Vikundi vya Kijaluba Zanzibar vyageuza ujuzi kuwa fursa

NA MWANDISHI WETU,

Kikundi cha Tuwezeshwe chaanza kuvuna matunda ya juhudi zake baada ya kuuza vicha 420 vya mchicha na kupata mapato ya shilingi 420,000.

Kikundi cha Tuwezeshwe, miongoni mwa vikundi vya ujasiriamali vya KIJALUBA iSAVE, kimeonesha namna mafunzo ya ujasiriamali na stadi za uzalishaji yanavyoweza kubadilisha maisha ya wanakikundi na kufungua fursa za kujitegemea kiuchumi. Kikundi hicho kimefanikiwa kuvuna na kuuza vicha 420 vya mchicha kwa bei ya shilingi 1,000 kila kimoja, na kupata mapato ya jumla ya shilingi 420,000.

Mafanikio hayo yamebainika katika ziara ya ufuatiliaji iliyofanywa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na SHIJUWAZA, ZANAB na NAD-ZNZ katika Wilaya za Kusini, Kati na Kaskazini B, Unguja ambapo ziara hiyo ilihusisha vikundi 13 vya ujasiriamali vya KIJALUBA iSAVE, vikiwemo Mzuri Tupo, Maendeleo Mbele, Kawiya Ufike, Mtu ni Utu, Nia Njema, Tusafiane Nia, Jambo Nia, Upendo, Tunaweza, Jitihada, Mungu Tubariki na Tuwezeshwe. Lengo lilikuwa kutathmini maendeleo ya shughuli zao za kiuchumi, kubaini mafanikio na changamoto zinazowakabili pamoja na mahitaji yanayohitajika ili kuimarisha uzalishaji na uwezo wao wa kujitegemea.

Akielezea mafanikio hayo, Mshika Fedha wa Kikundi cha Tuwezeshwe, Salehe Mzee Ramadhani, amesema mapato waliyopata kutokana na mauzo ya mchicha yamewasaidia kugharamia mahitaji ya shughuli zao za kilimo, kuweka mtaji kwa ajili ya uzalishaji wa sabuni na mafuta, pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya mfuko wa kijamii wa kikundi.

“Tunafurahi kuona kuwa juhudi zetu zinaanza kuzaa matunda. Kupitia kilimo cha mchicha tumevuna vichwa 420 na kupata mapato ya shilingi 420,000. Fedha hizo zimetuwezesha kununua mahitaji ya shambani, kuweka mtaji kwa ajili ya uzalishaji wa sabuni na mafuta, na pia kutenga shilingi 182,000 kwa ajili ya mfuko wetu wa jamii. Hii inatupa moyo na kutuonesha kuwa tunaweza kuzalisha, kupata kipato, kuendeleza shughuli zetu na wakati huohuo kusaidiana kama wanakikundi,” alisema Salehe.

Hatua hiyo inaonesha namna vikundi vinavyoanza kutumia mapato yanayotokana na shughuli zao kuendeleza uzalishaji, kuongeza mitaji na kuweka mifumo ya kusaidiana. Kwa kufanya hivyo, wanakikundi wanajenga msingi wa shughuli endelevu za kiuchumi badala ya kutegemea vyanzo vya nje pekee.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikundi cha Mzuri Tupo, Nasra Nahoza, amesema mafunzo waliyopata yamewasaidia kuongeza ujuzi na kujiamini katika uzalishaji na uendeshaji wa biashara.

“Awali hatukuwa na ujuzi wa kutosha wa kutengeneza bidhaa wala kuendesha biashara. Kupitia mafunzo tuliyopata, sasa tuna maarifa na ujasiri wa kuzalisha bidhaa zetu, kutafuta wateja na kuziuza. Tunaweza kupata kipato na kutumia sehemu ya mapato kuendeleza shughuli zetu. Mafunzo haya yametufungua macho na kutuonesha kuwa tuna uwezo wa kujiajiri na kujitegemea kiuchumi,” alisema Nasra.

Katika ziara hiyo, ilibainika kuwa vikundi mbalimbali vimeanza kutumia ujuzi walioupata kuzalisha bidhaa na kufanya shughuli za kiuchumi kulingana na maeneo yao ya utaalamu. Bidhaa na shughuli hizo ni pamoja na utengenezaji wa sabuni, siagi ya mwili na mafuta ya nywele yatokanayo na mwani, batiki, kilimo cha mbogamboga na mazao mengine. Baadhi ya vikundi tayari vimeanza kuuza bidhaa zao na kutumia mapato yanayopatikana kununua malighafi na kuendeleza uzalishaji.

Akizungumzia maendeleo hayo, Afisa Mkuu wa Programu ya uwezeshaji kiuchumi kutoka TAMWA-ZNZ, Zaina Abdalla Mzee, amesema inatia moyo kuona wanakikundi wakitumia maarifa waliyopata kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuboresha ubora wa bidhaa na kutafuta masoko.

“Ni jambo la kutia moyo kuona wanakikundi wakitumia maarifa waliyopata kuanzisha shughuli za uzalishaji na kuanza kupata kipato. Tunawahimiza kuendelea kuboresha ubora wa bidhaa zao, kufanya ubunifu na kutafuta masoko ili kuongeza ushindani. Vilevile, ni muhimu kujenga utamaduni wa kujitegemea kwa kutumia uwezo na rasilimali walizonazo kutatua mahitaji ya vikundi badala ya kutegemea msaada wa nje kwa kila jambo,” alisema.

Pamoja na mafanikio hayo, ziara ilibaini changamoto mbalimbali zinazoathiri maendeleo ya shughuli za vikundi, zikiwemo upungufu wa masoko na wateja, uhaba wa vifaa vya uzalishaji pamoja na ukosefu wa maeneo yanayofaa kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiuchumi.

Vikundi vinavyojishughulisha na kilimo vilieleza mahitaji ya pampu za maji, mabomba ya umwagiliaji, mbolea na dawa za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao. Kwa upande mwingine, vikundi vinavyozalisha bidhaa mbalimbali vinahitaji vifaa vya uzalishaji, mizani, mashine za kushonea, pamoja na kuboresha vifungashio na utambulisho wa bidhaa zao ili kuongeza ubora na kuvutia wateja.

Programu ya CADiR (Collective Actions for Disability Rights) inatekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na wadau wake ina lengo la kuimarisha ushiriki wa wanawake, wanaume na hasa watu wenye ulemavu katika shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za kujipatia kipato na kujenga uwezo wa kujitegemea.

 

No comments

Powered by Blogger.