Uchaguzi 2025 wafichua pengo la wanawake Zanzibar -Ushindi wa wanawake katika majimbo umeshuka kutoka wanane mwaka 2020 hadi wanne mwaka 2025, huku mjadala wa 50/50 ukielekezwa kwenye vyama, rasilimali na mazingira ya kisiasa


Na Maryam Nassor

Katika majimbo 50 ya uchaguzi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wanawake wanne pekee ndio waliofanikiwa kushinda moja kwa moja katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, idadi inayowakilisha asilimia nane ya wajumbe wanaochaguliwa katika majimbo.

Takwimu hiyo ni nusu ya iliyorekodiwa mwaka 2020, ambapo wanawake wanane, sawa na asilimia 16, walishinda moja kwa moja kati ya majimbo hayo 50.

Orodha rasmi ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ya Novemba 2025 inawataja Badria Atai Masoud wa Jimbo la Kijini, Mboja Ramadhan Mshenga wa Mahonda, Mwanaasha Khamis Juma wa Chukani na  Zawadi Amour Amour Nassor   wa jimbo la Konde  kuwa miongoni mwa wajumbe waliochaguliwa majimboni.

Hali hiyo imefungua upya mjadala kuhusu nafasi ya wanawake katika siasa za Zanzibar, hasa tofauti kati ya uwakilishi unaopatikana kupitia viti maalum na uwezo wa wanawake kushinda katika ushindani wa moja kwa moja wa majimbo.

Swali linalojitokeza ni iwapo mifumo iliyopo inatosha kuifikisha Zanzibar kwenye usawa wa kijinsia katika uongozi, au kama kuna haja ya kufanya mabadiliko zaidi ndani ya vyama vya siasa, sheria na mazingira ya uchaguzi.

Haki ya kushiriki siasa ipo, lakini ushindani bado una changamoto

Ushiriki wa wanawake katika uongozi si suala la hisani. Tanzania imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW), ambao kupitia Ibara ya 7 unatambua haki ya wanawake kushiriki katika maisha ya kisiasa na ya umma, ikiwa ni pamoja na kupiga kura, kugombea nafasi za kuchaguliwa na kushika madaraka ya umma kwa masharti sawa na wanaume.

Kwa upande wa kikanda, Itifaki ya SADC kuhusu Jinsia na Maendeleo inaweka mkazo katika uwakilishi na ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi. SADC pia imeweka lengo la kufikia angalau asilimia 50 ya wanawake katika nafasi za maamuzi ifikapo mwaka 2030.

Katika ufuatiliaji wake wa utekelezaji wa Itifaki hiyo, SADC imeendelea kusisitiza umuhimu wa hatua maalum, marekebisho ya mifumo ya vyama na kuondolewa kwa vikwazo vinavyowazuia wanawake kugombea nafasi za kuchaguliwa.

Kwa Zanzibar, Katiba imeweka mfumo wa viti maalum vya wanawake ndani ya Baraza la Wawakilishi kama hatua maalum ya kuongeza uwakilishi wao. Katiba ya Zanzibar inaeleza utaratibu wa uwakilishi wa wanawake kupitia vyama vinavyopata viti katika majimbo.

Baada ya uchaguzi wa 2025, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar iliteua wanawake 20 katika viti maalum, ambapo 16 ni kutoka CCM na wanne kutoka ACT-Wazalendo.

Hivyo, mjadala wa uwakilishi wa wanawake hauwezi kuishia kwenye idadi ya wanawake wanaoshinda majimboni pekee. Unahitaji pia kuangalia namna mfumo wa viti maalum unavyosaidia kuongeza uwakilishi, pamoja na sababu zinazofanya wanawake wachache wafanikiwe katika ushindani wa moja kwa moja.

Wanawake: Rasilimali na mitazamo bado ni vikwazo

Mboja Ramadhan Mshenga, mmoja wa wanawake wanne walioshinda jimbo katika uchaguzi wa 2025, anaamini uwezo wa wanawake wa kuongoza si tatizo, bali mazingira ya kisiasa yanayowazunguka.

“Wanawake huwa tunajitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi kwa sababu tunao uwezo, lakini wengi hawapewi nafasi ya kugombea na matokeo yake hatufikii usawa wa kijinsia,” anasema.

Kwa mtazamo wake, gharama za kampeni, upatikanaji wa rasilimali na mitazamo ya jamii kwamba uongozi ni jukumu la wanaume, ni miongoni mwa vikwazo vinavyoweza kupunguza nafasi ya wanawake katika ushindani wa majimbo.

“Bado wanawake hatujaweza kuongoza kwa usawa katika nafasi za majimbo. Zanzibar ina majimbo 50, wanawake kupata majimbo manne, bado tuko mbali katika safari ya kufikia 50/50,” anasema.

Hoja ya rasilimali pia imejitokeza katika mjadala mpana wa ushiriki wa wanawake katika uchaguzi. Mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya vyama unaweza kuamua kwa kiasi kikubwa ni wanawake wangapi wanafikia hatua ya kushindana katika uchaguzi wenyewe.

Upinzani: Hofu na ukosefu wa rasilimali

Kiongozi wa Wanawake wa Alliance for Democratic Change (ADC), Nadhira Ali Haji, anasema wanawake wanaotaka kuingia katika siasa, hukutana na changamoto zinazohusisha rasilimali, elimu ya kisiasa, uungwaji mkono kutoka ndani ya vyama na jamii, pamoja na hofu inayoweza kujengwa na mazingira ya kisiasa.

“Kiukweli tunataka kugombea katika majimbo, lakini kwa vyama vya upinzani inakuwa vigumu kutokana na siasa zilizopo hapa Zanzibar. Hofu na ukosefu wa rasilimali ni kikwazo kikubwa, hususani kwa wanawake,” anasema.

Nadhira anaongeza kuwa baadhi ya wanawake wanaojitokeza kugombea hukutana na kubezwa, vitisho au kukatishwa tamaa na watu wa karibu, hali ambayo inaweza kuwafanya baadhi yao kujiondoa katika mchakato wa kisiasa.

“Usawa wa kijinsia si ombi, ni haki ya wanawake ambayo imechelewa kutimizwa,” anasisitiza.

Hoja hizo zinaendana kwa kiasi na changamoto zilizoainishwa katika tathmini za ushiriki wa wanawake Zanzibar, ambazo zimehusisha mitazamo ya kijamii, upatikanaji wa rasilimali na mazingira ya kisiasa miongoni mwa vikwazo vya ushiriki wao katika uongozi.

UN Women imeeleza kuwa pengo la kijinsia katika nafasi za maamuzi bado ni eneo linalohitaji hatua zaidi.

Sera zipo, utekelezaji ndio mtihani

  UN Women inaeleza kuwa ,sera na mikakati ya usawa wa kijinsia ni sehemu ya juhudi za kukuza maendeleo jumuishi Zanzibar.

Changamoto, si kuwepo kwa sera pekee, bali namna zinavyotekelezwa na kama zinabadilisha mazingira halisi ambayo wanawake hukutana nayo wanapotaka kugombea nafasi za uongozi.

Mchambuzi wa masuala ya wanawake na uongozi, Almasi Mohd, anasema maendeleo ya Zanzibar hayawezi kuwa jumuishi iwapo wanawake wataendelea kuwa na uwakilishi mdogo katika meza za maamuzi.

“Zanzibar haiwezi kufikia dira ya maendeleo bila kuwapa wanawake nafasi sawa mezani katika meza ya maamuzi,” anasema.

Kwa mtazamo wake, matokeo ya uchaguzi wa 2025 hayapaswi kuangaliwa kama takwimu za uchaguzi pekee, bali kama ishara inayohitaji mjadala mpana kuhusu mifumo inayowezesha au kuzuia wanawake kushindana katika nafasi za uongozi.

Mabadiliko yaanzia ndani ya vyama

Mwaka 2024, TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Zanzibar Female Lawyers Association (ZAFELA), Pemba Environment and Gender Advocacy Organization (PEGAO) na Association of Women with Disabilities Zanzibar (JUWAUZA) ilizindua pendekezo la Gender Policy and Gender Desk Framework for Political Parties, likilenga kuhimiza vyama vya siasa kuweka mifumo ya kukuza usawa wa kijinsia.

Pendekezo hilo liliweka mkazo katika kuondoa vikwazo vinavyowakabili wanawake ndani ya vyama na kuongeza fursa zao za kushiriki katika uongozi na uchaguzi.

 Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania ( UWT)  kutoka Chama cha Mapinduzi  Salma Said, anasema   mradi wa SWIL umesaidia  vyama vya siasa  kuanzisha sera  na madawati ya kijinsia  ili kuhamasisha  wanawake kugombea nafasi za uongozi .

Mashavu Bakar Mgombea Ubunge jimbo la Chumbuni  kwa tiketi ya  ACT-Wazalendo anasema vyama vya siasa bado vinapaswa kuonesha utayari zaidi wa kuwekeza  kwa wanawake  ili kuwe na  ushindani katika majimbo.

Maandalizi ya wanawake nayo ni muhimu

Afisa Programu wa mradi wa Strengthening Women in Leadership (SWIL) wa TAMWA-ZNZ, Khairat Ali, anasema mitazamo ya kitamaduni inayochukulia siasa kama eneo la wanaume bado ni changamoto kwa wanawake wanaotaka kuingia katika uongozi.

Anasema programu hiyo imekuwa ikitoa mafunzo kwa wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa kwa lengo la kuongeza uwezo wao wa kushiriki katika nafasi za uongozi na michakato ya kidemokrasia.

 Mradi wa SWIL , inalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na michakato ya kidemokrasia Zanzibar, huku ikihusisha mafunzo, uhamasishaji na juhudi za kuboresha mazingira ya ushiriki wa wanawake.

Hata hivyo, kuongeza idadi ya wanawake wanaojitokeza kugombea hakutoshi. Wanahitaji pia maandalizi katika maeneo kama uongozi, sheria, mawasiliano ya kisiasa, kampeni, uhamasishaji wa wapiga kura na utafutaji wa rasilimali.

50/50: Nini kifanyike?

Matokeo ya uchaguzi wa 2025 yanaonesha kuwa mfumo wa sasa bado haujawawezesha wanawake kufikia uwiano wa karibu na wanaume katika ushindani wa moja kwa moja wa majimbo.

Hatua ya kwanza inaweza kuwa vyama vya siasa kuweka malengo yanayopimika ya kuongeza idadi ya wanawake wanaopitishwa kugombea majimbo, badala ya kutegemea viti maalum kama njia kuu ya kuongeza uwakilishi.

Pili, kuna haja ya kuendelea kutathmini sheria na taratibu za uchaguzi na uteuzi wa wagombea ili kubaini vikwazo vinavyoweza kuwazuia wanawake wenye uwezo kushindana kwa usawa.

Tatu, uwekezaji katika mafunzo ya uongozi unapaswa kuendelea, ukiwalenga pia wanawake vijana na wale wanaotoka katika maeneo ambayo fursa za kisiasa ni chache.

Nne, suala la rasilimali linahitaji mjadala wa wazi. Gharama za kushiriki katika siasa zinaweza kuwa kikwazo kwa mgombea mwenye uwezo iwapo hana mtandao wa kifedha au msaada wa kutosha wa chama.

Tano, usalama na mazingira ya kisiasa yanahitaji kupewa uzito. Wanawake wanaogombea wanapaswa kuwa na mazingira yanayowaruhusu kushiriki katika siasa bila vitisho, vitisho vya kijinsia, unyanyasaji au kampeni za kuwakatisha tamaa.

Mwisho, jamii nayo ina wajibu wa kubadili mitazamo inayohusisha uongozi na wanaume pekee. Uongozi unapaswa kupimwa kwa uwezo, uadilifu, uwajibikaji na utendaji, si kwa jinsia ya anayeshika nafasi.

Safari bado ni ndefu

Uchaguzi wa 2025 umeweka wazi pengo linaloendelea kuwepo kati ya lengo la usawa wa kijinsia na uhalisia wa ushindani wa kisiasa Zanzibar.

Wanawake wanne kati ya majimbo 50, sawa na asilimia nane, ni hatua muhimu kwa wale waliofanikiwa kushinda. Lakini ikilinganishwa na wanawake wanane walioshinda majimbo mwaka 2020, takwimu ya 2025 inaonesha kupungua kwa asilimia nane katika uwakilishi wa moja kwa moja, kutoka asilimia 16 hadi asilimia nane.

Kwa hiyo, mjadala wa 50/50 haupaswi kuangalia idadi ya wanawake waliopo katika Baraza pekee. Unapaswa pia kujiuliza wanawake wanafikiaje nafasi hizo, ni wangapi wanapewa nafasi ya kushindana moja kwa moja, na ni vikwazo gani vinavyowazuia wengine kufika huko.

SADC inaendelea kusukuma lengo la angalau asilimia 50 ya wanawake katika nafasi za maamuzi ifikapo 2030. Zanzibar ina mifumo ya kikatiba, sera na taasisi zinazotambua umuhimu wa ushiriki wa wanawake.

Kwa Zanzibar, safari ya 50/50 bado haijafika mwisho. Uchaguzi wa 2025 umeongeza sababu ya kuuliza si tu wanawake wangapi wameingia katika uongozi, bali pia kwa nini wanawake wengi zaidi hawajafika katika nafasi za ushindani wa moja kwa moja, na nini kifanyike kubadili hali hiyo.

 

No comments

Powered by Blogger.