VIJANA WAHAMASISHWA KUONGOZA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA

Na Maryam Nassor

VIJANA wa Vyuo Vikuu na shule za Sekondari Zanzibar wamehimizwa kuwa mstari wa mbele katika kupinga ukatili wa kijinsia na kuchukua nafasi za uongozi, wakitajwa kuwa nguzo muhimu ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Mradi wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Wasichana kutoka UN Women Kanda ya Zanzibar, Lucy Tesha, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika Tamasha la Sauti za Busara lililowashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu, lililofanyika Mpendae, Unguja.

Lucy amesema tamasha hilo ,limekusudia kuwajengea uwezo wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kuwapatia elimu kuhusu ukatili wa kijinsia pamoja na kuwahamasisha wanawake kujitokeza kugombea na kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

Amesema  kuwa, ushiriki wa vijana katika tamasha hilo ulikuwa mkubwa, huku wakishiriki kikamilifu katika maandalizi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za tamasha hilo.

"Lazima tukubali kuwa vijana ndio wenye nguvu za kuleta mabadiliko katika jamii na taifa kwa ujumla,  Ni muhimu kuwashirikisha katika kila sekta ili kuharakisha maendeleo," amesema Lucy.

Kwa upande wake, Mratibu wa Tamasha la Sauti za Busara Zanzibar, Zakia Lulu, amesema tamasha hilo linalenga kuwahamasisha wanawake na watoto wa kike kujenga uwezo wa uongozi kuanzia ngazi za chini, ikiwemo mashuleni, vyuoni na katika jamii.

"Tunataka watoto wa kike waanze kuchukua nafasi za uongozi wakiwa mashuleni au vyuoni. Wanapoona nafasi ya kuongoza wasisite kujitokeza," amesema Zakia.

Amesema, takwimu za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia bado zinatia wasiwasi, akieleza kuwa msichana mmoja kati ya watatu huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18, huku asilimia 17 ya wanawake nchini Tanzania wakikumbwa na aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia.

"Inaumiza kuona vitendo hivi vinaendelea , Kila mmoja ana wajibu wa kushiriki katika kuvikomesha , Ndiyo maana tumeona ni muhimu kuwafikia wanafunzi wa vyuo vikuu ili wajitambue na waweze kujikinga," amesema.

Aidha, amesema vijana wa shule za sekondari na vyuo vikuu ndio walio katika hatari zaidi ya kukumbana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kutokana na baadhi yao kuamini kuwa wana uwezo wa kujiamulia kila jambo bila kuzingatia athari zinazoweza kujitokeza.

Nao wanafunzi walioshiriki tamasha hilo,  Nadhra Juma  na Abuu Faidha Issa kutoka chuo cha Afya Mbweni Unguja , wamesema matamasha ya aina hiyo yana mchango mkubwa katika kuwapa vijana elimu muhimu kuhusu ukatili wa kijinsia pamoja na kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.

Wamesema vijana wengi wa vyuoni hukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri masomo na ndoto zao za baadaye, hivyo wamewashukuru waandaaji wa tamasha hilo kwa kuwapatia elimu itakayowasaidia kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji.

Tamasha la Sauti za Busara linafanyika Unguja na Pemba, likiwashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu na shule za sekondari, likibeba kaulimbiu isemayo "Mabadiliko Yanaanza na Mimi."


No comments

Powered by Blogger.