ZAMECO YAWEKA MIKAKATI UPATIKANAJI WA SHERIA RAFIKI YA HABARI ZANZIBAR
Na Maryam Nassor
MWENYEKITI mpya wa
Kamati ya wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO), Abdallah Mfaume,
ameahidi kuimarisha ushirikiano na taasisi zinazounda umoja huo pamoja na
vyombo vya habari ili kuharakisha upatikanaji wa sheria mpya na rafiki ya
habari nchini.
Mfaume alitoa ahadi hiyo
baada ya kuchaguliwa kuiongoza kamati hiyo katika kikao kilichofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar
(TAMWA ZNZ ) huko Tunguu mkoa wa kusini Unguja.
Alisema uongozi wake ,utaendelea kushirikiana kwa karibu na waandishi wa habari pamoja na taasisi mbalimbali zinazounda ZAMECO ili kuhakikisha kunapatikana sheria itakayolinda na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.
"Ni wajibu wetu
kuendelea kushirikiana na wadau wote wa sekta ya habari ili kuhakikisha
Zanzibar inapata sheria mpya itakayokwenda sambamba na mazingira ya sasa ya
utendaji kazi wa vyombo vya habari," alisema Mfaume.
Naye Makamu Mwenyekiti wa
ZAMECO, Dk. Mzuri Issa, aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kuwa mstari
wa mbele kutetea maslahi ya waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.
"Kujitolea kwetu kupigania maslahi ya waandishi wa
habari na wananchi ni jambo la msingi na la kuigwa, Tunapaswa kuendelea
kushikamana ili kufanikisha kupatikana kwa sheria rafiki ya habari
nchini," alisema Dk. Mzuri.
Kwa upande wake, mjumbe wa ZAMECO, Salma Said, alisema kamati hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo vitisho kwa baadhi ya wanachama na uhaba wa rasilimali fedha unaokwamisha utekelezaji wa shughuli zake.
Hata hivyo, alisema
licha ya changamoto hizo, ZAMECO imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutetea
maslahi ya sekta ya habari na kuchochea maendeleo ya taaluma hiyo Zanzibar.
Naye mwandishi wa habari mkongwe na mjumbe wa ZAMECO, Salim Said aliipongeza ZAMECO kwa mchango wake katika kuendeleza mapambano ya kupatikana kwa sheria mpya ya habari.
Amesema kamati hiyo,
imefanya kazi kubwa kufikisha sauti ya waandishi wa habari ndani ya Baraza la
Wawakilishi, hatua aliyosema ni mafanikio makubwa katika harakati za muda mrefu
za kutetea uhuru wa habari.
"Hili si jambo
dogo , Waandishi wa habari tumetoka mbali kupigania sheria mpya na rafiki ya
habari, hivyo ni muhimu kuendelea kushikamana hadi lengo hilo litimie,"
alisema.
Aliwataka wajumbe wa
kamati hiyo, kuendelea kufanya utetezi kwa kukutana na Waziri mwenye dhamana ya
habari ili kueleza umuhimu wa kufanyika kwa marekebisho ya sheria hiyo.
"Sheria ya habari
inamhusu kila mwananchi, si waandishi wa habari pekee. Ndiyo maana tunapaswa
kuunganisha nguvu zetu na kuendelea kufanya utetezi hadi tupate sheria
inayokidhi mahitaji ya sasa," alisema.
Akifunga kikao hicho,
Mwenyekiti wa kikao, Bi. Shifaa Said, aliwataka wajumbe kuendelea kushirikiana
na kuimarisha mshikamano katika juhudi za kulinda uhuru wa habari na kuendeleza
taaluma ya uandishi wa habari Zanzibar.
Kikao hicho cha Kamati ya wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) kiliwakutanisha wajumbe wa kamati hiyo kwa lengo la kujadili mafanikio yaliyopatikana, changamoto zinazoikabili kamati hiyo pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha utendaji wake katika kutetea uhuru wa habari nchini.
Post a Comment