MSAADA WA KISHERIA: TUMAINI JIPYA KWA WANANCHI KUPATA HAKI ZAO
Na Maryam Nassor
Kwa miaka mingi, wananchi wengi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini
wamekuwa wakishindwa kupata haki zao kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo
umbali wa huduma za kisheria, gharama kubwa za kufuatilia kesi pamoja na uelewa
mdogo wa sheria.
Hali hiyo imekuwa ikichangia
migogoro mingi ya ardhi, ndoa, mirathi na hata vitendo vya ukatili wa kijinsia
kumalizwa kienyeji au kubaki bila kushughulikiwa.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuimarisha huduma za
msaada wa kisheria ili kuhakikisha wananchi wote, bila kujali mahali wanapoishi
au uwezo wao wa kifedha, wanapata haki kwa wakati, kwa usawa na kwa ufanisi.
Akizindua Awamu ya Pili ya Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya
Mama Samia katika Viwanja vya Maonesho Kizimbani Dole, Mkoa wa Mjini Magharibi
Unguja, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali
Mwinyi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu
Hassan, alisema Serikali itaendelea kuboresha huduma hizo ili kuwafikia
wananchi wengi zaidi.
Alisema kampeni hiyo inalenga kuondoa vikwazo vya umbali, gharama na
uelewa mdogo wa sheria kwa kupeleka huduma za msaada wa kisheria hadi katika
ngazi za kata, vijiji, mitaa na shehia.
Aidha, alisema mafanikio ya awamu ya kwanza ya kampeni hiyo yalionesha
umuhimu wa huduma hizo baada ya zaidi ya wananchi milioni nne kutoka Tanzania
Bara na Zanzibar kufikiwa na kunufaika nazo.
"Upatikanaji wa haki ni msingi wa utawala bora, amani na utulivu wa
taifa, Hivyo ni wajibu wa Serikali na wadau wote kuhakikisha huduma hizi
zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan wanaoishi maeneo ya pembezoni na
makundi maalumu," alisema Dk. Mwinyi.
Kauli hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha sheria hazibaki
vitabuni bali zinawafikia wananchi kwa vitendo kupitia elimu na usaidizi wa
kisheria.
Kwa upande wake, Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Mradi wa Uwezeshaji
wa Upatikanaji wa Haki na Utawala Bora wa Kanisa Katoliki Kanda ya Zanzibar kwa
ufadhili wa Misereor, Msafiri Thomas Mombo, alisema taasisi yao imekuwa ikishirikiana
na wasaidizi wa sheria (Paralegals) katika kutoa elimu ya haki za kisheria kwa
wananchi wa shehia tano ambazo ni shehia ya Mkataleni, Mahonda, Kitope, Donge
Majenzi, Bubwini Misufini zilizopo wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja.
Alisema, bado wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu namna ya
kudai haki zao na kupata misaada ya kisheria, jambo linalochangia baadhi ya
matukio ya ukatili na udhalilishaji kutoripotiwa katika vyombo vya sheria na
kusuluhishwa kwa njia zisizo za kisheria (Zisizo rasmi).
"Matukio mengi ya udhalilishaji hutokea katika maeneo ya vijijini
ambako jamii bado haina uelewa wa kuyafikisha kwenye vyombo vya sheria ili
hatua stahiki zichukuliwe. Elimu ndiyo silaha muhimu ya kubadilisha hali
hiyo," alisema Msafiri.
Kwa mujibu wake, elimu ya msaada wa kisheria imeanza kuleta mabadiliko
chanya kwa wananchi wengi ambao sasa wanaelewa mahali pa kupeleka malalamiko
yao na namna ya kupata msaada bila gharama kubwa.
Naye Sheha wa Shehia ya Mahonda, Ali Issa Kinole, alisema huduma za
msaada wa kisheria zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo, kwani
zimechangia kupungua kwa migogoro ambayo hapo awali ilichukua muda mrefu
kutatuliwa.
Alisema wananchi wengi sasa wanapata haki zao kupitia ushauri wa
wataalamu wa sheria na kuwataka wale wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali
kutafuta msaada mapema badala ya kusubiri migogoro kuwa mikubwa.
"Tumekuwa tukiwapa elimu wananchi wenye migogoro ya ardhi, ndoa,
mirathi pamoja na kesi za udhalilishaji ili watafute ushauri wa kisheria mapema
na haki ipatikane kwa wakati," alisema Kinole.
Kwa upande wake, Mratibu wa UN Women Kanda ya Zanzibar, Lucy Tesha,
alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuwawezesha wanawake na vijana kwa kuwapatia
elimu ya haki zao na namna ya kuzidai.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa wanawake na wasichana bado wanaendelea
kuwa waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo elimu ya
msaada wa kisheria ni nyenzo muhimu ya kuwapa ujasiri wa kuripoti matukio hayo
na kupata haki.
"Tunahitaji jamii inayowajengea uwezo wanawake na vijana kujua haki
zao na namna ya kuzitetea. Elimu hii ni muhimu katika kupunguza vitendo vya
ukatili na kujenga jamii yenye usawa," alisema Tesha.
Kauli hiyo inaungwa mkono na mwananchi wa Mahonda, Asya Bakar, ambaye
alisema elimu ya msaada wa kisheria inapaswa kuwa endelevu, hasa kwa vijana
ambao mara nyingi ndio waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili.
Alisema mara nyingi ,jamii husikia taarifa za watoto kubakwa au
kulawitiwa, lakini baadhi ya kesi hizo huishia kufichwa ndani ya familia
kutokana na uoga, mila au kutokujua taratibu za kisheria.
"Kila siku tunasikia taarifa za watoto kubakwa au kulawitiwa, lakini
kesi nyingi haziendi mahakamani kwa sababu baadhi ya familia hazina uelewa wa
kutosha kuhusu haki zao na namna ya kuzidai," alisema Asya.
Wadau wa sekta ya sheria wanaamini kuwa mafanikio ya kampeni ya msaada wa
kisheria yatategemea ushirikiano wa Serikali, viongozi wa jamii, taasisi za
kiraia pamoja na wananchi wenyewe katika kuhakikisha elimu hiyo inaendelea
kutolewa kwa makundi yote ya jamii.
Kwa kufanya hivyo, wananchi wengi zaidi wataweza kupata haki zao kwa
wakati, kupunguza migogoro inayoweza kuzuilika na kujenga jamii inayozingatia
misingi ya sheria, haki, usawa na utawala bora.
MWISHO
Post a Comment