TAMWA-ZNZ YAANZA MCHAKATO WA KUTHIBITISHA SERA YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI NA FARAGHA

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimeanza mchakato wa kuthibitisha Sera ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Faragha (Data Protection and Privacy Policy) kupitia mkutano wa mashauriano na wadau uliofanyika Novemba 13, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mifumo ya taasisi katika kuhakikisha taarifa binafsi zinakusanywa, zinachakatwa, zinahifadhiwa na kutumiwa kwa kuzingatia misingi ya usalama, usiri na faragha.
Sera
hiyo inalenga kuweka mwongozo rasmi wa namna ya kusimamia na kulinda taarifa
zinazopatikana katika utekelezaji wa shughuli za TAMWA-ZNZ, zikiwemo taarifa za
wafanyakazi, wanufaika wa miradi, washirika na wadau. Aidha, itaweka utaratibu
wa uwajibikaji katika matumizi na usambazaji wa taarifa hizo ili kuzuia
uvujaji, matumizi yasiyoidhinishwa na ukiukwaji wa haki za faragha za wamiliki
wa taarifa.
Akielezea
sababu za kuandaa sera hiyo, Sabrina Mwintanga, Afisa Programu kutoka
TAMWA-ZNZ, amesema hatua hiyo imetokana na dhamira ya taasisi kuimarisha mifumo
yake ya kiutendaji kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia
ulinzi wa taarifa binafsi.
Amesema
katika utekelezaji wa programu na miradi yake, TAMWA-ZNZ hukusanya taarifa za
makundi mbalimbali katika jamii, hivyo ni muhimu kuwa na mwongozo unaoelekeza
namna taarifa hizo zinavyopaswa kushughulikiwa katika kila hatua.
“Tumeliona
suala la ulinzi wa taarifa binafsi kuwa muhimu kutokana na aina ya shughuli
tunazozitekeleza na makundi mbalimbali tunayofanya nayo kazi. Ni wajibu wetu
kuhakikisha taarifa tunazokusanya zinalindwa na kutumiwa kwa madhumuni
yaliyokusudiwa. Sera hii itatuwezesha kuwa na utaratibu ulio wazi wa
ukusanyaji, uhifadhi, matumizi na ushirikishwaji wa taarifa hizo kwa kuzingatia
usiri, usalama na haki za wamiliki wa taarifa,” amesema Sabrina.
Ameongeza
kuwa sera hiyo itasaidia kujenga utamaduni wa uwajibikaji miongoni mwa
wafanyakazi na kuimarisha uaminifu kati ya taasisi na wadau wake, hususan
makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, yakiwemo wanawake, watoto, manusura
wa ukatili wa kijinsia na watu wenye ulemavu.
Kwa
upande wake, Hijja Shamte Abdalla, Afisa Uhusiano na Utetezi kutoka Shirika la Jumuiya
za Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA), amesema uwepo wa sera hiyo ni
muhimu katika kulinda haki, utu na faragha za watu wenye ulemavu, ambao taarifa
zao binafsi hukusanywa na taasisi mbalimbali wakati wa utekelezaji wa programu
za maendeleo.
Amesisitiza
umuhimu wa kuhakikisha taarifa hizo zinashughulikiwa kwa usiri na usalama ili
kuepusha matumizi au usambazaji unaoweza kuhatarisha haki na usalama wao.
Naye
Hassan Saidi Salum kutoka Mwavuli wa Asasi za Kiraia Zanzibar ANGOZA amesema
taarifa binafsi ni rasilimali yenye thamani inayopaswa kulindwa, hivyo uwepo wa
sera hiyo utaiwezesha TAMWA-ZNZ kuimarisha mifumo yake ya ndani, kuongeza
uwajibikaji na kujenga imani kwa watu na taasisi zinazoshirikiana nayo.
Akichangia
katika mkutano huo, Salum Suleiman Ali, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha
Zanzibar (SUZA) na mwakilishi katika masuala ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na
Faragha, amesema ulinzi wa taarifa unapaswa kuzingatiwa katika shughuli zote za
taasisi, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kiteknolojia, usimamizi wa nyaraka na
mahusiano ya kikazi.
Ameeleza
kuwa taarifa binafsi zinahitaji kulindwa katika mzunguko wake wote, kuanzia
ukusanyaji, uchakataji na matumizi hadi uhifadhi, ushirikishwaji au uondoaji
wake kwa mujibu wa taratibu husika. Ameongeza kuwa mkutano huo ni sehemu ya
hatua ya uthibitishaji wa wadau (Stakeholders Validation), inayolenga kupata
maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuhakikisha rasimu ya sera inakidhi
mahitaji ya kiutendaji na kuzingatia misingi ya kisheria.
Tanzania ina Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 (Personal Data Protection Act, 2022), Na. 11 ya mwaka 2022, iliyotungwa kwa lengo la kulinda haki ya faragha ya watu binafsi kwa kuweka utaratibu wa kisheria unaosimamia ukusanyaji, uchakataji, matumizi na uhifadhi wa taarifa binafsi. Sheria hiyo pia ilianzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Commission – PDPC) kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wake. Sheria hiyo ilianza kutumika rasmi Mei 1, 2023, na juhudi za TAMWA-ZNZ kuandaa sera yake ya ndani ni sehemu ya kuimarisha mifumo ya taasisi katika kuzingatia matakwa ya kisheria na kuhakikisha taarifa za wafanyakazi, wanufaika na wadau wake zinalindwa dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa na ukiukwaji wa faragha.
Mkutano huo uliwakutanisha wadau kutoka taasisi mbalimbali, zikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Zanzibar University (ZU), Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Zanzibar (THRDC), SHIJUWAZA, ANGOZA, ZYF, PYI, TAMWA-ZNZ Pamoja na wadau wengine.

Post a Comment