SMZ IPO TAYARI KUSHIRIKIANA NA WANAHABARI KUTOKA OMAN

NA MARYAM NASSOR
SERIKALI ya
Mapinduzi ya Zanzibar imesema ipo tayari kushirikiana na wanahabari wa Oman
katika kuandaa maudhui yanayolenga kuimarisha
diplomasia ya Habari ya habari, utamaduni na utalii, kati ya Zanzibar na Oman.
Ameyasema hayo, Waziri wa Habari, Sanaa,
Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma, wakati akihutubia katika kongamano la Jukwaa
la waandishi wa Habari wa Oman na
Zanzibar.
Amesema,
ushirikiano huo unaweza kuhusisha utayarishaji wa vipindi maalumu vya utamaduni
vitakavyorushwa kupitia vyombo vya habari vya Zanzibar na Oman, ikiwemo
televisheni na redio.
Amesema
maudhui hayo yatasaidia kuonesha historia, utamaduni, urithi na fursa za utalii
zilizopo katika pande hizo mbili, huku akiwataka wanahabari kutumia nafasi hiyo
kuandika habari zinazojenga uelewa na kuimarisha mahusiano ya watu wa Zanzibar
na Oman.
Dkt. Riziki pia amewataka wanahabari kuzingatia maadili ya taaluma, kufanya uchunguzi na kuhakiki taarifa kabla ya kuzisambaza, akisema kasi ya teknolojia na mitandao ya kijamii isitumike kama sababu ya kusambaza taarifa zisizo sahihi.

Kwa upande
wake, Balozi Mdogo wa Oman Zanzibar, Said bin Salim Al Sinawi, amesema mkutano
huo ni fursa ya kuimarisha ushirikiano wa vyombo vya habari na kujenga uelewa
wa pamoja kuhusu historia na maisha ya watu wa Zanzibar na Oman.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari Oman, Dkt. Mohammed bin Mubarak Al Araimi,
amesema wanahabari wana nafasi kubwa katika kuhifadhi historia na kujenga
daraja kati ya jamii hizo mbili, huku akipendekeza kuwepo kwa mafunzo ya
pamoja, kubadilishana uzoefu na kuandaa habari za pamoja.
Naye Mwenyekiti wa Zanzibar Press Club, Abdalla Mfaume, amesema ushirikiano huo unapaswa kuwa wa muda mrefu na kuhusisha mafunzo, tafiti, warsha na miradi ya pamoja ya habari, akisisitiza kuwa vyombo vya habari vinaweza pia kukuza utalii, utamaduni, biashara na uwekezaji kati ya Zanzibar na Oman.


Aidha katika kongamano hilo, waandishi wa habari wa Zanzibar walisaini makubaliano maalum ya mashirikiano kati ya waandishi wa habari wa Zanzibar na wenzao wa kutoka Oman na kuahidi kuendelea kushirikiana.
Post a Comment