzo ya utengenezaji wa sabuni ndipo nilipoanza kupata kipato, na sasa najitegemea kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Naye Fatma Khamis Abdalla, anayejishughulisha na biashara ndogo ndogo pamoja na ufugaji wa kuku, anasema uwezeshaji wa kiuchumi huwapa watu wenye ulemavu heshima, kujiamini na kuwaondolea utegemezi.

“Mwanzoni nilikuwa nasubiri kusaidiwa kila mara. Lakini nilipoanza ufugaji mdogo, niligundua kuwa ninaweza kupata kipato na kusaidia familia yangu. Leo ninawashauri wenzangu kutafuta njia za kujiongezea kipato badala ya kusubiri misaada pekee,” anasema.

Fatma anafafanua kuwa misaada ya matumizi ya muda mfupi haiwezi kulinganishwa na uwekezaji wa muda mrefu katika uwezo wa mtu.

“Nikipewa pishi la mchele nitalitumia kwa muda mfupi tu. Lakini nikipewa mtaji wa biashara au mafunzo ya ujasiriamali, ninaweza kujenga maisha yangu kwa muda mrefu zaidi,” anasema.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Sabah Mohamed, anasema changamoto kubwa inayowakabili baadhi ya watu wenye ulemavu ni mtazamo wa kutegemea misaada badala ya kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo. 

Anasema jumuiya hiyo imekuwa ikitoa elimu na kuwahamasisha watu wenye ulemavu kuondokana na fikra za utegemezi na badala yake kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali. 

“Tunawahamasisha watu wenye ulemavu kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali, kupata mafunzo ya stadi za maisha na kutumia mikopo inayopatikana kupitia programu mbalimbali za maendeleo,” anasema.

Naye Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Mradi wa Uwezeshaji wa Haki za Binadamu na Utawala Bora Awamu ya Tano unaotekelezwa na Kanisa Katoliki Kanda ya Zanzibar, Msafiri Thomas, anasema mradi huo umejikita katika kuwawezesha watu wenye ulemavu pamoja na wanaoishi katika mazingira magumu.

Anasema wameandaa mkakati wa kuwawezesha watoto wenye ulemavu mashuleni kwa kuwapatia vifaa vya kujifunzia pamoja na kuanzisha vikoba vya kuweka na kukopa kwa familia zenye watoto wenye ulemavu ili kuimarisha hali zao za kiuchumi.

“Lengo ni kusaidia familia hizi kujiongezea kipato na kuondokana na utegemezi wa misaada, huku watoto wenye ulemavu wakipata mazingira bora ya kujifunzia na kutimiza ndoto zao,” anasema.

Kwa upande wa Serikali, jitihada mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Serikali imeendelea kusisitiza ushirikishwaji wao katika mipango ya maendeleo pamoja na kuwapatia fursa za mafunzo ya ufundi, ajira na mikopo.

Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja, Jina Mohamed Haji, anasema serikali inaamini kuwa uwezeshaji wa kiuchumi ndiyo njia bora ya kupunguza umaskini miongoni mwa watu wenye ulemavu.

Anasema kupitia halmashauri, mikopo ya asilimia 10 imekuwa ikitolewa kwa makundi maalumu, ambapo asilimia 4 hutengwa kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu. Hata hivyo, kwa mwaka 2026, ni vikundi viwili pekee vya watu wenye ulemavu vilivyofanikiwa kupata mikopo hiyo.

“Lengo letu ni kuona watu wenye ulemavu wanapata fursa sawa za elimu, ajira na ujasiriamali ili waweze kujitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa kama wananchi wengine,” anasema.

No comments

Powered by Blogger.