MAZINGIRA MAGUMU YANAVYOWANYIMA WATOTO WA KIKE HAKI YA ELIMU KASKAZINI 'B' UNGUJA
Na Maryam Nassor
Mapambazuko yanapoanza katika baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Kaskazini
'B', Unguja, watoto wengi wa kike hawaanzi siku zao kwa kujiandaa kwenda skuli.
Badala yake huanza kwa kuchota maji, kufagia, kuosha vyombo, kupika na kulea
wadogo kabla ya kushika daftari.
Wengine hufika darasani wakiwa
wamechoka, huku wengine wakikosa masomo kabisa kwa sababu ya majukumu ya
nyumbani na shughuli za kilimo.
Haya ndiyo maisha ya watoto wengi wanaoishi katika mazingira magumu ya
kiuchumi na kijamii, ambako umaskini na mtazamo wa jamii vinaendelea kuwanyima
haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Ingawa elimu ni haki ya kila mtoto, watoto wa kike bado wanaathirika
zaidi kuliko wavulana. Mbali na kuhudhuria masomo, wanatarajiwa kutimiza
majukumu mengi ya kifamilia.
Wakati wa msimu wa kilimo, wengi
hushiriki kulima, kupanda, kupalilia na kuvuna mazao, hali inayowafanya kukosa
muda wa kujisomea na wakati mwingine kuacha shule kabisa.
Mkurugenzi wa Elimu Mbadala na Elimu ya Watu Wazima, Bi. Mashavu Ahmada
Fakih, anasema Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuwasaidia watoto na
vijana waliokatiza masomo kurejea katika mfumo wa elimu kupitia programu za
elimu mbadala.
Akizungumza wakati wa kukabidhi baiskeli kwa wanafunzi wa kituo cha elimu
mbadala Mkwajuni, alisema lengo ni kuwapa nafasi ya kujifunza kusoma, kuandika,
kufanya hesabu na kupata stadi za maisha zitakazowasaidia kujitegemea.
"Tunaamini kuwa ujuzi hauzeeki ,Hata waliokatiza masomo bado wana
nafasi ya kujifunza na kujenga maisha yao kupitia elimu na mafunzo ya
ujasiriamali," alisema.
Afisa Ustawi wa Jamii kutoka
Wilaya ya Kaskazini 'B Unguja Fatma Ussi' alisema changamoto kubwa ni baadhi ya
wazazi kutothamini elimu kwa kiwango kinachostahili. Kutokana na shughuli za
utalii na utafutaji wa kipato, baadhi ya familia huwahusisha watoto katika kazi
badala ya kuwahimiza kuendelea na masomo.
Alisema kuwa , kupitia kampeni za uhamasishaji katika shehia mbalimbali,
vijana wengi waliokuwa wamekatiza masomo wamejitokeza na sasa wanaendelea na
elimu pamoja na kujifunza stadi za maisha.
Mwalimu wa Skuli ya Msingi Mahonda, Abbass Hassan, alisema hali hiyo
inaonekana kila siku darasani. Muda wa masomo unafika baadhi ya wanafunzi bado
wako njiani hawajafika .
"Utamkuta mwanafunzi anafika saa mbili wakati vipindi tayari
vimeanza. Ukimuuliza sababu anasema alikuwa anaosha vyombo nyumbani. Hii
inaonesha kuwa mzigo wa kazi za nyumbani bado ni kikwazo kikubwa kwa elimu ya
mtoto wa kike," alisema.
Aliongeza kuwa , wazazi wanapaswa kuwapa watoto muda wa kutosha wa
kujifunza badala ya kuwabebesha majukumu yanayozidi uwezo wao.
Kwa upande wake, Sheha wa Donge Majenzi, Ali Keis Jailan, alisema bado
kuna haja ya kuendelea kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu, hasa kwa
watoto wa kike.
"Jamii bado haijabadilika vya kutosha. Tunahitaji kuwahamasisha
wazazi kutambua kuwa elimu ndiyo msingi wa maisha bora ya watoto wao,"
alisema.
Kwa Salha Muharam, safari ya elimu ilisimama baada ya kumaliza Kidato cha Nne kutokana na wazazi kushindwa kumudu gharama za masomo. Alibaki nyumbani akijishughulisha na kazi za nyumbani na kilimo kabla ya kujiunga na programu ya elimu mbadala.
"Nimepata nafasi nyingine ya kujifunza Leo ninaweza kusoma, kuandika
na nimejifunza ujasiriamali Nina
matumaini ya kujiajiri na kujitegemea," alisema.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010,
inaelekeza Serikali kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa sawa ya elimu bila
ubaguzi wa kijinsia.
Hata hivyo, takwimu zinaonyesha bado kuna changamoto. Ripoti ya UNICEF
kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar na NBS
inaonyesha kuwa mwaka 2021 asilimia 7.6 ya watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 17
walikuwa wakijihusisha na kazi. Aidha, asilimia 75.9 walikuwa wakifanya kazi za
nyumbani kama kupika, kufua, kusafisha nyumba na kulea watoto, jambo
linalopunguza muda wa kujifunza.
Mashirika ya kiraia pia yanaendelea kutetea haki ya mtoto wa kike kupata
elimu. Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Nairat Abdullah, alisema watoto wa kike
hukumbana na changamoto nyingi, zikiwemo umaskini, ukatili wa kijinsia na
ukosefu wa ulinzi, hivyo wanapaswa kupewa fursa ya kuendelea na elimu bila
vikwazo.
Alisisitiza kuwa, suluhisho si kuwapeleka watoto skuli pekee, bali ni kubadili mitazamo ya jamii kuhusu mgawanyo wa kazi za nyumbani na kuwajengea watoto mazingira salama ya kujifunza.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Uwezeshaji wa Jamii kwa Ajili ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii Kanisa
Katoliki Jimbo la Zanzibar, Sister Editha Asimwe, alisema wanaendelea kutoa
mafunzo ya uongozi na kwa viongozi wa
shehia na utawala bora kwa wananchi ili wajenge utamaduni wa maamuzi shirikishi
yanayolinda haki za watoto.
Naye Afisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Idara ya Maendeleo ya Kanisa
Katoliki Kanda ya Zanzibar, Msafiri Thomas Mombo, alisema mradi huo unalenga
kujenga mazingira wezeshi ya upatikanaji wa haki, kuweka Mazingira wezeshi ya elimu
Jumuishi na fursa za kiuchumi kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu,
wakiwemo, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Alisema kupitia mradi huo wameandaa mikakati ya kuwasaidia watoto wenye
Ulemavu kwa kuwapatia vifaa vya masomo na kuhamasisha jamii kuwekeza katika
elimu badala ya kuwategemea watoto katika shughuli za uzalishaji.
Post a Comment