VIONGOZI WANAWAKE WATAKIWA KUWA NA MSHIKAMANO KUPANUA FURSA ZA UONGOZI
Na Maryam Nassor
VIONGOZI wanawake walio katika nafasi mbalimbali za uongozi wametakiwa
kuweka mshikamano na kushirikiana bila kujali tofauti za vyama vyao vya siasa
ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi nchini.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Nairat Abdullah, wakati akifungua
mafunzo ya siku mbili kwa madiwani wanawake na waratibu wa shehia yaliyofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Chama hicho Tunguu Unguja.
Mkurugenzi Nairat amesema, licha
ya hatua zinazopigwa katika kuwawezesha wanawake, bado uwakilishi wao katika
nafasi za uongozi ni mdogo, ukifikia asilimia 24 pekee, hali inayohitaji
mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wanawake ili kuongeza idadi hiyo.
“Ni lazima tushirikiane kwa pamoja ili wanawake wengi zaidi wapate nafasi
za uongozi bila kujali anatoka chama gani, Lengo letu ni kuona wanawake
wakiongeza uwakilishi wetu katika ngazi zote za maamuzi,” amesema.
Amesema kuwa, wanawake waliopo
katika nafasi za udiwani wanapaswa kujiandaa kugombea nafasi za juu zaidi,
ikiwemo Ubunge na Uwakilishi katika uchaguzi wa mwaka 2026, akieleza kuwa hilo
linawezekana endapo watajengewa uwezo na kujiamini.
Aidha, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo viongozi hao ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi, kuongeza kujiamini na kuwa viongozi wanaokubalika na jamii kwa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dk Imane Duwe, amesema kiongozi
bora ni mtumishi wa wananchi na si mtawala, hivyo viongozi wanawake wanapaswa
kuweka mbele maslahi ya wananchi wanaowaongoza.
Aidha amesisitiza, umuhimu wa
viongozi wanawake kuzingatia maadili na kuvaa mavazi ya staha, akieleza kuwa
wao ni kioo cha wanawake wengine wanaotarajia kuingia katika nafasi za uongozi.
“Sisi wanawake tunapaswa kuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa mwenendo na
mavazi yetu, kwa sababu tunawawakilisha wanawake wengi ambao bado hawajapata
nafasi za uongozi,” amesema.
Naye, Diwani wa Wadi ya Mwanakwerekwe, Fatma Juma Jabu, amesema mafunzo hayo yatamuwezesha kuboresha huduma kwa wananchi wa wadi yake na kuahidi kuendelea kuwahudumia kwa uadilifu, uwazi na bila upendeleo.
Ameipongeza TAMWA ZNZ, kwa kuendelea kuwawezesha wanawake kupitia mafunzo
mbalimbali yanayowaandaa kushika nafasi za uongozi, akisema wanawake wengi
wamefanikiwa kutimiza ndoto zao kutokana na programu hizo.
Kwa upande wake, Diwani wa Wadi ya Kihinani, Bahati Ali Rashid, amesema
mafunzo aliyoyapata kupitia TAMWA ZNZ mwaka uliopita yamechangia mafanikio yake
ya kisiasa na kumwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Ameiomba ,TAMWA ZNZ kuendelea kuandaa mafunzo kama hayo ili kuwajengea
uwezo viongozi wanawake zaidi na kuongeza ushiriki wao katika uongozi.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na TAMWA ZNZ na yamewakutanisha madiwani wanawake kutoka wadi mbalimbali za Unguja pamoja na waratibu wa shehia, yakilenga kuimarisha uwezo wao wa uongozi, uwajibikaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Post a Comment