UTAWALA BORA NGUZO YA UPATIKANAJI WA HAKI KATIKA JAMII
Viongozi wa Mahkama wawasihi wananchi, kushirikiana katika kutoa Ushahidi ili haki ipatikane.
Na Maryam Nassor
Katika jamii yoyote
inayoheshimu sheria, haki na usawa, utawala bora ni msingi muhimu unaowezesha
wananchi kupata haki zao kwa wakati na kwa usawa.
Utawala bora hujengwa kupitia uwajibikaji wa
viongozi, ushirikishwaji wa wananchi, uwazi katika maamuzi pamoja na utendaji
unaozingatia sheria.
Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, katika Ibara ya 13, inaeleza kuwa watu wote
ni sawa mbele ya sheria na wana haki ya kulindwa kwa usawa na sheria. Aidha,
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inasisitiza umuhimu wa kulindwa kwa haki za
msingi za binadamu na kuimarishwa kwa utawala unaozingatia sheria.
Licha ya kuwepo kwa
sheria na katiba hizo, bado wananchi wengi wa vijijini hukumbana na migogoro ya
kifamilia, migogoro ya ardhi, ukatili wa kijinsia na changamoto nyingine
zinazohitaji msaada wa viongozi wa shehia, wasaidizi wa sheria, Jeshi la Polisi
na Mahakama ili kupata haki zao.
Akizungumza na mwandishi
wa makala hii, Fatma Ali, mkaazi wa Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja,
anasema msaada wa viongozi wa shehia ulimwezesha kupata haki baada ya mgogoro
wa muda mrefu wa mipaka ya kiwanja chake kati yake na jirani yake.
Anasema ,mgogoro huo
ulidumu kwa zaidi ya mwaka mmoja na kusababisha ugomvi mkubwa kati ya familia
hizo mbili.
“Tulikuwa hatusemezani
kabisa ,Kila mmoja alidai eneo hilo ni lake Tulipofika kwa Sheha alituita pande zote
mbili, akatusikiliza na kutushauri kufuata taratibu za kisheria. Mwisho wa siku
tulipata suluhu na sasa tunaendelea vizuri,” anasema Fatma.
Anaeleza kuwa, kama
kusingekuwa na usimamizi mzuri wa viongozi wa shehia, mgogoro huo ungeweza
kusababisha vurugu kubwa katika eneo lao.
Mbali na viongozi wa
shehia, wasaidizi wa sheria wameendelea kuwa msaada mkubwa kwa wananchi
wanaohitaji mwongozo wa kisheria.
Khamis Maalim kutoka Mkoa
wa Kaskazini Unguja, anasema alipata msaada wa kisheria baada ya kunyimwa haki
ya urithi wa mali za familia kwa madai kuwa yeye ni mlemavu.
“Nilikuwa sifahamu
nifanye nini baada ya ndugu zangu kunitenga katika mgawanyo wa mali. Kupitia
msaidizi wa sheria nilielekezwa taratibu za kufuata na nikapata nafasi ya
kusikilizwa. Leo nimepata sehemu yangu ya urithi kwa mujibu wa sheria,” anasema
Khamis.
Anasema, elimu ya sheria
inayotolewa kwa wananchi imekuwa msaada mkubwa kwa watu wengi ambao awali
hawakujua namna ya kudai haki zao.
Katika masuala ya ukatili
wa kijinsia, Jeshi la Polisi limeendelea kuwa nguzo muhimu katika kulinda haki
za waathirika. Kupitia Dawati la Jinsia na Watoto, waathirika wa vitendo vya
ukatili hupata fursa ya kuripoti matukio yao na kufanyiwa uchunguzi kwa mujibu
wa sheria.
Mwanamke mmoja aliyeomba
kutotajwa jina lake kutokana na unyeti wa tukio lake, anasema alipata haki
baada ya kuripoti tukio la ubakaji katika Kituo cha Polisi Mahonda.
“Nilikuwa naogopa kutoa
taarifa kwa sababu nilihisi sitaaminiwa. Lakini nilipofika Polisi nilisikilizwa
na kupewa msaada. Uchunguzi ulifanyika na kesi ikapelekwa Mahakamani. Hilo
lilinipa matumaini kuwa sheria ipo kwa ajili ya kulinda haki zetu,” anasema.
Anaeleza kuwa, hatua ya
kuripoti tukio hilo ilimsaidia yeye pamoja na waathirika wengine kupata ujasiri
wa kusimama na kudai haki zao.
Kwa upande wake, Hakimu
wa Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, Lusiano Makoe Nyengo, anasema Mahakama
zimeendelea kuwa sehemu muhimu katika utoaji wa haki kwa wananchi, ambapo
migogoro mbalimbali ya kijamii hupatiwa ufumbuzi kwa kuzingatia sheria na ushahidi
uliopo.
“Ni vyema wananchi
kushirikiana na Mahakama katika kutoa ushahidi pale wanapoleta kesi zao
mahakamani, kwani bila ya ushirikiano ni vigumu kesi kuendelea kusikilizwa na
hatimaye kupata hukumu stahiki,” anasema Lusiano.
Naye Msaidizi wa Sheria
kutoka Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, Shabani Sariboko Makarani, anaeleza kuwa
ushirikiano kati ya viongozi wa shehia, wasaidizi wa sheria, Polisi, Mahakama
na wananchi ni muhimu katika kujenga jamii inayoheshimu sheria na kuzingatia
misingi ya utawala bora.
Hata hivyo, amesema ukosefu wa
utawala bora unaweza kusababisha madhara makubwa katika jamii. Miongoni mwa
madhara hayo ni kuongezeka kwa migogoro, rushwa, ubaguzi, ukiukwaji wa haki za
binadamu na kupungua kwa imani ya wananchi kwa taasisi za umma.
“Pale ambapo viongozi
hawawajibiki ipasavyo au sheria hazitekelezwi kwa usawa, wananchi wengi
hujikuta wakikosa haki zao. Hali hiyo inaweza kusababisha baadhi ya watu
kujichukulia sheria mkononi, jambo ambalo huathiri amani na mshikamano wa
jamii,” anasema.
Aidha, anasema ukosefu wa
utawala bora unaweza kuwafanya waathirika wa vitendo vya ubakaji, ukatili wa
kijinsia na migogoro mingine kushindwa kupata haki kwa wakati. Matokeo yake ni
kuongezeka kwa maumivu kwa waathirika na kuendelea kwa vitendo vya uvunjifu wa
sheria katika jamii.
Mchambuzi wa masuala ya
utawala bora, Almass Mohamed, anasema kuimarisha elimu ya sheria kwa wananchi,
kuongeza uwajibikaji wa viongozi na kuimarisha utendaji wa vyombo vya haki
kutasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi.
Anasema ,wananchi nao
wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda utawala bora kwa kutoa taarifa za
vitendo vya uhalifu, kuheshimu sheria na kushirikiana na viongozi pamoja na
vyombo vya dola katika kutatua changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao.
Naye, Afisa
Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Mradi wa
Uwezeshaji wa haki za kibinadamu na
Utawala bora kutoka kanisa katoliki Msafiri Thomas, amesema wamechagua Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja
kutekeleza mradi huo kwa sababu
wamegundua uwelewa wa wananchi bado ni mdogo
wananchi wengi hawajui haki zao .
Amesema,
katika tathimini ya awali waliyoifanya wamegundua kuwa maswali ya haki za
binadamu na utawala bora kwa wananchi wa wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja uwelewa wao uko chini kabisa.
“Upatikanaji wa haki katika jamii unategemea uwepo wa utawala bora unaohusisha ushirikiano kati ya wananchi na taasisi zote zinazosimamia sheria, ambapo misingi ya utawala bora inazingatiwa, wananchi hupata fursa ya kusikilizwa, kulindwa na kutendewa haki bila ubaguzi, jambo linalochangia kudumisha amani, maendeleo na mshikamano wa jamii” Amesisitiza .
MWISHO
Post a Comment