WATOTO WA KIKE WATAKIWA KURIPOTI MAPEMA VITENDO VYA UDHALILISHAJI
Na Maryam Nassor
WATOTO wa kike wametakiwa kutoa taarifa mapema wanapoona
viashiria vya vitendo vya udhalilishaji ili kujikinga na vitendo hivyo na
waweze kutimiza ndoto zao za kielimu.
Wito huo umetolewa na Bi Sabah Bakari Hassan, Mwanaharakati wa kupinga vitendo vya Udhalilishaji wakati
akizungumza na wanafunzi wa Skuli ya Dunga, Wilaya ya Kati, Unguja, ambapo
amewahimiza watoto wa kike kujiamini, kujitambua na kutumia fursa zinazotolewa
na Serikali kufikia malengo yao.
Amesema, watoto wa kike wana nafasi kubwa katika
maendeleo ya nchi, hivyo wanapaswa kujitambua na kujiamini ili waweze kufikia
ndoto zao na kuwa viongozi bora wa baadaye.
Ameeleza kuwa, ni muhimu watoto wa kike kujilinda dhidi
ya vitendo vya udhalilishaji, akisisitiza kuwa ulinzi wao ni msingi muhimu wa
kuwawezesha kuendelea na masomo na kushiriki katika maendeleo ya jamii.
Akizungumzia nafasi ya wanawake katika uongozi, Bi Sabah amesema watoto wa kike wanapaswa kuanza kushiriki katika shughuli za uongozi mapema ili kuwajengea uwezo wa kujiamini na hatimaye kushika nafasi mbalimbali za maamuzi wanapokuwa watu wazima.
Kwa upande wake, Afisa kutoka Chama cha Waandishi wa
Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Asya Hakim, amesema ziara hiyo
katika skuli za Wilaya ya Kati na Kaskazini Unguja inalenga kutoa elimu kwa
watoto kuhusu namna ya kujikinga na vitendo vya udhalilishaji.
Amesema katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike
Duniani, wamefikia skuli nne za msingi, ambapo mbili zipo Wilaya ya Kaskazini
‘A’ na nyingine mbili Wilaya ya Kati, Unguja.
“Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani,
tumeona ni vizuri kuwafikia watoto wa kike mashuleni na kuwapa elimu kuhusu
namna wanavyoweza kujikinga na vitendo vya udhalilishaji ili waweze kutimiza
ndoto zao,” amesema Asya.
Naye M’baya Ali Haji, kutoka Ofisi ya Baraza la Taifa la
Watu Wenye Ulemavu, amesema jamii ina wajibu wa kushirikiana kuweka mazingira
wezeshi kwa watoto wa kike ili waweze kufikia malengo yao.
Amesema ili watoto waweze kutimiza ndoto zao, wanapaswa
kuheshimiana na kuzingatia haki za kila mtoto, wakiwemo watoto wenye ulemavu,
ili kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayebaguliwa au kunyimwa fursa za maendeleo.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya
Kati, Unguja, Ali Shehe Kombo, amesema haki za msingi za watoto ni pamoja na
kupata elimu bora na malezi yanayochangia kuimarisha ulinzi na usalama wao.
Amesema ni wajibu wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla
kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya vitendo vya udhalilishaji ili waweze
kuendelea na masomo yao na kutimiza ndoto zao za kuwa viongozi bora wa sasa na
baadaye.
Akizungumzia hali ya usalama wa watoto wilayani humo, amesema katika mwezi huu zimeripotiwa kesi
mbili za watoto kutoroka nyumbani na kwenda kusikojulikana.
Kutokana na hali hiyo, amewasihi watoto wa kike kuwa
makini na vishawishi vinavyoweza kuhatarisha usalama wao, badala yake waweke
kipaumbele katika masomo ili kufikia malengo yao ya kielimu.
Aidha, ameeleza kuwa wazazi na walezi wanaendelea kufanya juhudi za kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo vya udhalilishaji, huku akiwataka watoto kuwa na ushirikiano na wazazi na walezi wao ili kwa pamoja waweze kuimarisha ulinzi na usalama wao.

TAMWA-ZNZ, kwa kushirikiana na wadau wengine wanaopinga udhalilishaji,
imeendelea kutoa elimu kwa wanafunzi wa skuli za msingi za Dunga na Bambi,
Wilaya ya Kati, Unguja, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike
Duniani. Ikiwa na kauli mbiu ya “ komesha mimba
za Utotoni na wekeza katika haki za Watoto
wa kike”



Post a Comment