ZEEA KUIFIKIA JAMII KUTOA ELIMU YA MIKOPO YA 4-4-2


Na Maryam Nassor

MATOKEO BAADA YA STORY ZANGU,    MAKALA ZILITOKA  KATIKA  GAZETI LA ZANZIBAR LEO NA BLOG YA ZENJI POST  TAREHE  18.JULAY 2026,  28, AGOSTI 2026 NA 2, SEPTEMBA 2026. 
 
BAADA YA MAKALA HIZO KUTOKA KATIKA VYOMBO HIVYO, MAMLAKA YA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI   ZANZIBAR ( ZEEA )  ILISEMA IMESIKIA MALALAMIKO YA WANACHI NA KUAHIDI KUANZIA MWEZI  HUU WA OKTOBA -DISEMBA WATAANZA KUTOA ELIMU YA MIKOPO HIYO, KATIKA WILAYA ZOTE ZA UNGUJA NA PEMBA NA KILA MWEZI WATATEMBELEA SHEHIA TATU. 

MAMLAKA ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) imejipanga kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kunufaika na mikopo inayotolewa na mamlaka hiyo, kufuatia changamoto zilizobainishwa kuhusu uelewa mdogo wa wananchi juu ya fursa hizo.

Hatua hiyo inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan wale ambao wamejisajili katika mfumo wa mikopo lakini bado hawajapata elimu ya kutosha kuhusu taratibu za kuipata na namna ya kunufaika nayo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa ZEEA, Gharib Salum Gharib  huko katika ofisi ya Mamlaka hiyo Kilimani Unguja, amesema mamlaka hiyo imepanga kutembelea shehia mbalimbali kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka huu ili kutoa elimu na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi.

Amesema ,katika utekelezaji wa mpango huo, ZEEA itaanza kwa kutembelea shehia tatu kila mwezi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mikopo ya kuwawezesha kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mfumo wa 4-4-2.

Kwa mujibu wa Gharib, hatua hiyo imekuja baada ya mamlaka hiyo kusikiliza changamoto zinazowasilishwa na wananchi kuhusu upatikanaji wa mikopo hiyo, hivyo kuona umuhimu wa kuwafikia moja kwa moja na kuwapa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu huduma hiyo.

Amesema pamoja na kuendelea kutoa mikopo isiyo na riba, ZEEA imeamua kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa kutumia njia mbalimbali, zikiwemo vyombo vya habari na kutembelea masoko, ili kuhakikisha taarifa kuhusu fursa hizo zinawafikia wananchi wengi zaidi.

“Licha ya kuendelea kutoa huduma ya mikopo ambayo haina riba, tumeanza pia kuwafikia wananchi ili kuwapa elimu kuhusu mikopo hiyo,” amesema Gharib.

 Semeni   Bundala   mkaazi wa shehia  ya Mahonda ,  amesema   Mpango wa ZEEA wa kwenda shehia kwa shehia utatoa nafasi ya kuwafikia wananchi moja kwa moja, kusikiliza changamoto zao na kuongeza uelewa kuhusu namna ya kunufaika na mikopo hiyo.

Hatua hiyo imekuja , kufuatia Makala zilizoandikwa  na gazeti la Zanzibar  leo  kuhusu changamoto zinazowakabili wananchi kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu mikopo ya ZEEA, ambapo ilibainika kuwa baadhi ya wananchi wamejisajili katika mfumo lakini bado hawajafikiwa na taarifa za kutosha kuhusu fursa hiyo.

 

No comments

Powered by Blogger.